Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuweza kuchangia bajeti ya Wizara hii. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja hatua ya Kambi Rasmi ya Upinzani. Tanga ulikuwa ni mji wa viwanda na biashara pamoja na kilimo cha zao la mkonge (palikuwepo mashamba 72).

Mheshimiwa Naibu Spika, Viwanda vya Zamani. Tanga ina bandari na reli ambavyo viliweza kusafirisha bidhaa zinazozalishwa viwandani, wakati ule katika miaka ya 1970 -1990 ambapo pia ajira zilipatikana kwa wingi. Viwanda vingi vimelenga kwa ama kubinafsishwa na kupewa (kuuziwa) watu wasio na uwezo wa kuendesha aina za viwanda hivyo. Mfano Tanga, Steel Rolling Mill (chuma) kimekufa, hali ya kuwa chuma bado kinahitajika na kina soko kubwa katika ujenzi wa madaraja, nyumba, mabodi ya magari na bidhaa nyingine za chuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Kamba Ngomeni Tanga kilikuwa kikizalisha kamba zitokanazo na zao la katani ambazo kwa sasa, mkonge umepata soko kubwa katika Soko la Dunia na kwamba bidhaa zitokanazo na katani zinahitajika sana kwa matumizi mbalimbali. Zana/ bidhaa za mkonge zina soko na mahitaji yake ni ndani na nje ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni mategemeo yangu kuwa kutokana na soko kuwa kubwa Serikali itawekeza upya au kutafuta wawekezaji makini na wenye uwezo wa kuendesha viwanda vya korona na viwanda vya kamba kwa lengo la kutoa ajira kwa Watanzania, lakini pia kuiwezesha Serikali kupata kodi na kuongeza mapato ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanga kulikuwa na viwanda vya sabuni kama Foma, Mbuni, Gardenia, mafuta ya nazi (nocolin) na kadhalika. Viwanda vyote nilivyovitaja vimekufa katika zoezi la ubinafsishaji mbovu lakini pia ukosekanaji wa umeme wa uhakika; vile vile kodi kubwa zilizopo. Hivyo nadhani kwa sababu nilizozitaja nimeeleweka. Ushauri wangu; viwanda vyote vilivyokufa au vilivyoshindwa kuendeshwa na wawekezaji wanavyovimiliki, vifufuliwe kwa kupewa wawekezaji wapya lakini pia Serikali ihakikishe kunapatikana yafuatayo:-

(i) Umeme wa uhakika na bei nafuu;

(ii) Mfumo wa kodi uwe rafiki kwa wawekezaji (VAT/CUSTOMs DUTY);

(iii) Vivutio vya kibiashara (Tax Holiday et cetera); na

(iv) Sheria ziwe rafiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Viwanda Vipya vya Nyama na Ngozi. Tanzania ni nchi ya tatu Afrika kwa kuwa na mifugo mingi lakini nchi yetu haipati/haifaidiki na mifugo hiyo ukilinganisha na nchi kama Ethiopia na Botswana. Vile vile mifugo (ng‘ombe) hutoa maziwa ambayo pia tunashindwa kuyasindika na kusimamia na hatimaye tunaagiza nyama za kopo (beaf tin) na maziwa ya kopo ya Lactogen, NIDO, NAN, Kerrygold, kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ethiopia imepata USD milioni 186 (2016) kwa mazao ya ngozi na inatarajia kuongeza US $ milioni 90 (2017) na kufikia USD 276 (2017). Je Tanzania inapata USD ngapi kwa 2015 – 2020? Zaidi ni migogoro ya wakulima na wafugaji, Maafisa Wanyamapori kuwapiga risasi ng’ombe na wafugaji na kashfa ile na kusababisha Mawaziri kujiuzulu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili (scandal) ya Wizara ya Maliasili na Utalii ilisababisha baadhi ya Mawaziri kujiuzulu. Ushauri wangu, (Serikali itafute wawekezaji wakubwa kuboresha sekta ya mifugo ili viwanda vya nyama na ngozi vijengwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vya kusindika mboga/matunda. Tanzania imejaaliwa na Mwenyezi Mungu katika mikoa na kanda aina mbalimbali za matunda na mboga mboga. Pia Tanzania inayo mito na maziwa yenye maji ya kutosha na kama tukifanya Irrigation scheme for fruits and vegetables tunaweza kupata mapato kwa wananchi (kujiajiri wenyewe). Serikali za mitaa zitapata mapato na Serikali kuu pia itapata mapato kutokana na kodi baada ya kulifanyia kazi kikamilifu eneo hili la kilimo cha matunda na mboga mboga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mazao ya Matunda na Mboga Mboga Katika Mkoa wa Tanga. Mkoa wa Tanga unazo wilaya nane (8) na kati ya hizi zipo ambazo ni wazalishaji wakubwa wa mazao husika na wilaya hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Muheza ni Wilaya inayozalisha matunda aina ya machungwa, machenza, madalanzi, malimao, mashuza, mafenesi na mapera, ambayo ikiwa Serikali itatafuta wawekezaji wa viwanda vya kusindika matunda ajira na mapato yatapatikana. Lushoto, ni wazalishaji wakubwa wa aina zote za mbogamboga na matunda (nyanya, vitunguu maji/saumu, cabages, spinaches, matango pamoja na pilipili hoho. Aina zote hizi zina soko kubwa katika Soko la Dunia (Europe na America) Serikali ilete wawekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda bila umeme ni sawa na gari bila mafuta. Umeme ndio Enquire kuu za viwanda, bila ya umeme wa uhakika, wataalam waliobobea na wenye weledi na uzalendo hata tujenge viwanda vingi kama utitiri baada ya muda vyote vitakufa tena. Ushauri, Serikali inahitajika kuhakikisha kwamba umeme wa uhakika unapatikana, mifumo ya kodi iwe rafiki na tuondoe urasimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.