Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza nasikitika kwamba nitachangia huu mchango wakati Waziri wa Fedha hayupo na hata Naibu wake hayupo, kwa hiyo, mambo mengi ambayo nitayasema hapa wao hawatayasikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba awafikishie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Kilimo. Kiukweli kabisa naunga mkono hotuba yetu ya Kamati yetu ya Kilimo. Waheshimiwa Wabunge mtakuwa mashahidi, hii Kamati katika Bunge hili la bajeti tumekuja na hotuba ambazo ni very constructive. Tumefanya hivyo kwenye Wizara ya Maji na leo tumerudia tena. Nampongeza zana Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Mary Nagu kwa kazi nzuri aliyoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri, hebu ajaribu kuchukua ile hotuba ile ya Kamati yetu tunafanya kazi pamoja, aiangalie. Tumeshauri vitu vya msingi sana kwa maslahi ya Taifa. Shida ninayoiona ambayo siku zote tunaeleza kwenye Kamati, Mheshimiwa Waziri hauna fedha. Hapewi pesa! Watu wanasema zaidi ya 75% ya Watanzania ni wakulima. Haifanani na fedha ambayo anaipata na ndiyo maana nikasema Waziri wa Fedha labda angekuwepo angetusikiliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wengi wanalalamika humu ndani, kwa nini hii Wizara haipewi fedha inazotengewa? Kwa nini Wizara ya kilimo ambayo ndiyo tunasema uti wa mgongo wa Taifa letu, fedha zinazotengewa tunapata pungufu? Mheshimiwa Waziri, sijui kama kuna Wizara ambayo imepata fedha chache kuliko hii!

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunavyochangia hapa tujue kwamba tunachangia kwa hotuba nzuri ya Waziri na kwa maneno mazuri aliyotuambia, lakini in reality hii Wizara haijapata fedha. Mwenyekiti wetu amesema hapa, fedha ya development ni asilimia 3.8; ni jambo la aibu sana! Sasa kama tunapata fedha ndogo kiasi hicho, tunadhani haya mambo tuliyoyazungumza yatafanikiwaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Jenista amfikishie Mheshimiwa Waziri wa Fedha; tumemkosea nini Watanzania; ambapo 75% ya Watanzania ni wakulima? Kwa nini hapeleki fedha kwenye Wizara ya Kilimo? Hilo ndio jambo langu la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, katika hotuba yetu ya Kamati tumezungumzia suala la bulk procurement ya mbolea. Kama kuna mtu yeyote aliyejiandaa kupinga huu mfumo, sisi kama Wajumbe wa Kamati, nami nasema huyo mtu kwa kweli labda ana maslahi yake mengine lakini siyo maslahi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mbolea linajulikana namna lilivyokuwa na utata, lakini jambo hili sisi pale Kilwa kunajengwa Kiwanda cha Mbolea. Kwa hiyo, tunahitaji na hawa ambao leo wanapinga, ndio hao hao wanafanya mipango ya kuhujumu kile Kiwanda cha Mbolea. Kwa hiyo, jambo hili linabeba maslahi ya Taifa, linabea maslahi mapana kabisa ya nchi yetu. Naomba jambo hili lianze haraka, mbolea ianze kuagizwa kwa mfumo huo; litakuja kutusaidia kama Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposimama kwenye maslahi ya Taifa, haya mambo ya itikadi zetu na mambo mengine tunaweka pembeni kwa sababu tunajenga nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumze pale alipoishia jirani yangu ndugu yangu Mheshimiwa Dau; amelalamika sana kuhusu masuala ya uvuvi. Kwenye fikra yangu nafikiri hii Wizara kubwa kwa sababu hata kwenye matamshi yake inaitwa Wizara ya Kilimo, Mifugo, yaani huo uvuvi wenyewe ndiyo umetamkwa mwishoni kabisa “na Uvuvi;” yaani as if ni supplementary, yaani uvuvi ni kama additional. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoamini ni kwamba kuna nchi kadhaa duniani zimepiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kutegemea uvuvi na tunayo mifano mingi katika hili. Sasa Mheshimiwa Waziri hebu angalia namna gani unatoa kipaumbele kwenye sekta ya uvuvi, leo tuna uvuvi wa bahari kuu, kuna nchi zinaendesha nchi zao kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu tu. Wapo wazungumzaji wamesema hapa kwamba lipo eneo kama Lindi na Mtwara ni kama ni virgin sea, bahari ambayo haijatumika kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mifano mingine, kulikuwa na samaki walikamatwa hapa, walikuwa wanaitwa samaki wa Magufuli, wakati ule Mheshimiwa Rais alikuwa Waziri wa Uvuvi. Wale samaki walikamatwa walivuliwa siku tatu tu walipokwenda kuuzwa thamani yake ilikuwa zaidi ya bilioni tatu, kwa mtu ambaye tulimpa leseni ya shilingi milioni 800 kwa mwaka kuvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili liangaliwe. Tukitegemea kupata mapato ya uvuvi wa bahari kuu kwa kutegemea leseni, we are very wrong na hatutaendelea. Tuwekeze sisi wenyewe, tuwawezeshe wavuvi wetu wa ndani waweze kuwa na uwezo wa kuvua bahari kuu. Tuna samaki wengi kule. Vile vile jambo hili liende sambamba na ujenzi wa bandari ya uvuvi, ili hata hawa wavuvi ambao leo tunawapa leseni, wakishavua waweze kushushia mzigo wao hapa Tanzania tuweze kukusanya kodi. Jambo hili kila siku tunalisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bahari kuna lasilimali nyingi. Leo ukitoka Tanga mpaka Mtwara watu walio karibu na bahari kwa bahati mbaya ndio maskini, yaani nchi hii ukikaa karibu na bahari wewe ndio kama umepigwa laana; wewe ndio maskini; wakati bahari ni utajiri. Leo
tunajua kuna mikoa mingi nchi hii wanategemea uvuvi, ukiwemo na Mkoa anaotoka Mheshimiwa Waziri; hawa wavuvi tunawasaidiaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo uvuvi tumeuweka ni kama additional, kama supplementary. Naomba sana, Katibu Mkuu wa Wizara namfahamu, ni mtu mzuri, ni mchapakazi, wamwezeshe, wampe pesa! Hawezi kufanya kazi! Hili nalalamika tena kwa Waziri wa Fedha, leo Sekta ya Uvuvi imeachwa kabisa. Ukiangalia mafungu, fedha walizozipata ni as if sisi nchi hii hatuna wavuvi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba sana suala hili tulizingatie kwa umakini mkubwa sana, litatusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais aliyepita alianzisha harakati za ujenzi wa bandari ya uvuvi, nataka kujua wameishia wapi? Tunataka tupate majibu ya kutosha kwamba ile bandari ya uvuvi iliyokuwa inataka kujengwa, mpaka leo imefikia wapi? Naamini kuna hatua kadhaa zilishachukuliwa, sasa je, wao ndio wameacha kabisa au wanaendelea? Mheshimiwa Waziri, naomba atakapokuja aje kunijibu hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la NFRA. Suala la chakula ni jambo muhimu sana. Hatuwezi kuwa na nchi ambayo haina chakula na hatuwezi kuwa na watu ambao watakuwa wanafanya kazi vizuri kama chakula hakuna. Mwaka huu tumeingia kwenye matatizo makubwa, wengine wanasema kuna njaa, wengine hakuna njaa, wengine kumekuwa na shida. Pia, hebu tujipime kama nchi; hifadhi yetu ya chakula ina kiasi gani cha chakula cha kuweza kutulisha? Kumekuwa na majanga mengi sasa hivi yanatokea kama ukame. Unaona Mkoa wa Dodoma uko na ukame mwaka huu na mikoa mingine. Uzalishaji wetu wa chakula umekuwa mdogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, NFRA hawaipi kabisa kipaumbele. Nawaambia, ukitokea mwaka mmoja hapa kama Wabunge wangekuwa wanajua kwamba ingetokea Mwenyezi Mungu akatupiga gharika hapa miezi mitatu; siyo jambo la kuombea na siombei na leo siku ya Ijumaa, Mwenyezi Mungu hili jambo atuepushie.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikitokea miezi mitatu tu nchi hii ikaingia njaa, nchi hii tunaparaganyika kabisa, kwa sababu hifadhi yetu ya chakula haiwezi kukidhi haja hata ya miezi miwili kulisha nchi hii. Leo mwaka 2017/2018 bajeti iliyopita NFRA ilitengewa shilingi bilioni 18 iweze kununua mahindi na nafaka. Mpaka hivi sasa tunapozungumza, mmeipa shilingi bilioni tisa tu. Yaani ni nusu ya fedha ambayo tumeitengea. Hata hii tulilalamikia kwamba ilikuwa ni fedha ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakupa mfano, mwaka 2014/2015, wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, Serikali ilitenga shilingi bilioni 109,656 kwa ajili ya NFRA, lakini ilitoa zaidi ya asilimia 110; Serikali ilitoa shilingi bilioni 111. 9. Leo mwaka 2016/2017 tunatoa bilioni tisa, are we serious? Hatuoni kwamba kuna mabadiliko ya tabianchi? Hatuoni kwamba hali ya uzalishaji wa chakula inapungua? Kwamba tumeifanyaje hiyo NFRA? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, suala la chakula; chakula ni siasa, food is politics, food is life; chakula ni maisha pia. Kwa hiyo, tusicheze na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie jambo la mwisho, naona muda unakwenda. Mheshimiwa Esther, naomba kidogo Mheshimiwa Waziri wa Maliasili anisikilize na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana nilisema pale Wizarani kwamba sisi tunafanya kazi kubwa kuwahimiza wakulima waweze kulima ili baadaye wajinasue na matatizo yao ikiwepo kuondoa njaa. Leo ndovu (maana nikisema tembo kuna watu wengine nawakwaza) mpaka hivi sasa ninavyokwambia, tangu juzi nimeomba Mwongozo hapa, mpaka hivi sasa wameshakula zaidi ya ekari 45 za wakulima. Mwaka 2016 zililiwa ekari 183, hakuna hatua iliyochukuliwa.

Hivi sasa ninapowaambia, hao ndovu wako Mchinga wanatembea tu kama mbuzi. Kwa hiyo, nasema na mwaka 2016 nilisema hapa, msituone wapole, nasi tunawaachia kwa sababu sisi tunajua kwamba ndovu ni rasilimali ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkulima ni mtu mnyonge. Ikifika siku akachoka, akaamua kufanya hicho anachokiweza, tusije tukalaumiana. Lazima tuliseme hilo! Haiwezekani mtu ambaye mwaka 2016 ameliwa ekari 183 hakuna hatua iliyochukuliwa. Naibu Waziri wa Maliasili amekwenda anasema kwamba tutawaletea hiyo laki moja kwa kila ekari, tangu mwaka 2016 amekwenda, mpaka leo hakuna hatua iliyochukuliwa. Leo hao hao ndovu wanakula tena!

Mheshimiwa Naibu Spika, ndovu wanatoka mbali sana, sisi hatujapakana na hifadhi, wamekuja kwa sababu ya mazingira mazuri tuliyonayo kwamba tuna misitu ya asili, tuna maeneo yana maji na bahari. Wakifika wanakaa msituni, usiku wanakwenda kula kwenye mashamba ya watu, mchana wanakwenda kupata upepo wa bahari, ndiyo mazingira yaliyowavutia! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema very serious, juzi nimeomba Mwongozo hapa lakini mpaka sasa hakuna hatua iliyochukuliwa Mheshimiwa Waziri. Nazungumza kwenye Wizara hii kwa sababu wale watu watakapoishiwa chakula, watapeleka tena. Juzi walipeleka tani 500 kwa sababu chakula kimekwisha. Nikienda tena kuwaomba tani 1,000 wasininyime kwa sababu ndovu ambaye anawatunza Mheshimiwa Waziri wa Maliasili wanakula vyakula vya wakulima wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.