Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ufafanuzi kuhusu miradi mingi ya umwagiliaji iliyoanzishwa katika Halmashauri mbalimbali hapa nchini, kwani haijakamilika na hivyo kupelekea fedha nyingi za walipa kodi kuwa zimetumika lakini hakuna matunda yaliyopatikana. Mifano ni mingi sana, lakini kwa sasa naomba kupata maelezo juu ya skimu mbili zilizopo katika Halmashauri yetu ya Lindi DC.

Mheshimiwa Naibu Spika, Skimu ya Kinyope iliyopo katika Jimbo langu ambayo ilikusudiwa kumwagilia hekari 400, lakini hadi sasa mradi unaonesha kuwa umekamilika ilhali bado, mradi ule haujatatua changamoto zilizopo pale, badala yake imeongeza maji kuwa yanamwagika hovyo katika mashamba ya wakulima, jambo ambalo linapelekea kilimo kuwa kigumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, skimu ya pili, ni ile ya Narunya iliyopo katika Kata ya Kiwalalu, Jimbo la Mtama ambapo shilingi milioni 600 zimetumika, lakini hadi leo hakuna kinachoendelea na badala yake maelezo yanayotolewa ni kwamba designer alikosea. Sasa Je, nini hatima ya mradi ule?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ni vile visima viwili ambavyo vilichimbwa Jimboni kwangu Mchinga na Wakala wa Serikali wa Uchimbaji na Visima (DDCA). Naomba tafadhali miundombinu ya visima vile vikamilishwe. Pia naomba kupatiwa visima vingine viwili katika Vijiji vya Maloo na Makumba. Vijiji hivi vina shida kubwa sana ya maji. Wananchi wa vijiji hivyo wanatembea zaidi ya kilometa tano kufuata maji. Tafadhali sana naomba Mheshimiwa Waziri anipatie maji katika vijiji hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, ni kuhusu kutotumika kwa bonde la Mto Rufiji ambalo ni very potential kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini bonde lile halitumiki kabisa. Hawa watu wa RUBADA hawafanyi juhudi yoyote kuhakikisha kuwa kilimo cha umwagiliaji kinashika kasi katika bonde la Mto Rufiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tafadhali sana, naomba Mheshimiwa Waziri achukue juhudi za makusudi kuhakikisha kuwa bonde hili linatumika ipasavyo ili tuondokane na taarifa za njaa katika Taifa ambalo lina ardhi ya kutosha na maji mengi yanayoweza kutumika katika kilimo cha umwagiliaji.