Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuweza kunipatia nami fursa kuchangia bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ambayo ni muhimu sana kwa ulinzi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa masikitiko makubwa kwamba tunakaa hapa tunapitisha bajeti ambazo hazina uhalisia na hatimaye utekelezaji wake unakuwa ni wa kusuasua. Waziri wakati anawasilisha bajeti yake hapa ameainisha bayana kwamba fedha za maendeleo ambazo zilikuwa ni shilingi bilioni 248 zimetolewa asilimia 14.5 tu ambazo ni sawa na shilingi bilioni 35.9

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kuna wazabuni wengi sana wanaidai Serikali ambao wametoa huduma kwenye Jeshi letu la JKT pamoja na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Hawa wazabuni wamekopa fedha kwenye benki, wanafilisiwa na wengine wanafariki kwa sababu ya pressure. Nilikuwa naomba Serikali tunapokuja hapa tunatenga hizi bajeti hasa za maendeleo ziwe na uhalisia ili ziweze kwenda kukidhi mahitaji kwa muda wa mwaka nzima kama tunavyokuwa tumepanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine napenda kuzungumzia fedha ambazo zinatolewa kwa ajili ya kupima, kuthamini na kulipa fidia kwa yale maeneo ambayo Jeshi imeyatoa kwa wananchi, tena wakati mwingine bila kufuata Sheria za Ardhi. Katika hili nitajikita zaidi katika eneo ambalo Jeshi la Wananchi wa Tanzania wamejitwalia kule Tarime katika kata ya Nyamisangura na kata ya Nkende ambapo kwa kweli kila mwaka ninakuwa ninasimama hapa naelezea, na Mheshimiwa Waziri amekuwa akiniambia kwamba wanakuja kumaliza kuwalipa fidia. Mwaka jana tulitenga shilingi bilioni 27.7 Mheshimiwa Waziri ameeleza hapa na wote tunaona kwamba haikutolewa hata shilingi 1,000 kwenda kufanya hii kazi; shilingi bilioni 27.7 hata shilingi 1,000 haijatolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa nashauri, kwa sababu wanajeshi kwa mfano kwa Tarime kile kosi kilipewa eneo kubwa sana Kata ya Nyandoto; tunaomba waondoke kwa sababu mmeshindwa kulipa kwa miaka yote hii kuanzia mwaka 2008, tunaomba hawa wanajeshi warudi kwenye maeneo yao kule Nyandoto eneo ni kubwa sana ni pori kubwa kuliko kuja kuchangamana na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi yao iko kule Nyandoto ya kikosi cha 28KJ warudi kule, wakakae kule ili waweze kulinda vizuri dhidi ya mipaka ya Nchi yetu kwa upande wa Kenya. Huku kwenye kata ya Nyamisangura na Nkende wanachangamana sana na wananchi na mmeshindwa kulipa. Kwa hiyo naomba leo Mheshimiwa Waziri uniambie either mnatulipa kwa kipindi cha bajeti ya mwaka huu au mwende mkawaombe wale wanajeshi waondoke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanachokifanya sasa hivi kwanza wanakodisha yale maeneo kwa raia yaani wamepoka maeneo ya wananchi halafu wanakodisha kwa kufanya biashara, zaidi ni maslahi ya watu binafsi kule. Naomba uje na wewe mwenyewe Tarime ukae na wataalam wako tulimalize suala hili. Mimi binafsi kama mwakilishi inaniuma sana ninapoona wananchi wanakaa kwa miaka mingi bila kufanya shughuli za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, wale ndugu zetu wanajeshi ambao wanakwenda kusoma nje ya nchi mnachelewesha kuwapelekea fedha za kijimu, wanakuwa wanateseka sana. Kwa hiyo, naomba kabisa wakati mnapanga bajeti muweze kuzingatia mjue kwamba mnapeleka wanajeshi wangapi kusoma nje ya nchi muwapelekee fedha za kujikimu ili wamalize mafunzo yao wakiwa na utulivu wa akili na kurudi Tanzania kuweza kulinda nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wanajeshi ambao unakuta wanatumwa kwenda kulinda amani kwenye nchi zingine; Kambi za Tanzania za wale wanajeshi wetu wanaokwenda kukaa kule ni mbovu, hazina hadhi ukilinganisha na kambi za nchi zingine ambazo wameenda kulinda amani kwenye sehemu husika.

Tunaomba wakati mnawatuma wanajeshi wetu kwenda kulinda amani huko basi na wenyewe muwape hadhi, wawe na makambi mazuri kama wale wengine ambao wametoka nchi zingine. Ukienda ukiangalia kambi za wanajeshi kule zinatia fedheha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwisho nimalizie kwenye top up allowance. Wanajeshi mara ya mwisho wamelipwa hizi top up allowance ni mwaka wa jana mwezi wa tatu. Sasa hivi ni zaidi ya mwaka hamuwalipi hizi stahiki zao. Tunarudi pale pale, tunapopanga bajeti zetu tupange bajeti yenye uhalisia, tujue kwamba katika Wizara hii tuna mahitaji haya na haya. Tuweze kutimiza yale mahitaji ambayo ni ya muhimu, kwa mfano hii top up allowance ni hitajio ambalo mtu anapokuwa anafanya kazi anajua kabisa anatakiwa alipwe. Sasa inapita mwaka bila kuwalipa; na ndiyo maana hotuba ya kambi rasmi ya Upinzania imejikita zaidi kuelezea matatizo na maslahi ya wanajeshi wetu.

Kwa hiyo, naomba kipekee kabisa; Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeelezea kwa kina sana, dakika tano ni chache kuchambua, naomba Mheshimiwa Waziri uifanyie kazi yale yote ambayo yamebainishwa kwenye Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni yafanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kuhusu wanajeshi wetu wastaafu na wale ambao unakuta wameaga dunia. Ni dhahiri na mimi mwenyewe nina ndugu ambao wengine waliaga dunia na wengine ni wastaafu wanakuwa wanaangahika sana kupata mafao yao; naomba muwatendee haki. Hawa ndugu unakuta wametumikia nchi hii kwa uaminifu zaidi, lakini ikija kwenye mafao inakuwa wanatendewa ndivyo sivyo, nashukuru.