Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuipa nafasi ya kuweza kuchangia hoja hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni uti wa mgongo, bila kilimo hatuwezi kufikia lengo letu la Tanzania ya Viwanda. Ukiangalia bajeti ya kilimo kama kweli kilimo ni uti wa mgongo bajeti ni ndogo sana, asilimia 4.9 ambayo inakwenda kuwasaidia Watanzania ambao ndiyo asimilia kubwa ya wakulima, asilimia 70. Bajeti hii ni ndogo naiomba Serikali iongeze bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushindani wa soko usio wa haki. Kuna ushindani wa soko usio wa haki. Kwa mfano, Mkoa wa Njombe wanazalisha viazi kwa wingi, viazi hivi hawaruhusiwi kuweka zaidi ya kilo mia moja wakati Wakenya wanaweka zaidi ya kilo mia moja na wanauza soko moja. Naiomba Serikali iliangalie suala hili kwa sababu Watanzania wanapata hasara, viazi vyao havitoki, Wakenya wanaweka vingi na viazi vyao vinatoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu gharama za upimaji wa udongo. Katika Mkoa wa Njombe wakulima wanachukua udongo ule kupeleka Mbeya kwa ajili ya kupima na udongo huu unapimwa kwa unit moja kwa Sh.75,000/=, kila shamba linatakiwa liwe na unit nane, kwa hivyo shamba moja linagharimiwa kwa shilingi laki sita na elfu saba. Kwa kweli wakulima hawataweza kuendelea na suala hili la upimaji wa udongo kwa sababu ya gharama hizo. Naiomba Serikali iwapunguzie au iwasaidie wakulima wa Njombe udongo huu upimwe kule kule Njombe badala ya kusafirishwa kwenda Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tozo. Ninaishukuru Serikali kwamba katika hotuba ya Waziri umeeleza kuondoa tozo mbalimbali, ninashauri kwamba tozo hizi zingeorodheshwa zote, halafu tuone ni tozo zipi zinatoka na tozo zipi zinabaki. Kwa sababu ukiangalia kwa mfano, wakulima ambao wana vyama vyao vya ushirika wametolewa ile tozo ya Sh.500/= isiwepo, nafikiri ni vema kuondoa zile tozo kubwa zinazotozwa na Serikali kuliko kuziondoa zile tozo ambazo ni za wakulima wadogowadogo, kwa sababu zile zitawasaidia kwenye vyama vyao vya ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninaiomba Serikali iliangalie suala hilo tena kwa sababu ni kweli tozo hii imetolewa kulingana na hotuba yako lakini bado wakulima wadogo ambao wana vyama vyao vya ushirika watapata hasara, kwa sababu hawatapata kitu chochote cha kuendeshea vyama vyao vya ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mbegu za viazi. Mwaka jana kulikuwa na tatizo katika Mkoa wa Njombe wa kuunguliwa viazi kutokana na hali ya hewa, hawakupata kabisa viazi na Serikali iliahidi kuwasaidia na wakawa wamesaidiwa kiasi fulani cha mbegu. Zile mbegu walizosaidiwa kwa kweli hazifai na siyo nzuri, hivyo wakulima hao wamepata hasara vile viazi haviuziki kwa sababu zile mbegu siyo kama mbegu ambazo walizoea kuzitumia miaka yote. Naiomba Serikali iwasaidie wakulima hawa kama inawezekana kufika Njombe na kuona ni namna gani wanaweza kuwasaidia wapate mbegu ambazo ni nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Benki ya Kilimo mpaka sasa hivi siielewi ni namna gani inawaisaidia wakulima. Mwaka jana tulipata maelezo mazuri tene ilikuwa semina nzuri sana ya Wabunge wote tulielekezwa kwamba benki hii itakwenda katika mikoa mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa hivi katika Mkoa wangu wa Njombe wakulima wanalalamika na wanahangaika sana kwa sababu benki hiyo ingeweza kuwasaidia sana wakulima kupata mikopo na kuweza kuboresha kilimo chao ili waweze kupata maao kwa wingi na iwasaidie angalau kupanda kwa uchumi wao na Mkoa wa Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Njombe ni kati ya Mikoa ambayo inazalisha chakula kwa wingi, tatizo kubwa ninaloliona ni kwamba hawana maghala ya kutosha. Kuna ghala moja Makambako. Naishauri Serikali kuhakikisha maeneo kama haya na hasa Nyanda za Juu Kusini na kila Mkoa unakuwa na ghala za kutosha kwa sababu vyakula wanavyozalisha vinaishia kuoza au kutawanya ovyo kwa sababu hawana ghala. Ghala zingesaidia sana angalau kuhifadhi chakula na kusaidia nchi nzima

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pembejeo; nashukuru kwamba Serikali imetamka sasa pembejeo na hasa mbolea zitawekwa madukani, ninachoomba na kusisitiza ni utekelezaji. Mbolea iwekwe madukani pamoja na pembejeo zingine ziwekwe madukani ili kusudi wananchi hawa waweze kununua kwa urahisi na kwa wakati wowote hasa kwa Mkoa wa Njombe karibu mwaka mzima wanalima. Kwa hivyo, kama watakuwa na mbolea hizi madukani maana yake watazalisha kwa wingi na muda wote hawatakuwa na shida na bei za pembejeo hizi zitakuwa zimeshuka kwa sababu zitakuwa madukani. Kwa hivyo, niiombe sana Serikali na nisisitize utekelezaji wa suala hili ambalo Serikali yenyewe imeahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la mifugo, wafugaji na wakulima. Kuna maeneo yanayopakana na Mbeya ambalo ni eneo la Wilaya ya Makete, kuna tatizo la wakulima na wafugaji, wakulima wanalima vyakula vyao lakini wafugaji wanapeleka mifugo yao wanalisha mashambani. Naiomba Serikali kwa sababu nafikiri ni maeneo mengi ambapo tatizo hili lipo, suala hili lishughulikiwe kwa sababu linawakatisha tamaa sana hasa wakulima, kwa kuwa wanalima kwa bidii halafu ng’ombe wanakuja wanakula, kwa hivyo tunawakatisha tamaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, naiomba Serikali isaidie kutatua mgogoro huu wa wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.