Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hon. Tundu Antiphas Mughwai Lissu

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

MHE. TUNDU A. M. LISSU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia. Naomba niseme kwamba nitachangia hoja ya Kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Tume ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe, kati ya Tanzania na Malawi. Kwa sababu ya muda naomba nijielekeze kwenye suala moja tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkataba kati ya Tanzania na Malawi juu ya Bonde la Mto Songwe ni Mkataba wa Kimataifa, it is an International Treaty, tuanzie hapo. Ni mkataba wa Kimataifa kati ya nchi mbili. Pili, kwa vile ni mkataba wa Kimataifa, mkataba wa Kimataifa huu kama kuna sheria nyingine yoyote ya Tanzania inayokwenda kinyume na matakwa ya mkataba huu wa Kimataifa, mkataba wa Kimataifa unasimama sheria ya nchi inatanguka, basic International Law 101. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, kitu ambacho ni muhimu sana na ambacho tunahitaji majibu ya Serikali kuhusiana na mkataba huu wa Kimataifa ni ule unaohusu utaratibu wa utatuaji wa migogoro chini ya mkataba huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Ibara ya 13(3) ya mkataba huu, The Songwe River Basin Convention, endapo kutakuwa na mgogoro kati ya Tanzania na Malawi ambao ndiyo wahusika wa mkataba huu, endapo kutakuwa na mgogoro kuhusiana na masuala mbalimbali yanayohusiana na mkataba huu wa Kimataifa, Ibara ya 13(3) inasema mgogoro huo utapelekwa kwenye Mahakama ya SADC; the parties shall refer the matter to the SADC Tribunal or shall appoint an adhoc arbitrator through mutual agreement which shall be in writing. The arbitrator’s decision shall be final and binding on the parties.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikipelekwa kwenye Mahakama ya SADC au ikapelekwa kwa msuluhishi wa Kimataifa, uamuzi wa Mahakama ya SADC au uamuzi wa huyu msuluhishi wa Kimataifa utakuwa ni wa mwisho na utatufunga sisi pamoja na Malawi, sasa shida iko hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkataba wa Bonde la Mto Songwe unahusu rasilimali ya maji, unahusu acquatic resources, unahusu water resources, unahusu lakes, unahusu rivers. Haya yote niliyoyataja yanajulikana katika sheria, ile sheria ilipitishwa kwa shamrashamra sana humu ndani, ile sheria ya kutangaza mamlaka ya kudumu ya utajiri wa nchi; The Natural Wealth and Resources Permanent Sovereignty Act iliyopitishwa hapa mwezi Julai. Sheria ile imesema, hizo nilizozisema, rasilimali za maji, vile vitu vilivyoko kwenye maji, samaki and so on and so fourth, lakes, rivers, everything, kifungu cha 11 cha sheria ile kimesema kwamba ni marufuku kwa rasilimali hizi zilizotajwa kuamuliwa nje ya Mahakama za Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba na Waheshimiwa Wajumbe wajiridhishe wakaangalie kifungu cha tatu cha sheria ile, waangalie na kifungu cha 11(1), (2) na (3) cha sheria ile ili wajiridhishe juu ya hiki ninachokisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo letu la miaka yote na tatizo letu hasa la Bunge hili ni ushabiki usiokuwa na maana yoyote. Tumeruhusu Bunge linapitisha sheria za mambo makubwa bila kuzitafakari, matokeo yake ndiyo haya. Sasa tuna mkataba wa Kimataifa unaosema rasilimali zetu za maji, maziwa, mito, kuhusiana na Bonde la Mto Songwe zitaamuliwa kama kutakuwa na mgogoro katika Mahakama ya SADC. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wale walioenda ku- negotiate huu mkataba na umesainiwa tarehe 18 ya Mei, hakukuwa na watu wa Attorney General’s Office, hakukuwa na watu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali? Hakukuwa na watu wa Wizara ya Katiba na Sheria na tuna maprofesa pale! Niliposema proffesorial rubbish, this is what I meant, hawakuwepo? Hawa ambao walileta baadaye hii Sheria ya Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) hawakujua kwamba kuna mkataba umekuwa negotiated, ume… (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. TUNDU A. M. LISSU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Maneno ya Mheshimiwa Mbene wala hayahitaji heshima ya kujibiwa, naomba niendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni hivi, nimeuliza swali la msingi hapa, huu mkataba umesainiwa tarehe 18, Mei 2017. Je, Mheshimiwa Waziri wa Maji Gerson Lwenge alienda peke yake? Yeye Engineer mambo ya sheria anaweza asiyafahamu, alikuwa peke yake? Hakupata ushauri wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali? Hakupata ushauri wa Waziri wa Sheria? Wale walioleta Sheria hii ya Permanent Sovereignty over Natural Wealth hawakujua matakwa ya mkataba huu?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, matokeo yake nimezungumza na nitaendelea kuzungumza tena, matokeo yake ni aibu hizi! Mmetunga sheria miezi miwili iliyopita, leo mnaleta mkataba mnatunga sheria nyingine ya kuitengua na mtaitengua. Waheshimiwa Wabunge, nawaomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili la mgongano kati ya sheria inayosema maliasili na utajiri wa nchi yetu ushughulikiwe na Mahakama zetu uko vilevile kwenye Mkataba ambao unakuja kesho wa Bomba la Mafuta, kaangalieni. Mkataba wa Bomba la Mafuta unasema tukigombana Uganda na Tanzania kwa sababu ya bomba la mafuta mgogoro ule unaenda kuamuliwa London na hawa ambao wanajifanya ndio watetezi wa rasilimali za nchi hii, hatuoni! (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, nawaombeni, mimi nina maneno makali sana, lakini nani aniambie kama haya ambayo tumeyapitisha yako sahihi. Aniambie haya ninayoyasema ni ya uwongo, kwamba hatujaleta mkanganyiko wa kisheria hapa, kama tumeleta mkanganyiko wa kisheria tunatunga mkataba wa Kimataifa, tunapindua kile tulichokipitisha hapa kwa majidai mengi. Tunakitengua miezi miwili baadaye, sisi ni watu wa aina gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, hasa Waheshimiwa Wabunge mlio wengi, narudia tena wito wangu, haraka haraka haina baraka, maangamizi ya Taifa hili na maanguko ya Bunge hili ni hicho kinacholetwa kila leo kwa hati ya dharura. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.