Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nianze kwa kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wa Elimu kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuhakikisha elimu yetu inakuwa bora na inaweza kwenda mbele.

Ninamshukuru pia Mheshimiwa Rais wetu kwa kuleta elimu bure kwa vitendo na sasa tunaona watoto wote wa Tanzania walioko mijini na vijijini waliokuwa wamekosa nafasi sasa wanaweza kuipata elimu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie point chache ambazo ziliongelewa; kwanza ilikuwa ni kwamba Kamati iliomba Serikai iongeze bajeti ya Wizara ya Elimu hadi kufikia asilimia 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo hili naomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba tulipoanza mwanzo tulianza Wizara ya Afya tukasema ipewe asilimia 15, leo tunasema Wizara ya Elimu ipewe asilimia 10 na tutakuja Wizara ya Kilimo tutasema kutokana na mikataba mbalimbali ipewe asilimia 10. Tukijumlisha hizi asilimia tunapata asilimia 35 ya bajeti nzima inakwenda kwa Wizara tatu tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikatai kwamba tumeingia mikataba hii, lakini niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwamba tuiamini Serikali yetu, dhamira yake ni ya dhati, tunapotoa bajeti cealing tunaangalia vipaumbele vya Serikali yetu kwa pamoja, kila mmoja apate ili tuweze kuhakikisha kwamba tunaweza kufikisha maendeleo katika sekta zote ndani ya jamii yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba bajeti ya Wizara ya Elimu imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, tukichukulia mwaka 2015/2016 bajeti ya sekta ya elimu ilikuwa shilingi bilioni 3870; mwaka 2016/2017 bajeti ya elimu ilipanda na kufika shilingi bilioni 4570 ambayo ni ongezeko la asilimia 22. Kwa hiyo, Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha elimu yetu inapata bajeti ya kutosha na hii inaoneshwa na hizi jitihada ambazo zimekuwa zikiendelea. Tunafahamu umuhimu wa elimu katika maendeleo ya Taifa letu na wananchi wetu kwa ujumla na Serikali yetu ni sikivu, itakuwa inaongeza bajeti ya Wizara ya Elimu pindi uchumi wa Taifa letu unapoimarika na pato la Taifa letu linapokuwa limekaa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili napenda niseme Kamati yetu pia ilipendekeza kwamba iongezwe bajeti katika Bodi ya Mikopo. Naomba kuliambia Bunge lako Tukufu kama nilivyosema mwanzo, azma ya Serikali ni kuhakikisha elimu yetu inakaa vizuri, watoto wetu wanapata elimu tena elimu ambayo ni nzuri, elimu ambayo wananchi wetu wataweza kuifurahia matunda yake. Katika hili naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu kwamba pia katika Bodi ya Mikopo tunafahamu mwaka huu tumeleta bajeti kama ilivyokuwa mwaka jana ya shilingi bilioni 427.55, lakini tusisahau kwamba Bunge letu hili lilipitisha mwaka jana kwamba Wizara yetu ya Elimu pamoja na Wizara ya Fedha tuhakikishe kwamba tunakusanya mikopo ile ambayo walikopeshwa wanafunzi wetu na sasa wapo makazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba kwa mwezi mmoja sasa tuna uwezo wa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 13 na pesa zote hizi zinazokusanywa tukizidisha kwa mwaka mzima ni zaidi ya shilingi bilioni 150. Serikali yetu kwa kujua umuhimu wa elimu, pesa zote hizi tumesema ziwe ni Revolving Fund waendelee kukopeshwa wanafunzi wetu wa elimu ya juu. Kwa hiyo, tutaona kwa mwaka mmoja Serikali yetu imeongeza shilingi bilioni 150 kwa Bodi ya Mikopo. Hiki ni kiwango kikubwa na tunayo imani kuwa wanafunzi wetu watazweza kukopeshwa mikopo hii na wataweza kupata elimu kuendelea kuonesha ithibati ya Serikali yetu katika kufikisha elimu iliyo sahihi na kila mwananchi ambaye ana qualify kupata mikopo hii aweze kupata mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kulisemea jambo moja ambalo limesemwa ni kodi nyingi zilizopo katika sekta ya elimu. Tumewaona wenzetu ambao wana shule binafsi wakilisemea kwa kiwango kikubwa. Napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba, kodi hizi zilipitishwa na Bunge lako Tukufu. Tukiangalia Sheria ya Kodi ya Mapato, imeletwa hapa tumeipitisha na inatambua kabisa kwa wale ambao hawafanyi elimu kama ni biashara wanapewa msamaha wa kodi nyingi ambazo ziko ndani ya sheria hii, lakini kwa mtu ambaye anafanya biashara ya elimu, anatoa huduma sawa, lakini anatengeneza faida, hivi kweli Waheshimiwa Wabunge tunaweza kuliachia hili kwamba tuwasemehe tu, tuangalie vizuri, tulipitisha sheria hii wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapa mfano mmoja, hakuna asiyetambua ada zinazotozwa na International School of Tanganyika, lakini katika shule zilizokuwa zikipata msamaha wa kodi ni shule hii. Hivi ndani ya shule hii, kuna mtoto wa maskini nani anayeweza kusoma katika shule hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufikirie kwa mapana tunahitaji kuongeza bajeti yetu ya Wizara ya Elimu, hapo hapo tunataka tupunguze vyanzo vya mapato. Tuwe makini katika mapendekezo yetu tunayoyaleta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya ninakushukuru kwa kunipatia nafasi kusema haya machache.