Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia katika hii Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba aliyetangulia amesema hatupaswi kupongeza, lakini wanasema usiposhukuru kwa kidogo, hata kwa kikubwa hutashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ambayo imefanywa na Wizara hasa ya kuondoa hizo tozo ambazo ndizo kero kubwa kwa wananchi wetu, ni kazi nzuri ambayo inahitaji kupongezwa. Vilevile naendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa taarifa nzuri. Taarifa nzuri kwa maana gani? Wizara imeendelea kuzungumza aidha madhaifu au mafanikio, yote wameendelea kuyaweka bayana. Hii siyo kwa sababu nyingine; wamefanya hivyo ili waweze kupata ushauri. Mheshimiwa Waziri, nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, ninachohitaji tu kusema, mfano ukisoma kwenye ukurasa wetu wa nne unasema, kilimo kinachangia asilimia 65 ya ajira; lakini ameendelea kusema, kwenye upande wa chakula kilimo kinachangia asilimia 100 na kwenye pato la Taifa kinachangia asilimia 29. Hii ameisema kwa sababu ya kuonesha hali halisi na umuhimu wa kilimo. Tunapokuja kwenye ukweli ni kwamba kwa kweli Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni Wizara ambayo haikupewa fedha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kupitia kwenye hiki kitabu, ukiangalia pale page number 27 na 28, kwenye miradi ya maendeleo ya mwaka 2016/2017, zile fedha za maendeleo zilizokuwa zimetengwa, shilingi bilioni 800, zilizotolewa ni 4% peke yake, kwa maana ya shilingi milioni
280. Fedha za wafadhili ndiyo zimetoka kidogo kama shilingi milioni 900 ambayo ni asilimia 12. Kwa hiyo, hii tu inaonesha kwamba ni kweli tuna changamoto kubwa kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia, leo sisi hasa watu wa Kanda ya Ziwa tunalia sana tatizo la kilimo kwa maana hatuna chakula. Siyo kwamba ni wavivu lakini ni kwamba tunalima, tukishalima kwa sababu ya kukosa maji, kile chakula kinakufa. Bahati nzuri ndugu yangu Mheshimiwa Tizeba, ukipita tu pale Magu utawaona wako pale vijana wa Kisukuma wanahangaika na vi-pump vya maji, tena vile vya petrol, vi-pump vidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe kinachopaswa kufanyika pale ni kwamba, ukiangalia kwenye mabonde kama haya tuliyonayo mengi, ni kwa nini basi tusianzishe zile irrigation scheme tena kwa utaratibu rahisi tu, tunatangaza tender kama tunavyotangaza tender za barabara? Nani anataka hizi hapa ekari 3,000 aje afanye irrigation! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namna ya kuwalipa, ule mpunga wenyewe kama ni mpunga ambao ukiangalia mchele una soko kubwa Kenya, Uganda, Rwanda na tuna soko kubwa la ndani. Kwa hiyo, ni kwamba wale wakulima wenyewe wataweza kulipa zile gharama za kuendesha shamba lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya maeneo tuliyonayo yako mengi. Nilidhani tu kwamba kupitia ile Benki ya Kilimo ni vizuri basi tukaweka mkakati mahsusi kwa ajili ya kilimo cha irrigation na hii itatupunguzia adha ya chakula; hii ambayo kila leo tunaipigia Serikali kelele kusema Serikali ilete chakula. Tunaamini kwamba Serikali kwa majukumu iliyonayo na kwa shughuli ilizonazo, fedha za kuweza kutuletea chakula hazipo. Kwa hiyo, nilidhani kama Mheshimiwa Waziri atauchukua huo ushauri, atakuwa ametusaidia katika upande huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nizungumze kidogo kuhusu uvuvi. Sisi pale kwetu Musoma Mjini tunavyo viwanda visivyopungua vitano vya samaki. Kwa taarifa yako na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri anafahamu, vile viwanda vyote vimekufa. Vile viwanda vimekufa siyo kwa sababu nyingine, ni kwa sababu ya uvuvi haramu, wale samaki wameisha, vile viwanda kwa Musoma Mjini vilikuwa vinachangia uchumi kwa kiasi kikubwa sana, lakini siyo Musoma tu, hata Mwanza vile viwanda vya samaki vimekufa, hata kule Bukoba vile viwanda vya samaki vimekufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi nini kifanyike? Njia pekee ni kwamba lazima uvuvi haramu uendelee kupigwa vita. Mheshimiwa Waziri yeye anao ushahidi, pale kwetu Musoma Mjini bahati nzuri tunaye DC mmoja anaitwa Anney Vincent. Ni DC ambaye hata Mheshimiwa Waziri anajua amefanya kazi nzuri sana. Kwa Musoma Mjini, uvuvi haramu haupo; lakini sasa cha ajabu ni kwamba ukiondoka tu pale Mjini, ukianzia Bunda na kuelekea kwenye maeneo mengine, ule uvuvi haramu unaendelea kama kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama ndio hivyo, maana yake ni kwamba hata ile juhudi anayoifanya ya kuhakikisha kwamba huu uvuvi haramu unaisha, maadamu anafanya katika eneo moja, tafsiri yake ni kwamba hao samaki watakuwa wanaenda maeneo mengine na wataendelea kwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwa kazi ile iliyofanyika, mpaka hivi sasa, angalau kwa pale mjini samaki tunaokula ni wale wazuri. Sasa kinachotakiwa kufanyika ni kumwangalia mtu kama huyu tukampa overall ya Ziwa Victoria akahakikisha kwamba anapata resources. Naamini wale wenye viwanda watachangia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanazuia uvuvi haramu. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo, tunadhani kwamba itatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine dogo, hebu tuanzishe vile vikundi vinavyofuga samaki kwa njia ya caging ambapo wakifuga vile wale wenyewe watakuwa walinzi wakubwa wa wale wanaovua uvuvi haramu. Kwa kufanya hivyo, itatusaidia sana kuhakikisha kwamba hilo tatizo la uvuvi haramu linaisha, viwanda vyetu vinafufuka na uchumi wetu unakua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niguse kwenye upande wa ufugaji. Kwa kweli kwenye ufugaji bado hatujafanya kitu. Hatujafanya kitu kwa sababu gani? Tunazo ranch nyingi, nimeangalia hapa kwa haraka haraka, tuna Sao Hill, Mabuki, Kitulo mpaka ranch yetu ya NARCO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukisoma kwenye ukurasa wa 110 pale, Mheshimiwa Waziri mwenyewe anasema kwamba kwa mwaka 2016 tumeweza kuzalisha mitamba 634. Sasa hizi ranch zote zina uwezo wa kuzalisha mitamba 634 peke yake? Tafsiri yake ni kwamba zile ranch tumewapa watu wachache wafaidike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenyewe bahati nzuri ni mfugaji, unapozungumza mitamba 634 hiyo, ukienda kwenye zizi langu pale kwenye wale ng’ombe nilionao, unawapata hao mitamba 634, tena mitamba wazuri na wa kisasa. Hata siku moja niliweza kuleta ng’ombe wangu hapa Dodoma machinjioni, bahati nzuri nikamwalika Mheshimiwa Naibu Waziri, alifika akawaona. Ng’ombe mmoja nilikuwa nauza siyo chini ya shilingi 1,200,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kumbe tunachohitaji kufanya katika kusaidia mifugo, ushauri wangu ni kwamba hizi ranch nyingi tulizonazo, hebu tuwachukue wale wafugaji wanaofanya kazi ya kunenepesha. Hata ukipita pale Mwanza baada ya Coca Cola hapo njiani utakuta Wasukuma wapo pale wanahangaika, wanalisha mashudu, hakuna eneo la malisho. Ukiangalia hizi ranch nyingi tulizonazo hizi, zimekaa tu. Hivi kwa nini tusiwapangishe waka-lease, halafu wakaweza kufuga mifugo ya kutosha, mingi tukaweza kuendelea?

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Ahsante sana. Naunga mkono hoja.