Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Mary Deo Muro

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haki yangu dakika kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nina machache ya kuchangia hoja iliyoko mezani. Kwanza ningependa kuungana na wengine wote waliosema Serikali iimarishe utafiti kwa sababu utafiti ndiyo utafanya zile tafiti zifike kwa wananchi waweze kulima kilimo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongolea kuhusu ushirika. Tunafahamu kabisa ushirika ulikuwa ndiyo Sera ya Mwalimu Nyerere ambayo iliwaunganisha wananchi kufikia malengo kwa pamoja. Ushirika huu kwa sasa hivi umeyumba baada ya wafanyakazi wengi kupunguzwa na ukaguzi wa Vyama vya Ushirika kuwa mgumu. Kwa hiyo, ningeishauri Serikali iangalie kwa upya kuongeza wafanyakazi watakaokagua Vyama vya Ushirika kuanzia kwenye Vyama vya Msingi mpaka Vyama Vikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea kuhusu mifugo. Wananchi wa Pwani wanaomba Waziri anapo-wind up awaeleze shamba letu la majani la Vikuge linayumba, lina shida, hakuna majani. Wananchi walikuwa wamezoea kununua majani kwa ajili ya mifugo, ile zero grazing lakini shamba la Vikuge halina majani, ukifika pale limeota miti, Waziri aeleze kuna nini hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia wananchi wa Pwani wanauliza, je, Bonde la Rufiji kilimo kile kimeishia wapi na ile RUBADA imeishia wapi. Waziri tunaomba atueleze ili waweze kujua kwamba labda ipo siku watafikia yale malengo yaliyokuwa yametarajiwa na waanzilishi ya RUBADA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchangia kwenye eneo la uvuvi. Kwenye uvuvi kuna matatizo ya nyavu na makokoro kama wanavyoita wavuvi. Hata hivyo, mara nyingi unakuta kwamba wananchi wanachomewa nyavu zao shida unaambiwa kwamba kwa sababu wanavua samaki wadogo lakini sijaona mkakakati wa makusudi wa kuzuia watengenezaji wa nyavu au waingizaji wanyavu bali wanawachomea wale ambao wananunua.

Mimi napenda Serikali iweke mkakati wa kuhakikisha kwamba nyavu ambazo hazihitajiki haziingii hapa nchini kwa sababu sio kosa la mvuvi. Mnamuonea mvuvi ambaye anakwenda dukani ananunua zile nyavu kwa sababu yeye siyo muagizaji. Serikali inatakiwa iangalie suala hilo kwamba mvuvi apate haki yake, amenunua zile nyavu kwa sababu ziliingizwa na kuna watu ambao wapo kwa ajili kufanya kazi ya kuhakikisha kwamba nyavu hizo haziingii hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia kuhusu kilimo na niungane na wale wote waliosema kwamba Wagani wamekosa vitendea kazi. Ni kweli kabisa tusitarajie kwamba Mgani huyu yuko ofisini anatakiwa kuwafikia wananchi, aende kwa mshahara wake huo mdogo, hana posho wala kitu chochote akafanye kazi arudi na watoto wake wale nini? Hebu Serikali iangalie hapo kwamba tukitaka Mgani aweze kufanya kazi yake ni lazima tumjali kama tunavyojali wafanyakazi wengine. Hata sisi wenyewe leo hapa tungekuwa hakupati posho leo hakuna mtu angekuwepo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuzungumzia kuhusu mgogoro wa wakulima na wafugaji. Mgogoro huu ni wa siku nyingi na kila siku maelezo na majibu ni yale yale. Hivi kwa nini tusifanye research ili kujua ardhi ya Tanzania ni kiasi gani na matumizi ya ardhi ya hiyo ni yapi, tukayapanga kwa vipaumbele ili tujue kwamba mfugaji atakuwa na eneo lake la kufuga na mkulima atakuwa na eneo lake la kulima ili tusilete migongano. Nashauri Wizara mbili hizi zikae zikatathimini, ardhi ipi itumike kwa ajili ya ufugaji, kilimo na reserve kwa ajili ya wanyamapori. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mifugo hiyo hiyo na napenda kuzungumzia kuhusu walaji wa nyama itokanayo na mifugo. Watanzania wengi au wenzetu anaokuja kutoka nchi za nje wanaogopa kula nyama ya Tanzania kwa sababu moja tu. Sababu ni kwamba nyama ya Tanzania ni hatari kwa sababu machinjio ni mabovu na machafu, hakuna machinjio ya kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali iliangalie hili kwamba kama tunaamua kuwalisha Watanzania nyama basi tuangalie hao ng’ombe wananchinjiwa wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefika hapa Dodoma nimekuta kuna machinjio ya kisasa lakini kule kwangu nakotoka Kibaha, Pwani yote ile haina machinjio ya kisasa. Wizara hakikisheni kwamba mnaboresha machinjio ili wananchi Watanzania wasije wakapata maafa kwa kula nyama chafu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo pia napenda kuzungunzia suala la uingizaji wa mazao ya mifugo kutoka nchi jirani. Ni kweli kabisa tuna nia ya dhati na mimi ni mfugaji vilevile, lakini kuna kitu ambacho wafugaji wa Tanzania wanapata shida ni pale ambapo unakuta tunashindana na Kenya au na Uganda kuingiza mazao ya mifugo au mazao ya kilimo bila Serikali kujali angalau wafugaji au wakulima wa ndani. Naishauri Serikali iangalie kwa sababu wananchi wanakuwa wame-invest fedha nyingi kwenye kilimo au kwenye mifugo, mtu anafuga kuku anaenda sokoni anakosa pa kuuza mayai kwa sababu mayai ya Kenya yamejaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo tumeona sehemu nyingi sana wananchi wanalima kwa kujitegemea. Wanajitegemea kwa sababu yeye ndiyo atatafuta mbegu na kila kitu, lakini Serikali inataka kupanga bei au inamzuia kwamba asiuze mazao yake au auze kwa wakati fulani. Tunatakiwa tufahamu kwamba kama unamwambia mwananchi asiuze mazao yake na ana watoto wanatakiwa kwenda shule na anatakiwa kwenda kwenye matibabu bila kuuza mazao yake atategemea nini na yeye anategemea mazao yake ndio ATM yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali itoe elimu kwamba mkulima atalima lakini auze kwa namna moja, mbili tatu lakini isizuie kabisa kwamba wakulima hakuna kusafirisha kwenda kuuza wapi kwa sababu sometimes anakwenda labda kuuza Uganda kwa sababu anajua kabisa Uganda kuna bei nzuri. Kama Serikali inanunua kwa bei ndogo, kwa nini asiuze sehemu nyingine ili aweze kurudisha gharama zake alizotumia wakati wa kilimo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia kuhusu maghala na ununuzi wa Serikali wa mazao ya wakulima. Mazao mengi yanabaki bila kununuliwa na Serikali inanunua mazao machache, kwa mfano tuchukulie mikoa ambayo ni big five unakuta mara nyingi wana mazao mengi kuliko uwezo wa Serikali wa kununua. Kwa nini Serikali isiongeze uwezo wa kununua mazao ili wananchi wasiweze kupoteza mazao yao kwa sababu unakuta hakuna maghala ya kuhifadhia na hakuna ununuzi, watu wameweka mazao yao nje yananyeshewa na mvua, nguvu za wananchi zinapotea bure. Naishauri Serikali iliangalie hilo na ilitendee kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani.