Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

Hon. Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nimepokea taarifa kwa Mheshimiwa Fakharia Shomar akisema kwamba uchaguzi wa Zanzibar ulitawaliwa na Jeshi la Wananchi la Tanzania, hongera sana Mheshimiwa Fakharia tumepokea taarifa na sisi upande wa pili tujiandae zaidi kwa kushinda kura si kwa njia nyingine yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rweikiza nikwambie tu kwamba Jeshi la Marekani wakati wa amani linafanya shughuli za uchumi, watu waliotembea sana shughuli hizo wanajua na majeshi mengi duniani wakati amani yanafanya shughuli za uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukarasa saba Mheshimiwa Waziri anasema dhima kubwa ni kuwa na jeshi dogo na mahiri la ulinzi wa nchi lenye weledi. Hatuwezi kuwa na jeshi dogo, mahiri na lenye weledi ikiwa bajeti ya maendeleo yenye shilingi bilioni kumi unatoa shilingi bilioni moja, hakuna kitu. Hatuwezi kuwa na jeshi lenye weledi na mahiri ikiwa bajeti ya maendeleo ya JKT shilingi bilioni nane unatoa shilingi bilioni moja, hakuna kitu, hapo hakuna weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutaki kuona sisi umeme unakatwa kwenye Kambi za Jeshi la Wananchi wa Tanzania, hatutaki. Hatutaki kuona kabisa wanajeshi wanafanya kazi pamoja na mkataba wao kula kiapo ndani ya masaa 24 lakini kwamba baada ya saa tisa na nusu ration allowance yao nayo inaondoka, hatutaki. Tunataka kuona ration allowance ya wanajeshi wetu inapandishwa si kwamba ration allowance inaondolewa kiaina aina hatutaki. Hiyo ilikuwa ni chombeza ya kwanza mambo hasa yanakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalamiko ya muda mrefu sana juu ya fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa na Serikali kwa ajili ya Jeshi la Wananchi. Maeneo haya ambayo wanajeshi wana shughuli zao jumla yake ni maeneo 262, kati ya maeneo haya ambayo yamepimwa ni maeneo 17 tu. Kwa kweli hii ni njia ya dhuluma, wananchi wamenyanganywa, wananchi wamedhulumiwa na mpaka leo Jeshi la Wananchi katika maeneo 262 maeneo 17 waliyoyapima na kuthamini hakuna fidia na mengine hayajapimwa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 1966, 1970 mpaka leo miaka 50, wananchi wengine wameshakufa wameacha watoto wao wanadai, wala hawajui waende wapi, mmechukua maeneo yao mbalimbali, mbona mambo mnayotaka kufanya mnayafanya? Mbona hawa hamuwapi fedha zao? Hamtoi fidia zao? Kuna mambo mengine ambayo mnayafanya na fedha zinapatikana, kwa nini hamtoi fidia kwa hawa na tatizo ni nini? Nakuomba Mheshimiwa Waziri utuambie utakapokuja hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Fungu 57 - Wizara, katika mwaka 2016/2017 ulikuwa na shilingi bilioni 27.7 ni kasma 2004, zilitengwa hizi fedha hakuna shilingi iliyotoka! Wananchi wasemee wapi sasa? Wananchi wanadhulumiwa na wananyonywa hawana mdomo wa kusema, mdomo wao ni sisi, lakini Serikali inasema inatafuta fedha, fedha ikipatikana, mbona fedha za kuhamia Dodoma mlizipata, zilikuwa kwenye bajeti? Fedha za kuhamia Dodoma mlizipata wapi na hazikuwa kwenye bajeti? Kwa nini hawa fedha zao hamuwapi? Kuna wazee wamekufa wameacha watoto wao nao wamekufa, shida kweli Tanzania jamani! Twende wapi sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo mambo ya msingi ya kuwasemea wananchi wetu na kuwaonea huruma, kwamba Serikali inasema inawapenda wananchi wake, inawathamini wananchi wake lakini wapi! Miaka 50 fedha zao hamuwapi mnawatesa kwa njaa, tutafika kweli? Hatufiki, shida kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee, ni miaka kadhaa tumesema, tunajifunzaje baada ya mlipuko wa mabomu kule Mbagala na Gongo la Mboto? Baada ya hapo wakasema wanajenga maghala fedha mimi ni mmoja wa walioidhinisha, maghala yamekuwa magofu hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabilioni ya fedha yamepotea, maghala hayaendelezwi yako vilevile. Mungu asijaalie kutokea, likitokea la kutokea nani ataulaumiwa? Maghala mengi ambayo tumetoa fedha yakianzwa hayamalizwi. Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi utakapokuja naomba hili uliseme ni kwa nini mpaka sasa maghala haya bado hayajamalizwa na fedha hizo zimetumika zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sera ya Ulinzi wa Taifa, umesema sana kwenye kitabu chako hiki. Mambo ya Sera bado hujakaa vizuri. Tangu mwaka 1966 mpaka leo sera ni ya zamani. Unataka jeshi la weledi lakini sera ndiyo itakayopelekea sheria, Sheria ya Ulinzi ni ya zamani. Kwa hiyo hili nalo ni tatizo kubwa. Mheshimiwa Waziri sasa utuambie hii sera lini itaweza kukamilika? Tatizo wewe unalijua zaidi, tena sana, tu kwamba utuambie hii sera ya ulinzi wa Taifa ni lini itakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine ningesema jambo linguine, wanajeshi wanakwenda kulinda amani Darfur, DRC na Lebanon wengine wameshaletwa tumeshawazika. Sawa ni kazi zao na wajibu wao lakini mbona familia zao hamzitunzi? Mnawapa fedha za muda wa miezi minne wale vizuka mpaka leo lakini watoto wao hawasomi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inakuwa ni tatizo kubwa, kwamba tumeshaletewa hapa sisi wale maiti tumeshazika lakini watoto hawasomi, familia zimekuwa masikini imekuwa kama wale wanajeshi wastaafu au wengine ambao walikwenda kwenye vita. Tunawapeleka Lebanon, Darfur na kwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri utuambie mpango mkakati wa ziada kuona kwamba watu hawa hasa wajane wanapatiwa fedha zinazostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hayo basi ningeomba kusema kwamba sambamba na hilo Mheshimiwa Waziri utakapokuja utuambie wastaafu walio kuanzia ngazi ya private hadi Brigadier General kwa nini hamrekebishi maslahi yao, tatizo ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ngazi nyingine wanalipwa vizuri wengine hawa mnawadhulumu na wewe ulisha ahidi mwaka wa jana kwamba kuanzia Private hadi Brigadier General, wastaafu hawa wa Jeshi hasa wale wa zamani basi mafao yako katika machakato na mkasema kwamba yako katika hatua ya mwisho ni hatua ipi, mbona mnachelewa sana na hakuna kitu? Naomba Mheshimiwa Waziri na hili uliseme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache, nashukuru lakini muda wangu naona kama mmenibia.