Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia bajeti hii muhimu ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Magufuli na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuendelea kuchapa kazi ya kuwahudumia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa kujenga uchumi wa viwanda unaendana sambamba na kuboresha huduma za jamii ikiwemo kuhakikisha tunapata maji safi na salama kwa kila Mtanzania. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri na hizi jitihada.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji na Naibu Waziri, wanafanya kazi nzuri, ni wasikivu na kwa kweli nawapongeza kwa kuleta mpango mzuri wa bajeti kwa ajili ya mwaka 2017/2018. Niwape moyo kwa sababu katika bajeti iliyopita hata wenzetu wa Upinzani walikuwa wanasema tuwe tuna realistic budget. Sasa Wizara imeleta bajeti ambayo inatekelezeka na badala yake wenzetu wanasema kwamba iongezwe na wakati hao hao mwaka 2016 walikuwa wanasema tunaleta bajeti ambazo ziko ambitious, tuzi- reduce ziwe realistic. Sasa bajeti imekuja realistic lakini bado unaona wanapinga. Kwa hiyo, mpinzani ni mpinzani. Kwa hiyo, niwape moyo, Serikali chapeni kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naipongeze Kamati ya Maji ya Bunge kwa kuleta hoja ya kuongeza tozo kwenye Mfuko wa Maji. Nawapongeza sana kwa sababu ni muda muafaka kuleta hiyo hoja ili tuweze kuiunga mkono. Nashukuru Waheshimiwa Wabunge wengi wameunga mkono hoja, kwa sababu ukiangalia fedha kutoka kwa wahisani zinazidi kupungua, kwa hiyo, lazima kama nchi tuhakikishe tunaweka utaratibu wa kutoa huduma muhimu kama huduma ya maji kwa Watanzania kwa kutegemea fedha za ndani. Kwa hiyo, naishukuru sana Kamati ya Maji ya Bunge kwa kuleta hii hoja, naomba tuiunge mkono na naamini Serikali ni sikivu, itaichukua na kuifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hoja hii inatekelezeka kwa sababu tayari tuna uzoefu kwa upande REA. REA tulivyoitengea mfuko, unaona sasa hivi yale matumaini ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya umeme, yanatekelezeka. Kwa hiyo, tukifanya hivyo kwenye upande wa maji, naamini kabisa tutafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo sasa niende Jimboni. Naishukuru sana Serikali; namshukuru Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Serikali nzima kwa Mradi wa maji wa Rwakajunju kwa kutenga Dola milioni 30 kwa ajili ya kutekeleza mradi huu ambao tumeusubiri sana Karagwe. Naishukuru sana Serikali kwa kutenga fedha Dola milioni 30, lakini naomba sana sasa twende kwenye utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa fedha 2016/2017 fedha hii pia ilikuwa imewekwa lakini mchakato ulichukua muda. Kwa hiyo, naiomba Serikali tuweke jitihada ili wana Karagwe tuwatue akina mama ndoo vichwani na watoto wetu ili tuweze kutumia muda huu kufanya kazi za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi huu wa Rwakajunju napenda kuiomba sana Wizara izingatie vile vijiji ambavyo vinatoa haya maji vinavyopakana na Ziwa Rwakajunju. Kuna kijiji cha Kafunjo,…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.