Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Silvestry Fransis Koka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa utendaji usiochelewa. Nasema hivyo kwa sababu tulisimama hapa na tukasema tunahitaji Rais na Serikali ambayo inafanya maamuzi hata kama ndani yake kutakuwa na makosa madogo madogo, naye anafanya hivyo na nina imani tutakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri aikumbuke Kibaha. Tunalo eneo lapata hekta 1,500 lililotengwa kwa ajili ya viwanda na yeye kama alivyo imara kutoa viwanda basi namuomba atoe viwanda hadi eneo hili liweze kukamilika na namuunga mkono kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, malengo ya Tanzania ya Viwanda ni jambo linalowezekana na nia nzuri ya Serikali iliyonayo inawezekana endapo kwa uhakika tutakwenda kuondoa kero na matatizo mbalimbali ambayo yanaturudisha nyuma kwenda kufanikiwa katika azma hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na azma hii tunaiomba Serikali iendelee kutengeneza mazingira bora na rafiki zaidi na wawekezaji na wafanyabiashara. Tunaiomba Serikali iondoe kero mbalimbali ikiwa ni pamoja na tozo za aina moja ambazo sasa zinatozwa na taasisi ambazo ni za usimamizi (Regulatory Authority) utakuta taasisi mbili au tatu zinatoa tozo ambazo zinafanana kwa wafanyabiashara. Hili ni tatizo na ni kikwazo katika uanzishwaji wa viwanda na uendeshaji wa biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna kero nyingine kubwa ambapo viwanda vyetu vya ndani vinapozalisha vinashindwa hasa kushindana na mali zinazotoka nje ya nchi. Hii ni kwa sababu baadhi ya malighafi na utaratibu mzima wa mchakato wa uzalishaji katika viwanda vya ndani vinatozwa kodi, ikiwa ni pamoja na kodi ya VAT. Hii inafanya mali zinazozalishwa na viwanda vya ndani zishindwe kushindana na mali kama hizo zinazotoka nje kwa sababu wao katika uzalishaji hawalipi kodi hizo. Hili ni tatizo kubwa na ningeomba sasa Serikali kupitia Wizara yake ilitazame na kulifanyia kazi ili tuweze kushamirisha nia na madhumuni ya viwanda Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu ni wajibu wa Serikali kulea wafanyabiashara na viwanda, kwa sababu kimsingi Serikali inamiliki asilimia 30 ya makampuni na biashara zote zilizopo ndani ya nchi. Ndiyo maana siku ya mwisho biashara zote zinawajibika kulipa asilimia 30 ya faida inayopatikana na shughuli nzima ya uzalishaji au ya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni wajibu wa Serikali kulea, kutunza na kusaidia ili siku ya mwisho iweze kufaidika na kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Vivyo hivyo, kwa wafanyabiashara na wazalishaji wanatakiwa wawajibike kwa Serikali na wananchi kwa kutimiza taratibu zote kwa mujibu wa sheria zinazowahusu ikiwa ni ulipaji wa kodi na mengineyo ili kila mmoja aweze kufanya linalofaa na tuwe tunapata win win situation; kwa maana hakika mtu ambaye ana aslimia 30 kama na yeye hutamtimizia haki ni wazi kwamba biashara haitaweza kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu ameonesha nia ya dhati ya kuwasaidia Watanzania, wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania. Katika mkutano wa Tanzania Business Council uliokaa tarehe 6 mwezi huu, Mheshimiwa Rais alitamka wazi kwamba yupo tayari kuendelea kuwasaidia wawekezaji kwa kuwapa incentives mbalimbali ikiwa ni pamoja na tax holiday ilimradi uwekezaji huo unalenga kunufaisha na kuisaidia nchi, Serikali pamoja na wananchi kwa ujumla wake. Kwa hiyo, ni wazi kwamba nafasi ipo kazi ni kwetu sisi wawekezaji na wafanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu hili ameliweka wazi na amewaagiza watendaji waende wakalitekeleze. Rai yangu kwa wawekezaji, tusilale, rai yangu kwa wafanyabiashara, tusilale. Hatuna sababu ya kuendelea kupata vikwazo kwa sababu Rais amekwisha tamka wazi na yupo tayari kufanya maamuzi yoyote ili lengo na madhumuni ya kuwaunga mkono wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na hata wa nje likamilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nichukue nafasi hii kutaka mamlaka zote husika ikiwa ni pamoja na Wizara mbalimbali ziweze sasa kushirikiana na kuhakikisha kwamba azma hii inakwenda kukamilika na tunasonga mbele katika kuimarisha viwanda na vile vile biashara na hatimaye uchumi na maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi sana nizungumzie madeni kwa kuwa kimsingi yanahusika moja kwa moja na biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu mzigo mkubwa wa madeni ya nje na madeni ya ndani ambao Serikali inao, lakini naiomba sana Serikali katika utaratibu wake, ijikite sasa kupunguza mzigo wa madeni ya ndani. Lengo ni lile lile, madeni ya ndani yatakavyolipwa wafanyabiashara na wawekezaji wataendelea kuwekeza na matokeo yake manufaa yale yatakuwa ni kwa ajili ya Serikali na wananchi kwa ujumla wake, ina maana Serikali itaendelea kukusanya kodi kutokana na ile pesa kuingia kwenye mzunguko. Athari ya kupungua kwa ajira itaondoka, maana yake ajira zitaongezeka na hatimaye Serikali itafaidika zaidi pamoja na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Serikali itapata fursa ya kutumia mitaji ya wafanyabiashara na wawekezaji katika kutekeleza malengo na mambo mbalimbali ya maendeleo. Pamoja na hilo uwekezaji wa ndani utaweza vile vile kuvutia zaidi uwekezaji wa nje ambao tunauhitaji ili kwenda kuimarisha uchumi wetu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulipwa kwa madeni ya ndani kutaisaidia Serikali kupata huduma na bidhaa kwa bei nafuu, kwa sababu kunapokuwa na tendency ya Serikali kuchelewa kulipa huduma na bidhaa zinazotokana na wafanyabiashara na za uzalishaji wa viwandani, maana yake ni kwamba kinachofuata huduma zile Serikali itaendelea kuzipata kwa bei ya juu na huku wafanyabiashara wakihofia kwamba ukifanya biashara na Serikali, basi fedha zako zitakaa muda mrefu na ikiwa umezikopa matokeo yake utapata matatizo makubwa. Kwa hiyo, matokeo yake ni kwamba bei zitakuwa ni kubwa na hatimaye hatutafikia malengo ya kubana matumizi na kwenda sambamba katika utoaji wa huduma katika serikali yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli kwamba tutasaidia wafanyabiashara wetu, maana wengi tayari wapo kwenye matatizo makubwa na mabenki. Wengine wanafilisiwa na wengine wanapoteza mali zao. Kwa hiyo kwa kuanza kuwalipa wafanyabiashara wa ndani ni wazi kwamba tutachangamsha uchumi na hatimaye wananchi watafurahia na tutasonga mbele kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, madeni ya ndani yakilipwa itawasaidia vile vile Watanzania wengi ambao wanadaiwa kodi waweze kuzilipa kwa wakati na hatimaye siku ya mwisho itakuwa ni win win situation kati ya wafanyabiashara, wawekezaji na Serikali na kimsingi fedha nyingi zitatumika katika kuwekeza na hatimaye tutafikia malengo ya viwanda, ajira na ustawi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na haya machache ya kuishauri Serikali yangu, inaunga mkono hoja asilimia mia moja.