Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii. Nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mwijage, kwa hotuba nzuri ya bajeti yenye kuleta matumaini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuweka mbele mapinduzi ya viwanda. Juhudi hizi tumeanza kuona matunda chanya na Tanzania ya viwanda sasa inaonekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kisiwa cha Mafia wamehamasika katika kilimo cha miwa na kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kupata mazao mengi, lakini tatizo limekuwa ni kutokuwepo na kiwanda cha kuchakata miwa ili kupunguza ukubwa wa mzigo na kujirahisishia usafirishaji wa mazao. Namwomba tu Mheshimiwa Waziri kupitia Shirika la SIDO, aangalie uwezekano wa Mtaalam kuja na kiwanda rahisi kusaidia wakulima wa miwa wa Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kisiwa cha Mafia pia ni maarufu kwa ulimaji wa zao la nazi. Kwa kuwa zao la nazi linatoa mafuta na tui kwa matumizi ya mwanadamu, nichukue fursa hii kumwomba Mheshimiwa Waziri aangalie uwezekano wa kutupatia kiwanda kitakachochakata mazao yatokanayo na nazi ili kusaidia kukuza kipato cha mwananchi wa Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais mwaka anazindua Bunge hili la Kumi na Moja alionesha masikitiko yake ya kukosekana kiwanda cha kusindika samaki kwa ukanda mzima wa Pwani kuanzia Mkoa wa Tanga mpaka Msimbati Mtwara. Namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa ukaribu suala hili la kiwanda cha kusindika samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijadili suala Kitaifa la viwanda. Niiombe tu Serikali yangu kwenye kuelekea viwanda, mkazo uwekwe kwenye kuweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi badala ya Serikali kujenga viwanda vyake yenyewe. Serikali haifanyi biashara, Serikali isubiri kutoza kodi na kupata fursa ya kutoa ajira kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, naomba Serikali ianzishe vyuo aina ya VETA katika makambi yetu ya Jeshi la Kujenga Taifa. Aina ya viwanda inayokuja sasa, lazima tuandae vijana wetu kwenye kada za kuendesha mashine (Machines Operators). Hii itasaidia kwao kupata ajira kwenye viwanda hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuoanisha uanzishaji wa viwanda na kilimo chetu. Sisi mazao yetu mengi ya matunda yanaoza mashambani kwa kukosa kiwanda cha kusindika matunda.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ukweli kwamba tuna kiwanda cha Azam pale Mkuranga, lakini kiasi kikubwa wanaagiza matunda concentrate kutoka nje ya nchi. Hii inatokana na ukweli kwamba matunda yetu hayalimwi kitaalam na kupelekea shamba moja kutoa matunda yenye ladha tofauti na kushindwa kutengenezwa juice. Kilimo cha kisasa ndiyo namna pekee ya kuoanisha ladha ya mazao haya ya matunda ili yaweze kutumika kutengeneza juice.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.