Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza jitihada ya Serikali kwa wafadhili kwa utekelezaji wa kusambaza maji mijini na sasa tuongeze nguvu katika kusambaza maji vijijini, kwani kuna wananchi kwa asilimia kubwa zaidi ya asilimia 70 wanahitaji maji, ingawa hadi sasa tumefanikiwa kwa asilimia19.8 ya fedha zote za bajeti ya maendeleo ambazo hazikidhi mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa kweli tumedhamiria kwa dhati kuwatua ndoo kichwani akinamama, Serikali isingepunguza bajeti ya maji kutoka sh.939,631,302,771/= hadi sh.648,064,207,705/=, kwa mwaka 2017/2018 bali kuongezea au tukabakia na bajeti ya 2016/2017 na kuendeleza mikakati ya kutatua upatikanaji wa fedha za kuwezesha tatizo la maji kutoweka kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Kala, Kipili, Kirando, Katete na Wampembe, Kabuve, Samazi ni maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika, lakini hawana maji safi na salama. Kata ya Muze, Mtowisa, Mfinga, Zimba, Milepa, Ilemba, Kalumbaleza maeneo ya bonde la Rukwa wakiwa na Ziwa Rukwa hawana maji safi na salama. Vile vile Kata ya Mambwe, Nkoswe, Mambwe Keunga, Ulumii, Mnokola, Mwazye, Katazi, Mkowe, Kisiimba, Mpombwe maeneo mengi haya hakuna maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bajeti ya 2017/2018, kwa mchanganuo wa fedha za maendeleo kwa Mkoa wa Rukwa wa sh.4,307,846,000/= hazitatosheleza mahitaji, kwani kutoka kwake zote ni ngumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nashauri kwa ujumla kwamba tozo ya sh.50/= ni vema ikaongezeka hadi kufikia shilingi 100/= ili makusanyo yake yaelekezwe kwenye mahitaji ya maji, kama tulivyoamua kwenye umeme na miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema tukawa pia na Wakala wa Maji Vijijini ambaye atasimamia na kufuatilia utekelezaji wa usambazaji wa maji hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa mvua, kuwepo na utaratibu wa kuvuna maji na kuandaa mabwawa ya kuhifadhia maji. Maji yanayoporomoka kutoka milimani hadi bonde la Rukwa na kuingia Ziwa Rukwa na kujaza udongo na kupunguza kina cha Ziwa hilo, ni vema utaratibu ukawepo wa kuyakinga (kuyavuna) maji hayo yakasaidia wananchi kupata maji safi na salama na pia wananchi watakuwa na kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara ya Fedha ihakikishe Wizara ya Maji na Umwagiliaji inapatiwa fedha kwa asilimia 75 kama siyo wote, kwa utekelezaji wa utatuzi wa maji kwa wananchi wetu.