Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia dakika hizi mbili, tatu za mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ya kwangu ni ushauri. Kwanza napenda ni-declare interest kwamba katika fani ambazo nimezisomea ni pamoja na hii fani ya uvuvi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niishauri Serikali yangu, nimshauri Mheshimiwa Rais na kwa kusema ukweli, Mheshimiwa Rais wetu nia yake ni njema sana. Nataka nimwambie kwamba kuna mapato makubwa sana kwenye uvuvi wa Bahari Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa dunia nzima inahamia kwenye jambo linaitwa blue economy. Naomba niitolee mfano Kisiwa kidogo cha Maldives ambacho kina wavuvi 8,139, sisi tuna wavuvi wadogo wadogo 203,000. Maldives ina vyombo vilivyosajiliwa vya kufanya uvuvi ambao wao wanategemea spicies moja tu ya samaki aina ya tuna, mwenzangu Mheshimiwa Ngwali ametoka kusema hapa, tena amesema kwa kufoka kwelikweli, sisi tuna vyombo vilivyosajiliwa vya maji baridi na maji chumvi zaidi ya 59,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ikiwekeza katika uvuvi, hasa huu wa Bahari Kuu ambao hatujautumia vyema mpaka hivi leo, nataka nikuhakikishie kwamba tutapata kipato kikubwa sana na inaweza ikawa ni sababu ya kuinua uchumi wetu na ajira za watu wetu kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, Mheshimiwa Rais katika mwaka mmoja huu na nusu amenunua ndege za kutosha na anaendelea kutuboreshea, tunajenga SGR, tunajenga flyovers, namwambia Mheshimiwa Dkt. Tizeba mwambie Rais wetu anunue meli ya uvuvi wa kisasa, wa kibiashara. Meli ambayo itachakata na itafanya na mambo mengine yote, utaona namna ambavyo GDP inayopatikana kutokana na uvuvi, Wabunge wote humu tutakuja kushuhudia sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni huo, najua kwa kufanya hivyo, sisi watu wa Mkuranga tutapata sasa matrekta tunayoyalilia. Maana Wilaya nzima ya Mkuranga haina trekta la Serikali hata moja, tuna matrekta 22 katika vijiji 125, yote ni ya watu na yote ni mabovu. Sasa katika uchumi wa namna hii tutapataje lakini tukienda katika blue economy, sisi tumesoma pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwalimu wangu, Mheshimiwa Dkt. Sware yule pale na wapo Walimu wangu wengine wengi kule, akina Dkt. Tamatama Rashid na wengineo, hawajatumika ipasavyo katika blue economy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena, Mheshimiwa Dkt. Tizeba na kaka yangu Mheshimiwa Olenasha, mwambieni Mheshimiwa Rais tununue meli ya uvuvi hata moja tu ya Serikali, mtaona namna ambavyo uchumi wa nchi hii utakavyopanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii niliyopata.