Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote kwanza naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na Kambi ambazo zimezungukwa na maeneo ya raia. Naomba Serikali ilishughulikie suala hili kwa haraka kwa sababu tayari kuna baadhi ya maeneo ya kambi ukipita nje yanayofanyika ndani ya Kambi ya Jeshi yote raia wanayaona. Mfano Kambi ya Mwanyanya inahitaji ukarabati wa kujengewa ukuta. Pia naomba Serikali sasa ilipe fidia lakini pia izungumze na Serikali kupata maeneo mengine kwa ajili ya Jeshi, maeneo yawe ni ya Serikali yasiyohitaji watu kulipwa fidia ili kuweka akiba kwa hapo baadaye kwa ujenzi wa Kambi na matumizi mengine ya Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira za JKT, nashauri pia isiwe kwenye vikosi vya Jeshi tu lakini pia hata ajira za taasisi nyingine za Serikali na Serikali kwa ujumla iwafikirie vijana wetu hawa wanatoka katika Jeshi la Kujenga Taifa ili wapewe kipaumbele kwa sababu vijana hawa tayari wameshafunzwa uzalendo, ujasiri pamoja na maandili ya kuitumikia nchi na Taifa kwa jumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalipongeza Jeshi letu kwa kukabiliana na vitendo mbalimbali viovu vinavyofanyika katika mipaka yetu ndani na nje ya Tanzania ikiwemo kudhibiti mambo ya uharamia na mambo mengine yote yanayojitokeza yanayoashiria mambo ya kigaidi na mengineyo. Nalipongeza sana Jeshi letu kwa kazi nzuri linayoifanya katika kusaidia mambo mbalimbali yakiwemo majanga na maafa yanayotokea ndani ya nchi, wamekuwa mstari wa mbele sana kutoa msaada wa hali na mali na nguvu zao zote katika kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe pongezi za dhati kabisa kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania, Waziri wa Ulinzi, Mkuu wa Majeshi, Kamanda wetu wa Majeshi na Majeshi yote nchini Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kulinda nchi yetu, mipaka yetu na raia kwa ujumla. Kama ilivyotokea kuashiria kwa uvunjifu wa amani uliotokea Zanzibar wakaenda pale kwa ajili ya kulinda amani ya nchi na hawakwenda kushiriki uchaguzi wamekwenda kusimamia amani ya nchi na wameifanya kwa uzalendo mkubwa na nchi sasa iko shwari nchi iko salama, mipaka ya nchi yetu iko salama, tunawashukuru wanajeshi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba mahitaji yao ya msingi tuwasaidie, yakiwemo marupurupu na mambo mengine ya kupandishwa vyeo na madaraja ili waweze kufanya kaz zao kwa weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninaloliomba, mwenzangu alichangia kuhusu vituo hivi vya afya, ni kweli vituo vya afya na Hospitali za Jeshi zinatoa msaada mkubwa sana kwa raia. Naomba ziongezewe vifaa na ziongezewe watalaam na kuwapatia mafunzo zaidi ikiwemo kuwapatia mafunzo wanajeshi wetu ili kukabiliana na hatari zinazojitokeza za kimataifa za uharamia na ugaidi. Naomba mafunzo hayo yaendelee kutolewa zaidi kwa wanajeshi wetu na hasa vijana wadogo ambao ni nguvu kazi kubwa ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niongezee tu kwa kusema kwamba Jeshi letu ni imara, Jeshi letu linafanya kazi nzuri, na ninakipongeza kwa dhati kikosi kile ya Makomandoo wa Jeshi. Mheshimiwa Waziri kikosi kile ukione kwa jicho lingine zaidi la huruma kwa sababu ndicho kikosi ambacho tunakitegemea yatakapotokea majanga na maafa makubwa ndani ya nchi yetu, lakini Mwenyenzi Mungu naomba yasitokee hayo, nchi yetu iendelee kuishi tuishi kwa amani na salama, mipaka yetu iwekwe salama, na nchi yetu iwekwe salama. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.