Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Prof. Joyce Lazaro Ndalichako

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama tena mbele yako ili niweze kutoa ufafanuzi wa hoja ambayo niliiwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu tarehe 13 Mei, 2016.

Mheshimiwa Mwenyekito, Waheshimiwa Wabunge wametoa hoja mbalimbali, wakati wakijadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka 2016/ 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru kwa dhati Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba na wajumbe wake kwa kuchambua na kujadili kwa kina bajeti ya Wizara yangu. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Hussein Bashe kwa kuwasilisha vyema Maoni ya Kamati hapa mbele ya Bunge lako Tukufu. Niseme kwamba Wizara yangu imepokea maoni na ushauri ambao umetolewa na Kamati yangu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na tutaufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumshukuru Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani na Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani, na niseme kwamba ushauri ambao wameutoa utazingatiwa na Wizara yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuchukua fursa hii, kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa maoni mazuri na kwa michango yao ambayo wameitoa katika sekta ya elimu lakini pia ambayo waliitoa wakati wakijadili hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo jumla ya Wabunge 85 walichangia kuhusu sekta ya elimu. Katika hoja hii ambayo nimeiwasilisha tarehe 13 Mei; jumla ya Wabunge 53 walichangia hoja kwa kuongea na Waheshimwa Wabunge 57 walichangia kwa maandishi. Ninawashukuru sana Waheshimiwa wote kwa michango yao mizuri ambayo hakika itachangia kuimarisha sekta ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mjadala ulikuwa umeletwa kwa hisia na umekuwa ni mjadala ambao umeibua mambo mengi, lakini niseme tu kwamba Wizara yangu inapenda kulihakikishia kabisa Bunge lako Tukufu kwamba ushauri wote ambao umetolewa na Waheshimiwa Wabunge ambao unalenga kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata elimu iliyo bora inayoendana na mahitaji ya sasa, Serikali itauchukulia ushauri wao kwa uzito wa hali ya juu na itafanyia kazi mapendekezo yote na maoni ambayo Waheshimiwa Wabunge wametoa wakiwa na lengo la kuhakikisha kwamba azma ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda inaweza kutekelezwa; na wakitambua kwamba elimu ndio nguzo pekee ya kutufikisha hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imejipanga kutoa ufafanuzi wa hoja zilizotolewa na kwa kweli kutokana na umuhimu na michango mizuri ya Waheshimiwa Wabunge ningetamani kila ambaye alisimama hapa kuongea au aliyechangia kwa maandishi niweze kumpa fafanuzi. Hata hivyo kutokana na muda nilio nao sitaweza kutoa fafanuzi wa hoja zote. Naomba Waheshimiwa Wabunge mkubali kwamba nitatoa fafanuzi kwa yale ambayo nitaweza kujaliwa kulingana na muda, lakini ninawahakikishia kwamba hoja zenu zote ambazo mmezitoa nitawapa ufafanuzi kwa maandishi na nitaziwasilisha kwenu kabla hatujamaliza kikao hiki cha Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo sasa naomba kujibu hoja za Waheshimiwa na kwa sababu ya muda na kwa sababu pia siwezi kuwataja Waheshimiwa wote basi nitataja tu hoja bila kueleza nani ameisema, lakini nitakapotoa katika maandishi nitawatambua wote ambao wamezitoa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala la elimu maalum. Suala la elimu maalum limezungumzwa kwa hisia kali sana kuhusu changamoto ambazo watoto wetu wa Kitanzania ambao wana mahitaji maalum wamekuwa wakizipata katika jitihada zao za kupata haki yao ya msingi ya elimu. Kwa kweli mambo mengi yamezungumzwa kuhusiana na mazingira ambayo si rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, kuhusiana na vifaa vyao vya kujifunzia na changamoto nyingine ambazo wanazipata ambapo wengine wanalazimika kukaa shuleni hata hawaendi likizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba kama kuna kitu ambacho Wizara yangu inaipa kipaumbele ni hawa watoto wenye mahitaji maalum. Kwa kweli wakati hoja hizo zilipokuwa zinawasilishwa ziligusa sana hisia yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itoshe tu kusema kwamba suala la watoto wenye mahitaji maalum ni kipaumbele katika Serikali ya Awamu ya Tano, na niseme kwamba kwa kuzingatia uzito wa hoja ambazo zimetolewa hata katika vitabu kama kuna mambo ambayo tunaweza tukayafanya tutajitazama upya hata kama ni kufanya re-allocation lakini kwa kweli tutahakikisha kwamba tunaweka kasi ya nguvu ya kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ambazo zinawakabili wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Kwa hiyo, niseme kwamba yote mliyoyazungumza kuhusu wanafunzi wenye mahitaji maalum Waheshimiwa Wabunge nimeyapokea na ninawaahidi kwa moyo mkunjufu nitayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limezungumzwa na ninaona katika michango ya maandishi Waheshimiwa Wabunge wengi wamelizungumza ni kuhusiana na suala la ukarabati wa shule kongwe. Kumekuwa na michango mingi ambayo wanaiuliza kwamba mbona hapa hakuna na mpaka nimeulizwa kwamba Waziri hukumbuki ulikotoka, hata shule yako ya Tabora Girls haipo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ufafanuzi kwamba shule hizi kongwe zinakarabatiwa zote, na tulizo hesabu kwa vigezo ambavyo tulitumia ni zile shule ambazo zimeanza miaka ya zamani miaka ya 60 kwenda mbele, yaani kati ya 60 na 70 ambazo zilikuwa ni shule za Kitaifa. Tunazifahamu shule kama Malangali, Ungwe, Tabora Girls, Tabora Boys, Kwiro kwa hiyo niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba zote zitakarabatiwa; na kuna mpango wa ukarabati ambao nimewasilisha karatasi kwenu ukionyesha kila shule iko katika mpango gani. Shule ya Tabora Girls, Tabora Boys zipo katika awamu ya kwanza na zinafadhiliwa na TEA kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge muondoe wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limeulizwa sana hasa katika michango ya maandishi, ni kuhusu vigezo vya kuanzisha kidato cha tano. Waheshimiwa Wabunge ni kwamba Wizara yangu itagawa kwa sababu ya muda mwongozo ambao mnapaswa kuzingatia katika kuanzisha kidato cha tano. Naahidi kwamba mpaka wiki ijayo nitawapa muongozo kwa utaratibu ambao mnatakiwa muufuate. Hata hivyo Waheshimiwa Wabunge ningependa kuwaambia kwamba shule zote za A-Level ni shule za kitaifa. Ipo dhana kwamba ukibadilisha shule ikawa ya A-Level basi watakaochaguliwa watakuwa ni wale ambao wanatoka katika jumuiya yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu iko tayari na itafurahi kupokea maombi na itayafanyia kazi. Hata hivyo tutambue kwamba tunapozibadilisha kuwa shule za A-Level zinakuwa ni shule za kitaifa. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge sina haja ya kuusoma muongozo hapa kwa sababu ya muda lakini ninawahakikishia kwamba wote nitawagawia ili muweze kuufahamu na muweze kutekeleza jukumu lenu la msingi la kuhakikisha kwamba mnapeleka elimu si tu elimu ya sekondari ya chini lakini hata na A-Level ziweze kuwa nyingi katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limezungumziwa na wachangiaji wengi ni suala la ukaguzi wa shule. Wachangiaji wameonyesha kutoridhishwa, kutofurahishwa na mazingira ya ukaguzi shule ambayo yako katika maeneo yetu. Waheshimiwa Wabunge na mimi nikiri kwamba kweli Idara yetu ya Ukaguzi inakabiliwa na changamoto, na ndiyo maana katika bajeti hii Wizara yangu imetenga fedha hata za kuwawezesha kupata ofisi, kwa sababu wengi wanakaa katika sehemu za kupanga, na sote tunafahamu mambo ya kupanga yana adha yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Wizara yangu itaendelea kuimaridha mazingira ya wakaguzi wa shule kwa kutambua kwamba wathibiti wa ubora wa shule, wana mchango wa pekee, wao ndilo jicho letu la kutuambia kitu gani kitaendelea katika sekta ya elimu. Kama Wizara lazima tutahakikisha kwamba tunawapa vitendea kazi, tunawapa mazingira mazuri ya kufanyia kazi ili waweze kutuangalizia vizuri elimu yetu katika ngazi zote kwa sababu wao wako katika sehemu zote kuanzia huko kwenye vijiji mpaka kwenye ngazi ya Taifa; wanaweza wakaona kwa urahisi kama tutawezesha vizuri. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge napokea ushauri wenu na Serikali itaendelea kufanyia kazi suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo limechangiwa na Waheshimiwa Wabunge ni kuhusiana na suala la makato ya asilimia 15 kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu. Niseme kwamba suala hili kuna kesi ambayo imefunguliwa mahakamani miscellaneous case course namba 6/2017, kwa hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 64(1)(c) cha kanuni za kudumu za Bunge sitaweza kutolea ufafanuzi suala hili kwa sababu kifungu hiki kinazuia kujadili mambo ambayo yako mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie hoja na mapendekezo ambayo yametolewa na yamekuwa yakitolewa pia hata na Kamati yetu ya kuweza kupitia na kuangalia upya mfumo wetu wa elimu kwa lengo la kuweka misingi imara ili Taifa liweze kupata kasi ya maendeleo hasa sasa hivi ambapo tunatekeleza sera ya viwanda katika awamu hii ya tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba Serikali imekuwa ikifanya mapitio ya mfumo wake wa elimu na itaendelea kufanya mapitio ya mfumo wake wa elimu. Hata hivyo kwa kuzingatia kwamba suala hili limekuwa likijitokeza mara kwa mara mimi ninaomba kwa dhati kabisa, kama kuna maeneo, kama kuna hadidu za rejea ambazo inaonekana ni vema Serikali ikazingatia inapokuwa inafanya mapitio, Wizara yangu iko tayari kupokea. Kama nilivyosema tutaendelea kufanya mapitio kwa sababu lengo letu ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata elimu iliyo bora. Kwa hiyo, maoni yoyote, ushauri wowote ambao unalenga kumpatia mtoto wa Kitanzania elimu iliyo bora Wizara yangu itaupokea kwa mikono miwili kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumziwa pia suala la uhaba wa wahadhili katika vyuo vyetu vya elimu ya juu.

Mimi nikiri kwamba hiyo ni changamoto ambayo ipo na Serikali imekua ikitatua changamoto hiyo kwa kutafuta ufadhili kutoka kwenye nchi mbalimbali kwa sababu kumekuwa na baadhi ya nchi ambazo waekuwa wakitoa scholarship kama vile China, Uingereza, Misri, kuna wanaosoma Ujerumani kupitia DAAD scholarship.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema charity begins at home, katika bajeti hii ambayo Waheshimiwa Wabunge ninaomba sana mnipitishie tumetenga kiasi cha shilingi bilioni nane za kwetu wenyewe kwa ajili ya kuongezea nguvu ambayo wahadhili wetu waliokuwa wakifundisha watoka nje zaidi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge naomba mniunge mkono ili tuendelee kutatua hiyo changamoto ya uhaba wa walimu katika vyuo vyetu vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumziwa suala la hospitali yetu ya kisasa ya Mloganzila. Kwanza nipokee pongezi za dhati ambapo Waheshimiwa Wabunge wengi wamepongeza kwa hospitali ya kisasa na yenye vifaa tiba vya kisasa. Serikali imepokea pongezi zenu na tunawashukuru sana. Waheshiniwa Wabunge niwahakikishie kwamba kama mnavyoona hiyo ni hospitali ya kisasa imejengwa kwa gharama kubwa na dhamira ya Serikali ya kuanzisha hiyo hospitali iko pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Utumishi amenisaidia kutoa ufafanuzi kuhusu ajira za watumishi na Kamati ya Bunge ilisema kwemba nilikuwa nimeahidi nilipokutana nao tarehe 27 Machi, kwamba Serikali itatoa kiasi cha shilingi bilioni tano. Nafurahi kulialifu Bunge lako Tukufu tayari Serikali imekwisha ipatia hospitali ile ya Mloganzila shilingi bilioni tano ili kuiwezesha hospitali hiyo kukamilisha maandalizi muhimu ili tuweze kuifungua rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaamini kwamba ndani ya muda mfupi nitakuja na habari njema na nitawakaribisha Waheshimiwa Wabunge tutakapokuwa tunazindua rasmi huduma katika hospitali hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limeongelewa nalo ntaliongea kwa kifupi kwa sababu ya muda ni suala la wamiliki wa shule binafsi na kwa maoni yangu na kwa michango ambayo imekuwa ikisemwa kama kumekuwa na dhana kama vile sasa wamekuwa ni watu ambao hawakubaliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Waziri mwenye dhamana ya elimu naomba niwatoe wasiwasi na niwahakikishie kabisa kwamba Serikali bado inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na sekta binafsi katika sekta ya elimu. Hivyo basi niombe hata Waswahili wanasema vikombe viwili vikaa pamoja havikosi kugongana. kama kuna mambo ni changamoto za kawaida, mimi sioni kama kuna jambo ambalo mkikaa mkiwa na dhamira, kwa sababu cha kwanza ni dhamira na kukiwa na dhamira hakuna jambo ambalo linashindikana.

Kwa hiyo, naomba sana hizi changamoto ambazo zimezungumzwa nadhani hapa hatuwezi kuzimaliza, lakini niwaambie wamiliki wa shule binafsi tuko pamoja na ninyi na mimi nitaomba tuwe na kikao ili tuweze kukaa kwa pamoja tuangalie kwa kina na tupate ufumbuzi wa moja kwa moja kwa sababu haipendezi kila siku jambo linakuwa linasemwa hilo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kwenye suala ambalo limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge na limezungumzwa kwa hisia kubwa sana; suala la wasichana ambao wanapata ujauzito wanapokuwa shuleni. Nimesimama hapa nikiwa kama mama, kama mzazi na kama Waziri mwenye dhamana ya elimu. Hili suala ukitazama michango ambayo imetolewa ni suala ambalo kwa kweli inabidi tuliangalie vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kwanza inasikitika sana inapoona watoto wa kike wanakatisha ndoto zao za elimu kutokana na sababu yoyote ile ikiwemo ya mimba. Ninafahamu kwamba mimba kabla ya ndoa inaathiri sana hata kisaikolojia kwa sababu unakuwa kama vile hata ukubaliki na kadhalika. Kwa hiyo, kunakuwa na madhara makubwa ambayo yanakuwa yanajitokeza. Pamoja na tatizo kubwa la mimba za utotoni kwa watoto wa shule ambao wanakuwa wanakosa fursa ya kuendelea lakini lipo tatizo pia kubwa la utoro shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ningeomba nitoe takwimu, ukiangalia takwimu za kitabu cha elimu Basic Education Statistics cha mwaka 2016, ambacho nitaomba Waheshimiwa Wabunge wote wapatiwe nakala mapema iwezekanavyo. Takwimu zinatuonesha kwamba katika mwaka 2015 wanafunzi wa kike ambao waliacha shule ya msingi kwa ajili ya ujauzito walikuwa 251, na watoto wa kike walioacha shule kwa sababu ya kupata ujauzito walikuwa 37,658. Ukienda kwa watoto wa kiume walioacha shule kwa utoro ni 44,930.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, tatizo la mimba ni kweli ni tatizo kubwa na linawatesa hata watoto wetu kisaikolojia, lakini naomba niseme kwamba tatizo la utoro ni kubwa zaidi kuliko hata la mimba. Tunapoteza wanafunzi wa kike peke yake 37,658, na hawa ni wa msingi peke yake, ukienda sekondari watoto wa kike walioacha shule kwa utoro walikuwa 26,069 na watoto wa kiume walikuwa 31,209. Ukijumlisha wote wa msingi na wa sekondari jumla yao walioacha shule kwa utoro ilikuwa ni 139,886 na walioacha shule kwa mimba walikuwa 3,637. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, kama ninavyosema Serikali yetu imesaini makubaliano ya kutekeleza mpango wa maendeleo endelevu mwaka 2030 ambapo tunawajibika kuhakikisha watoto wote wa Kitanzania wanaenda shule mpaka sekondari. Kama Waziri mwenye dhamana ninatambua hivyo na ninapoona kwamba unakuwa na wanafunzi 139,000 ambao hawaendi shule kwa sababu ya utoro, Waheshimiwa Wabunge ninaomba sote tuungane kwa kuhakikisha kwamba kwanza tunashughulikia tatizo la utoro shuleni. Kwa sababu tatizo la utoro shuleni ndilo ambalo linapoteza vijana wengi zaidi kuliko hata mimba. Tukianza na tatizo la utoro tutakuwa tumeokoa vijana wengi zaidi.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie suala la wanafunzi ambao wanapata mimba shuleni. Nchi yetu inaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu na bahati nzuri Waheshimiwa Wabunge sisi wenyewe ndio ambao tunatunga sheria. Ninashukuru sana watu ambao wamegusia sheria ambayo Bunge hili lilipitisha mwaka 2016, ambayo ilifanya marekebisho ya Sheria ya Elimu na kuweka kifungu ambacho kinatoa adhabu kwa mtu yoyote ambaye anatoa ujauzito kwa mtoto wa kike akafungwe jela miaka
30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia naomba sambamba na kuzungumzia na mimba shuleni naomba nilifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba zipo sababu nyingine ambazo zinapelekea pia wanafunzi kukosa haki yao ya msingi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, katika Sheria ya Elimu Sura ya 353 (61)(o) kinatoa utaratibu wa kuandaa kanuni za kuainisha vigezo vitakavyotumika kufukuza mwanafunzi shuleni kutokana na masuala mbalimbali. Kanuni ya nne ya elimu ya mwaka 214 inatoa mwogozo kuhusu mambo ambayo yanaweza yakasababisha mwanafunzi akafukuzwa shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niyasome kwa ridhaa yako, kwanza, utovu wa nidhamu wa makusudi unaojirudiarudia na unaohatarisha nidhamu ya wanafunzi shuleni au kuharibu hadhi ya shule kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya pili, kufanya makosa ya jinai kama vile wizi, kuharibu mali za umma na mali za shule; tatu, uasherati; ya nne dawa za kulevya; ya tano kosa lolote jingine ambalo litaenda kinyume na maadili bila kujali kama aliwahi kutumikia kosa hilo au hapana. Nchi yetu imekuwa ikiwajengea vijana malezi ambayo yanazingatia maadili na utamaduni wa kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua feelings ambazo zimeonyeshwa katika hili suala na kama ninavyosema mimi linanigusa moja kwa moja kwa sababu sitakiwi kumwacha mtoto hata mmoja katika sekta ya elimu, awe mtoto wa kike au awe mtoto wa kiume ni jukumu langu kuhakikisha kwamba anapata elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hayo niliyoyaeleza na kwa kuzingatia kwamba pia zipo sababu nyingine ambazo zinasababisha mtu kufukuzwa shule; kutokana na hii sheria mwanafunzi anapobainika anabusiana shuleni anafukuzwa shule, kitendo cha kubusiana tu. Kwa hiyo, ninachotaka kusema kwa nini ninayasema haya yote, niseme nimepokea hoja na hisia za Wabunge wote, lakini kwa kuzingatia haya ambayo ninaelekeza ambayo ninaeleza ninaona pia bado upo umuhimu wa kuliangalia hili jambo kwa mapana yake. Kama tunaangalia basi tuangalie vipengele vyote vinavyosababisha mwanafunzi kufukuzwa shule na kadhalika lakini pia tuzingatie mila na desturi na vitu vingine ambavyo vinatunza kama kielelezo cha maadili ya utu wa Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelizungumza na mimi hili linanitia hasira sana, ni suala la vitabu kuwa na makosa. Mheshimiwa Naibu Waziri wangu ameomba hapa msamaha lakini mimi siwezi kuomba msamaha kwa ajili ya uzembe wa watu, ila nasema nitawawajibisha, siwezi kuomba msamaha kwa ajili ya uzembe wa watu ambao wanalipwa mshahara kwa kodi za Watanzania kufanya kazi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kama nilivyozungumza katika hotuba yangu, nilipokea taarifa kuhusu hivyo vitabu na nikiri kwamba sijapata muda binafsi wa kuviangalia; lakini kile kitabu cha kiingereza darasa la tatu binafsi nilikiangalia, ni aibu nilikiangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwamba kitabu cha darasa la tatu cha kiingereza watu walioandika ni aibu, watu wanaoajiriwa Taasisi ya Elimu kigezo cha chini kabisa cha elimu ili mtu aweze kuwa Mkuza Mitaala ni degree. Hivi mtu ambaye amesoma mpaka akapata degree, na elimu yetu sekondari ni kwa kiingereza, hata kama amepita diploma akaenda mpaka akapata degree kwa kiingereza, kiingereza cha namna ilie, hili jambo haliwezi kukubalika hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba wote tunafahamu makali ya Serikali ya Awamu ya Tano, kama tumethubutu watumishi wasiokuwa na vyeti 9,900 kwa mkupuo wakaondoka, hawa wanaotaka kuhujumu elimu yetu ni nani? Hili ni jambo ambalo Serikali inalichukulia kwa uzito wa hali ya juu sana na kila mmoja ambaye amehusika na kadhia hii kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema tayari kuna kamati ambayo imeundwa na Wizara yangu ya kuchambua; kwa sababu nimesema kwamba binafsi nimeona kitabu kimoja na kama Waziri mwenye dhamana siwezi kufanya maamuzi bila kuwa na taarifa inayochambua vitabu vyote tayari wataalam wapo kazini wanachambua kitabu kimoja baada ya kingine ili tuweze kubaini ukubwa wa tatito hili na hivyo basi Serikali iweze kuchukua hatua stahiki.

Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge katika suala hili la vitabu ni kwamba binafsi naungana na ninyi na hata kama mnaweza mkatusaidia kutuonyesha makosa ambayo ninyi mmeyabaini zaidi, Serikali itafanyia kazi kwa sababu hatuwezi kucheza na elimu yetu na vitabu ndio chanzo cha maarifa kwa watoto wetu hatuwezi ku-afford kama Serikali tukawa na vitabu ambavyo vina makosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona umeshanipigia kengele na nisingependa ukanipigia kengele ya mwisho, lakini labda tu nizumgumzie jambo moja la mwisho kuhusiana na mabweni ya chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala haya yameainishwa na ndugu yangu msemaji kambi ya upinzani kuhusiana na gharama za ujenzi na kwamba hata katika mchango wake wa maandishi amekuwa na wasiwasi kwamba hivi shilingi bilioni 10 zinaweza zikajenga majengo yale yanayoonekana. Niseme kwamba Serikali imetumia force account ambayo ni utaratibu ambao uliidhinishwa na Bunge lenyewe ambao unawezesha vifaa kununuliwa moja kwa moja na kazi ikasimamiwa na wakala au Taasisi ya Serikali.

Majengo yamejengwa na Wakala wa Majengo Tanzania, na niseme kwamba Wizara yangu imelipa kiasi cha shilingi bilioni 10 kwa ajili ya majengo na mimi nilikuwa nategemea kwamba mngetupongeza kwamba tumeweza kujenga mabweni kwa bei ambayo ni ya nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na suala la kwamba hizi fedha hazikupitishwa na Bunge naomba niweke sawa. Ahadi ya kujenga mabweni aliitoa Mheshimiwa Rais wetu tarehe 4/06/2016 alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar essalaam na alipokuwa ametoa hata mkiangalia katika vitabu vyenu vya volume estimates mtaona kwamba katika mwaka huu wa fedha kulikuwa na shilingi bilioni tano, ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya Chuo Kikuu kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa chuo kikuu cha Dar e salaam. Mara baada ya ahadi hiyo hicho kiasi cha shilingi bilioni tano za mwaka wa fedha 2015/2016 zilipelekwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ukiangalia hata katika vitabu utaona kwamba walikuwa wametengewa shilingi bilioni tisa ambapo tayari bilioni tano zilitolewa kwa ajili ya mabweni na bilioni nne nyingine zitakuwa kwa ajili ya ukarabati kwa sababu mwaka wa fedha haujaisha. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niwahakikishie kwamba hakuna kitu ambacho kimekiukwa, na niombe tu kwamba tumpongeze Rais wetu kwa uamuzi mzuri na kweli ametatua tatizo kubwa kwa wanafunzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo ya ufafanuzi wa hoja ambazo nimeweza kuzifafanua kutokana na muda, kama nilivyosema hapo awali naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hoja zenu zote ambazo mmezitoa tutawapa ufafanuzi kwa maandishi kabla hatujaondoka katika kikao hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na baada ya maelezo hayo niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wote tunapoenda sasa kwenye kupitia mafungu ili kupitisha bajeti yangu naomba wote kwa umoja wenu mniunge mkono ili niweze kuendelea kutumikia katika sekta hii ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kutoa hoja.