Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kidogo katika hii hotuba ya bajeti ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba wote tunajua kazi kubwa ya ulinzi inayofanywa na Jeshi letu, ni kazi nzuri na niseme tu kwamba hasa kwetu sisi ambao wakati mwingine tumekuwa watembezi tembezi kidogo katika nchi za wenzetu, ukija Tanzania ndiyo unaweza kujua kwamba kweli Jeshi letu linafanya kazi nzuri kwasababu ukilala una uhakika wa kuamka kesho yake. Kwa hiyo baada ya kuwapongeza kwa hiyo kazi nzuri lakini kuna baadhi ya mambo ambayo tunapaswa tuendelee kuwasaidia na ambayo yatahakikisha kwamba kazi zao zinakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; Jeshi letu bado lina matatizo makubwa ambayo ni pamoja na madeni. Tunaamini kwamba wanashindwa kufanya mipango yao mizuri kutokana na madeni na kwa maana ya ukwasi wa fedha. Kwa mfano kati ya miradi mizuri waliyonayo ni pamoja na kile kiwanda cha kutengeenza magari kile cha Nyumbu, ni kiwanda ambacho tulitakiwa tuone matokeo yake ya haraka, lakini naamini kwamba kinasua sua hii yote si kwa sababu nyingine lakini ni kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. Kwa hiyo, ningeomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwasaidia ili waweze kufanya kazi zao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba Jeshi wanayo madeni, kwa maana ya wale wazabuni. Kwa hiyo, napo kuna tatizo kubwa kwa sababu fedha wanazopata hazikidhi mahitaji yao, kwa hiyo, Serikali inahitaji kuangalia namna ya kuendelea kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tu niseme kwamba katika miradi waliyonayo, kwa mfano hawa wenzetu wa JKT; JKT kwangu mimi ninavyofahamu leo tukiamua kuitumia vizuri inaweza ikaleta impact kubwa hasa kwa vijana wetu. Nadhani Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakubaliana na mimi kwamba kila linapotoka tangazo kwamba sasa kuna nafasi za kwenda JKT katika kila Wilaya unakuta wapo vijana zaidi ya 1,000 wanajipanga pale msululu kwa ajili ya kuomba waende JKT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na wote tunakubaliana kwamba katika nchi hii kama kuna tatizo kubwa tulilonalo ni tatizo la ajira kwa vijana. Sasa basi JKT kwanza wanafundisha maadili, lakini wanaendelea kufundisha vijana kuipenda nchi yao. Kwa hiyo, katika yale mafunzo wanayofundisha ambayo ni pamoja na mafunzo ya kufanya kazi ambayo ni ya ujuzi ni imani yangu kwamba kama Serikali itaweka nguvu kubwa kwa JKT basi kwa kiasi kikubwa itapunguza tatizo la ajira kwa hawa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kwamba kwa yale mafunzo ambayo vijana wangekuwa wanayapata pale mfano unazungumzia mafunzo ya kilimo. Ingekuwa ni rahisi zaidi vijana wakafika pale wakapata mafunzo ya uvuvi na mafunzo mbalimbali, sasa wakitoka hapo ni rahisi zaidi wakasaidiwa kidogo na wakaenda kuanza maisha yao kuliko hivi ambavyo tunavyowaacha vijana wanahangaika mtaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninaamini kwamba JKT ni mahali pekee ambapo panaweza pakaleta impact kubwa. Unaona tunafikia mahali tunakuwa na upungufu wa chakula, lakini tunayo mabonde mazuri, na mengine; labda niseme tu moja, kwa mfano ukiangalia pale kwenye Wilaya ya Musoma walipewa eneo kubwa lakini hawakupewa uwezo; kwa hiyo, mwisho wa yote wameendelea tu kuliangalia lile eneo mpaka mwisho. Kwa hiyo, tunadhani kwamba hayo ni baadhi ya mambo ambayo Serikali ikiwasaidia basi wataweza kufanya mambo mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja karibu na mwisho; kwa bahati nzuri hili tulishalizungumza na Mheshimiwa Waziri; ni suala la fidia kwa ajili ya wale wananchi walioombwa waondoke kwenye eneo ambalo Jeshi imelichukua, eneo la Makoko. Hili ni suala ambalo tumehangaika nalo sasa zaidi ya miaka 15. Tangu mwaka 2005 tumekuwa tukilizungumzia lakini hadi leo. Jeshi walishakubali kwamba wanalipa fidia, kwa maana ya Serikali, lakini hadi leo kila leo wale wananchi wameshindwa kuyaendeleza maeneo yale, lakini vile vile wameshindwa kuhamia mahali pengine kwa sababu bado hawajalipwa fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwisho, nadhani ni wiki tatu zilizopita wale wananchi walituma wawakilishi wao, bahati nzuri baada ya kuona nimezidiwa niliwapeleka moja kwa moja tukakaa na Mheshimiwa Waziri na akahaidi kwamba kwenye bajeti hii tutawalipa fidia. Sasa Mheshimiwa Waziri naomba commitment yako utakaposimama kuzungumza uwahakikishie hawa wananchi ili wakae wakijua, kama ulivyoniambia siku ile, wawe na uhakika kwamba kama kweli watapata hizi fedha zao. Maana sasa ukiangalia ni muda mrefu na hata kati ya hao wenye hizo familia wengine walishafariki, sasa familia zao nazo zipo pale zile nyumba zinaelekea kuanguka lakini wameshindwa waende wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni imani yangu kwamba baada ya kupata hayo majibu mazuri kwa mwaka huu tunaweza kumaliza hilo tatizo la wananchi ambalo limewasumbua kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo na mimi naungana na wenzangu kusema naipongeza Serikali yangu kwa kazi nzuri ambayo inaifanya, na ninaendelea kusema tupo pamoja na ni jukumu letu sisi kuendelea kuisaidia ili waendelee kutekeleza majukumu hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante.