Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu kwa maisha na maendeleo ya Watanzania. Vision ya viwanda, Mwalimu Nyerere aliwahi kuiona na ilikuwa implemented kuanzia miaka 1967, ambapo mikoa mbalimbali ilionesha kwa vitendo kwa kuwa na viwanda na vilikuwa vikifanya kazi. Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa Mikoa ambayo ilinufaika na vision hiyo kwa kuwa na viwanda zaidi ya 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tunavyozungumza viwanda vilivyokuwa vimewekeza katika Mkoa wa Morogoro kwa miaka hiyo ya 1960 viliwezesha wananchi wa Mkoa wa Morogoro kupata fursa za kupata ajira. Ilikuwa siyo rahisi kwa Mkoa wa Morogoro kupata house girl; ilikuwa siyo rahisi kwa Mkoa wa Morogoro kupita kukuta watu wanacheza bao; ilikuwa siyo rahisi kwa Mkoa wa Morogoro kupita kukuta Wamachinga; ilikuwa siyo rahisi kupita Mkoa wa Morogoro ukakuta watu wamekaa vijiweni, kwa sababu kulikuwa na viwanda na viwanda vile vilikuwa vikitoa ajira kwa wananchi walio wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo sasa, namwomba Mheshimiwa Waziri, nimejaribu kupitia sana katika taarifa yake hii, iko wapi mikakati ya kufufua viwanda vya Mkoa wa Morogoro vilivyokufa? Ubinafsishaji wa viwanda badala ya kuongeza efficiency, ubinafsishaji wa viwanda umekuwa ni wa kunufaisha watu wachache ambao wamechukua viwanda kama collateral kwenda kukopa katika mabenki, kunufaika wenyewe na wananchi kukosa ajira. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha, atuambie uko wapi mkakati halisi wa kuvirudisha viwanda vya Mkoa wa Morogoro? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Morogoro hivi sasa kuna viwanda, kwa mfano, Kiwanda cha Canvas ambacho kilikuwa kikinua hata pamba kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa, lakini hivi sasa wameacha kulima pamba kwa sababu kiwanda kimekufa. Kipo kiwanda cha Asante Moproco cha Mafuta; kiwanda hiki wananchi walikuwa wanalima alizeti kwa sababu walikuwa na uhakika wa sehemu ya kuuza. Hivi sasa wananchi hawalimi alizeti kwa kuwa hakuna kiwanda. Kipo kiwanda cha Komoa, kipo kiwanda cha CERAMIC, Morogoro Leather Shoe, UNNAT cha Matunda ambacho kilikuwa kikinunua matunda ya wananchi wa Mkoa Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri atupe mkakati wa kufufua viwanda hivi. Siyo hivyo tu, atuambie Serikali ina mpango gani wa kuwachukulia hatua wawekezaji hawa ambao kwa makusudi waliviua viwanda hivi? Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha watu hawa ambao wengine kwenye viwanda vile wameuza vipuri, hivi sasa yamebaki kuwa magodauni na wengine wanachunga mbuzi. Je, ni sahihi kwa watu hawa kutumia collateral kupata faida lakini wanaviua viwanda badala ya kunufaisha? Atuambie, Mheshimiwa Rais alipita Morogoro akasema atalishughulikia, tunataka kuona kwa vitendo kwamba hawa wamiliki wa viwanda ambao wameziweka ajira za wananchi wa Mkoa wa Morogoro mfukoni, wanachukuliwa hatua gani kama kweli mna nia ya kuleta viwanda kwa nchi hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la nyumba. Wakati wa ubinafsishaji zipo nyumba ambazo zilikuwa zinamilikiwa na viwanda vile na zilikuwa ni nyumba za Serikali. Zile nyumba hivi sasa zinamilikiwa na watu ambao ndio waliobinafsishiwa viwanda, lakini hivi sasa wafanyakazi wa Serikali hawana nyumba, hawana pa kuishi. Wale watu wamepeana nyumba zile kinyemela, hawalipi pango na hawalipi kodi. Maofisa wanakosa mahali pa kuishi lakini watu waliobinafsishiwa wanang’anga’nia kuishi kwenye nyumba hizi. Hii siyo sahihi kabisa. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri amulike, aangalie ili hatua mahususi ziweze kuchukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia biashara ya mwendokasi; mabasi ya Dar es Salaam, tuna mengi ya kujiuliza. Biashara hii imekuwa kama ni ya watu wachache. Serikali imeamua kuleta mabasi ya mwendokasi kwa lengo la kusaidia kupunguza msongamano, lakini kuna wazawa, kuna Watanzania ambao walikuwa wakifanya biashara za daladala ambao nao walikuwa na uwezo wa kupata fursa ya kuwekeza katika mwendokasi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)