Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hotuba hii ya Wizara muhimu sana. Pili, nampongeza sana Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, kwa hotuba ambayo imeweza kuchambua, kukosoa na kutoa mapendekezo ya namna gani ya kuboresha. Vile vile, nampongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara kwa kuleta maoni ya Kamati na maoni ya Kamati ndiyo maoni ya Bunge, kwa sababu Kamati inafanya kazi kwa niaba ya Bunge. Naamini kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri ataweza kuyafanyia kazi yote haya; hotuba ya Waziri kivuli na hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ili kuweza kuboresha kazi ambazo tunafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 mwezi kama huu tulipokutana kwa ajili ya kujadili hotuba ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Tanzania ilikuwa inauza nje bidhaa za viwanda za thamani ya Dola za Kimarekani bilioni
1.4 kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya mwezi Machi, 2016. Bidhaa za viwanda ziliingizia Taifa mapato ya fedha za kigeni wakiwa ni wa pili baada ya utalii na wakiwa mbele ya dhahabu ambayo iliingiza Dola za Kimarekani bilioni 1.2; utalii bilioni mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tumekutana mwaka mmoja baadaye kwa kuchukua mwezi Machi, 2016 na mwezi Machi, 2017 bidhaa za viwanda ambazo tunauza nje, zimeshuka kwa Dola za Kimarekani milioni 500 kutoka 1.4 mpaka 0.9 million Dollars. Sasa tunaposimama hapa na kusema kazi inafanyika, Mheshimiwa Waziri atusaidie kwamba iwapo kazi inafanyika, kuna ongezeko la uzalishaji, ni kwa nini mauzo yetu nje yamepungua kwa kiwango kikubwa kiasi hiki?

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ndiyo mambo ambayo ni vizuri sana Waheshimiwa Wabunge wazingatie. Kwa sababu bidhaa za viwanda zinazouzwa nje zinavyopungua, maana yake ni kwamba viwanda vyetu vya ndani vimepunguza uzalishaji; maana yake ni kwamba kuna watu wapoteza kazi; maana yake ni kwamba kuna mapato ya Serikali ambayo yamepotea. Sasa ndani ya miezi 12, tumepoteza mauzo nje kwa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 500. Sijui ikifika 2020 kama kutakuwa kuna hata senti moja ambayo tutakuwa tunaipata kutokana na mauzo nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tuna tatizo kubwa kwamba tuna viwanda ambavyo vimekuwepo, lakini uwezo wetu wa kulinda viwanda vyetu umekuwa ni mdogo sana. Mheshimiwa Waziri ni shahidi wa malalamiko ambayo anapelekewa kila mwezi ya watu ambao wanaingiza nguo kinyemela katika nchi yetu, wanaingiza mafuta ya kula kinyemela katika nchi yetu, wanaingiza battery kinyemela katika nchi yetu, zinakuwa na bei ndogo; na matokeo yake ni kwamba viwanda vya ndani vinashindwa kushindana nao katika soko na tunapoteza ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mfano mzuri sana; jana niliangalia takwimu za kiwango gani cha battery tumeagiza kutoka China kwa miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016. Ukienda Idara ya Customs ya China, utakuta kwamba kati ya Januari mpaka Septemba, mwaka 2016, kwa records za China, tuliagiza battery za thamani ya Dola za Kimarekani milioni 36.5, kwa takwimu za China.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kuangalia Idara yetu ya Forodha hapa, battery ambazo zimeingia nchini na ukilinganisha na TBS, battery ambazo wamezifanyia ukaguzi kuona ni ngapi zimeingia nchini ni za thamani ya Dola za Kimarekani milioni 5.3. Maana yake ni kwamba, kuna battery nyingi sana ambazo zinaingia nchini hazipiti katika njia za kawaida. Viwanda ambavyo vinazalisha battery hapa nchini kama Panasonic ambavyo vimeajiri watu, vinashindwa ku- compete na hizo battery zinazotoka especially China. matokeo yake ni kwamba tutaongea humu kuhusu viwanda lakini in real sense tunaviua hivyo viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni mambo ambayo tungetegemea kuona Mheshimiwa Waziri akihangaika nayo, kwa sababu wahenga wanasema “Ni bora ndege ambaye unae mkononi kuliko ndege ambaye yuko juu ya mti ambaye unataka kwenda kumtungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo nataka kulizungumzia; sisi tuna miradi mikubwa mingi sana, miradi mingine ni ya mabilioni ya fedha. Kuna miradi ambayo inatoa fedha nje na kutengeneza ajira nje. Kwa mfano, manunuzi ya ndege, tunaposema tunanunua boeing, maana yake ni kwamba tunapeleka ajira Marekani. Kuna miradi ambayo inatengeneza ajira ndani na ingeweza kwa kiwango kikubwa kuchochote ukuaji wa Sekta ya Viwanda na mfano mzuri sana ni reli.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mradi wa zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni saba kwenye reli. Reli raw materials zake ni nini? Sehemu kubwa ni chuma. Unahitaji tani 50 za steel, chuma cha pua, kujenga kilomita moja ya reli. Sasa hivi sisi tumewapa Waturuki mkataba. Wataagiza kila chuma ambacho kinakuja kwenye reli yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Deo pale amezungumzia Mchuchuma na Liganga; siyo kama hatuna chuma; tunacho chuma Mchuchuma na Linganga. Kabla ya kuanza kufikiria kutandika haya matararuma ya reli, ilitakiwa tuwe tayari tumejenga uwezo wa kuzalisha kule ili fedha zote zibakie ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashindwa kuelewa; mimi kwa kweli sielewi. Hivi Mheshimiwa Mwijage mnakaa kwenye Cabinet Baraza zima, mkajadili hii mipango? Kwa sababu mkikaa, lazima kuna mtu atasema aah, huu ujenzi mimi miradi yangu fulani itaweza kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajenga mabehewa. Mabehewa yana viti. Hivi wamefikiria namna gani ya kuendeleza zao la katani ili viti vya kwenye mabehewa viweze kuwa ni viti vya katani! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna concrete, mmeandaa vipi watu ambao wanazalisha kokoto kwa ajili ya ku-supply kwenye reli? Hili ndiyo fungamanisho, kwa sababu una fedha, una dola shilingi bilioni saba zitakazoingia ndani ya nchi, over a period of five years or seven years, hizi fedha kama seventy percent zinatoka nje, tunafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, angalieni interior decoration za mabehewa, ni ngozi. Mmekaa mkafikiria namna gani ya kufungamanisha Sekta ya Ngozi na mabehewa? Haya ndiyo mambo ambayo tungependa kuyaona tukiyajadili. Kwa sababu hizi huhitaji foreign direct investments, hizi ni fedha ambazo tayari mnaziingiza. Ni kiasi cha kuingia kwenye mikataba na kuweza kufanya. Kwa hiyo, sasa hivi sisi kwenye reli tutafaidika na nini? Ajira tu! Ajira za vibarua baada ya zile, hakuna kuchochewa kwa... (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Katibu Mkuu wa Mheshimiwa Waziri wa Viwanda ni Mwalimu wangu wa Economics. Mwaka wa tatu amenifundisha input, output modal. Sekta zote za uchumi, yaani unachukua sekta, njia hii na njia hii, ukiingiza kwenye transport unapata nini kwenye manufacturing? Unapata nini kwenye kilimo? Unapata nini kwenye nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sitaki kumwambia Profesa Mkenda kwamba nimrudishie degree yake. Kwa sababu yeye ndio Katibu Mkuu responsible wa hii Wizara; yeye pamoja na mwenzake Dkt. Meru. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo ni mambo ambayo yanapaswa kutengenezewa mkakati, tusipoteze fedha. Kwa sababu ni fedha zetu! Tena tunasema tunajenga kwa fedha za ndani, lakini fedha za ndani zitaenda kutengeneza reli India au China au Uturuki, ziletwe hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwaambia hapa wakati nachangia mchango wa Wizara ya Uchukuzi. Kumbukeni bomba la gesi, kila kitu ambacho kimejenga bomba la gesi kimetoka China. Nothing ambacho kimetoka hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba Wizara wakae upya waangalie, fungamanisho ndiyo solution. Tutaweza kupiga hatua kubwa na kuchochea maendeleo makubwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunatumia fedha za miradi yetu kwa ajili ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwa leo ni hayo tu. Usia wangu ni huo tu, sina mengine ambayo nataka kuyachangia.