Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Na mimi niungane na wenzangu kusema kwamba tozo zilizofutwa kwenye kilimo, mifugo pamoja uvuvi zinawafariji wadau zaidi wa maeneo hayo hasa wananchi wetu. Nipongeze Serikali kwa hatua hiyo. Lakini nitapongeza zaidi kama tabia ya kuchelewesha pembejeo itaachwa mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamepitia vizuri kwenye vitabu na wameeleza kwamba kama kilimo ni tegemeo letu kwa nini sasa pesa zinazotengwa kwenye kilimo zinakuwa chache. Nimeangalia na nimeona kila mwaka pesa tunazotenga kwenye kilimo ni kidogo, lakini hata utoaji wa fedha zenyewe zile za kwenye bajeti zinakuwa kidogo zaidi, zile za wafadhili zinakuwa zimeongezeka yaani kama sisi wenyewe hatujaona umuhimu wa kilimo licha ya takwimu kuonyesha kwamba kilimo kinategemewa na Watanzania wengi. Kilimo ni mhimili wa uchumi wa Taifa letu na ni mhimili wa chakula katika nchi yetu kwa asilimia mia moja. Kwa hiyo, ni vitu vya kuangalia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mpango wa Uendelezaji wa Kilimo Awamu ya Pili umelenga kuongeza thamani ya chakula na tija zaidi kwa wakulima. Naishauri Serikali mpango huu uelekezwe zaidi kwenye vijiji vya uzalishaji mali kwa kuangalia miundombinu ya barabara. Kuna vijiji vyangu pale kwenye Jimbo langu, kijiji cha Milundikwa kwenda Kisula kuna barabara ya uzalishaji na si nzuri sana.

Mkiiweka kwenye mpango huu wa kuboresha maeneo ya kilimo kwa utaratibu wa kuboresha barabara zao inaweza ikatusaidia. Ipo barabara pia ya kutoka Katani kwenda Myula, barabara ya kutoka Kasu kwenda Malongwe ni maeneo ambayo yanatusaidia sana katika suala zima la uzalishaji katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nizungumzie pia juu ya Ranchi za Taifa. Kupitia kitabu cha Mheshimiwa Waziri nimeona ni kama Ranchi ya Taifa (NARCO) ni kama haina mtaji wa kutosha kuwezesha kusaidia Ranchi zetu za Taifa. Nikitolea mfano juu ya Ranchi yetu ya Kalambo ambayo ina ukubwa wa hekta za eneo 23,000 yenye uwezo wa kuwa na ng’ombe zaidi ya 7,000; lakini leo hii Kalambo ina ng’ombe 700, sasa utaona kama ipo under utilized.

Kwa hiyo, ni vizuri Serikali itusaidie kuimarisha ranchi zetu hizi ili iwe ni mfano wa kuigwa kwa wafugaji wanaozizunguka. Kwa sasa mchango huo huuoni kwa wananchi wanaozunguka ranchi hizo, nadhani ndiyo ilikuwa maana kubwa ya Serikali ya kuweka ranchi hizi katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaohudumiwa na Kalambo hasa katika blocks zile zilizobinafsishwa sasa hivi wana mgogoro pia wa mpaka kati ya Rwamfi Game Reserve na Kalambo yenyewe. Wanapoendeleza shughuli zao na huku wanalipa kodi ya Serikali lakini Serikali bado inawafanyia fujo kwenye mipaka ile ya Rwamfi Game Reserve. Kwa hiyo, kuna sababu ya kupitia mipaka upya ili kutowasumbua wananchi hawa ambao wanalipa kodi. (Makofi)

Vilevile kwenye uzalishaji wa mifugo (ng’ombe), kuna shida ya kupata madume, madume ni machache. Tungetegemea madume yazalishwe kwa wingi ili wananchi walio katika block hizi waweze kunufaika na breed hizi mpya za kisasa zenye kuleta tija za ufugaji. Hii ingeweza kutusaidia kuliko ilivyo sasa hivi madume tunategemea uhaimilishaji ambao wananchi hawajauzoea na wakati mwingine wanaona kama ni gharama kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuongelea chanjo na dawa za mifugo. Katika Mkoa wa Rukwa imetajwa Wilaya ya Nkasi hapa kwamba ni eneo ambalo mnataka mliendeleze liwe free kwa magonjwa lakini dawa tunapata kutoka Arusha, ni mbali. Hakuna center ya karibu ya kupata dawa na chanjo ili wakulima na wafugaji waweze kupata dawa katika maeneo ya karibu. Hii ingeweza kutusaidia kuboresha eneo la ufugaji kwa maeneo ya Mkoa wa Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuhusu soko, wafugaji wanafuga lakini hakuna soko la karibu la kuuza nyama kwa bei nzuri. Tuna kiwanda pale cha Mheshimiwa Mzindakaya, tungeweza kuona Serikali kama kuna changamoto yoyote kiweze kuboreshwa ili kiweze kuhudumia center ya eneo letu katika suala zima la mifugo yetu ambayo tunaizalisha pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu suala zima la uvuvi. Katika eneo la uvuvi hatujafanya vizuri. Wakati tunaongeza uchangiaji wa ruzuku kwenye kilimo lakini wavuvi kidogo tumewaacha nyuma. Naomba Serikali tuongeze zaidi kuwachangia wavuvi katika vifaa ambavyo vinaasaidia na mikopo ambayo inaweza ikawasaidia. Hivi karibuni mlitueleza hapa kwamba wavuvi wangeweza kuweka utaratibu wa mfuko wao wa kuwakopesha lakini huo mfuko sijauona kama umetusaidia kwa kiwango chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa Tanganyika lile lina mwambao mkubwa sana na wavuvi wengi wanaokaa kule ni maskini lakini hatujasaidiwa vya kutosha na pesa yoyote iliyotoka Serikalini kwa ajili ya kusaidia vikundi vya wavuvi ili waweze kuboresha maisha yao. Wamezungukwa na rasilimali ambazo ni tajiri sana, lakini bado naona kama ni maskini. Naiomba Serikali ione uwezekano wa kutoa pesa za kutosha kusaidia wavuvi kama vile tunavyosaidia wakulima na wafugaji wakati mwingine wanasaidiwa kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja.