Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Yosepher Ferdinand Komba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda ku-declare interest angalau haiko kwenye hela lakini mimi nimetokea Tanga na mnajua historia ya Mkoa wa Tanga katika suala la viwanda. Mnajua Tanga miaka ya 1980 ni kati ya Mkoa ambao ulikuwa maarufu sana kwa viwanda kwa Tanzania hii. Tunavyoongea sasa hivi, viwanda vingi vimefungwa, vilivyobinafsishwa, vimekufa, watu wameiba vifaa, viwanda Tanga hakuna tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanga tumejaliwa kuwa na bandari, viwanja vya ndege na reli ambayo mpaka sasa hivi hatujajua Serikali lini itaamua kutujengea kwa kiwango cha standard gauge.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi pia natokea Muheza, Wilaya ambayo ni maarufu sana kwa kilimo cha matunda hasa machungwa. Wilaya ambayo ina hali zote za hewa tunazozijua; kuna hali ya baridi na joto, kiasi kwamba tunaweza kulima mazao yanayotokana na baridi na mazao yanayotokana na joto.

Mheshimia Naibu Spika, nakumbuka Mheshimiwa Waziri wa Viwanda niliwahi kumgusia suala la Muheza nikaomba kwamba atafute mwekezaji kwa ajili ya machungwa yetu yanayozalishwa Muheza. Wakulima wamekuwa wakipata hasara sana ya machungwa yanayozalishwa pale, yamekuwa yakioza. Wamekuwa kama wana uwezo zaidi kutegemea soko la Kenya lakini Tanzania hakuna kiwanda karibu; Tanzania, Muheza hakuna kiwanda wakulima wanapata shida sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri tunajua lengo la Tanzania ya viwanda ni jema, lakini kama tusipokuwa makini hatuwezi kufikia huko. Kama hamkujiandaa, tafuteni namna nyingine ya kuliweka sawa. Kwa nini nasema hivyo? Waziri wa Viwanda yeye kama yeye hawezi kufikia lengo la viwanda kama Wizara nyingine hazijaonesha ushirikiano kwako. Yeye kama yeye hawezi kufikia kwenye viwanda, kama Wizara ya Fedha haijaamua kuona kama suala la viwanda ni muhimu. Pia hawezi kufikia lengo kama Wizara ya Ardhi na Wizara ya Usalama na mambo mengine hazijamsaidia. Kwa hiyo, inatakiwa suala la viwanda liwe ni la nchi, siyo Wizara. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa na miundombinu mizuri kwa ajili ya uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee viwanda na wanawake. Sensa ya viwanda inaonesha asilimia 99.15 ni viwanda vidogo sana na viwanda vidogo. Kwa haraka haraka ukiangalia katika sensa hii, utaona viwanda vidogo sana ni kati ya mtu mmoja mpaka wanne; viwanda vidogo ni kati ya mtu mmoja mpaka 50. Ukiangalia kwa undani zaidi utakuta hivi viwanda vidogo vingi vinamilikiwa na wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, sijaona popote kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri ambapo ameonesha namna ambavyo atamsaidia mwanamke aingie kwenye uchumi wa viwanda akiwa anajiaamini. Tunajua hali ya kipato cha wanawake wengi wa nchi hii ni cha chini. Wizara haijaandaa utaratibu wowote kumwezesha mwanamke ambaye kwa asilimia kubwa ndio amewekeza kwenye hivi viwanda vidogo aweze kujikwamua. Kwa hiyo, tuna viwanda vingi vya mtu mmoja mpaka watano, tutafika lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kitu kingine tunapoongelea Tanzania ya viwanda, lazima tukubali na tuamue tunataka viwanda vya aina gani? Hatuwezi kuwa na viwanda nchi nzima kwa mara moja. Lazima tutenge maeneo, lazima tuwe na point ya kuanzia. Tanzania tunataka viwanda ndiyo, tunataka viwanda vya aina gani? Tunataka viwanda vya kutumia malighafi gani? Tutakapokuwa tumefanya hayo maamuzi, itakuwa ni rahisi. Hatuwezi kujenga viwanda nchi nzima, lazima tuamue baada ya miaka 10 miaka 15 tunataka katika viwanda Tanzania ijulikane katika kitu gani? Ziko nchi ambazo zinajulikana kwa ajili ya kuzalisha products za maziwa peke yake. Tanzania tunataka tujulikane kwenye nini katika viwanda? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niongee suala la VETA. Tunajua inatakiwa kuwe na elimu na ujuzi wa kutosha ili tuingie kwenye viwanda tukiwa tunajiamini. Kumekuwa na tatizo kubwa sana katika Vyuo vyetu vya VETA, siyo tu udahili lakini pia vifaa na mashine zinazotengenezwa VETA zina bei ghali kuliko sehemu nyingine yoyote. Sasa kwa namna hii hamwezi ku-encourage viwanda wakati watengenezaji wetu wa ndani wanapitia mazingira magumu katika kuanda hizo zana za kufikia kwenye viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali isaidie wale wataalam wa VETA ambao wanatengeneza mashine ambazo zinaweza zikatumika kwenye nchi yetu, wapunguzieni kodi ambazo ni mzigo kwa wafanyabiashara wengi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)