Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa mapenzi yake ya kuniwezesha kuiona siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuipongeza Wizara kwa jitihada zake nzuri katika kuiboresha elimu ya Kitanzania, pamoja na juhudi hizo bado kumekuwa na changamoto zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa vyoo vya kutosha na maji mashuleni. Mara nyingi unakuta watoto zaidi ya 70 wanatumia tundu moja la choo, hili halikubaliki na Serikali ihakikishe kuwa shule haipewi kibali kama haina matundu ya vyoo ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la maji mashuleni, shule zisipewe vibali vya kuanza kufanya kazi kama hazina miundombinu ya kuvuna maji. Bado maji ni muhimu sana katika afya ya watoto mashuleni hasa wa kike pale wanapokuwa katika siku zao za hedhi, ambapo wengi wamekuwa wakikosa kwenda shule kwa hofu ya kukosa maji pale anapokuwa shule. Maji hayo bado yanachangia katika utoro wa wanafunzi wa kike katika maeneo ambayo hayana maji. Mara nyingi wasichana hawa wamekuwa wakitumika majumbani kutafuta maji hivyo wamejikuta wanaacha shule ama kukosa masomo baadhi ya shule.

Kuhusu utoro wa watoto wasichana mashuleni, unasababishwa pia na ukosefu wa hedhi salama kwa watoto hawa. Pia kwa sababu katika utoaji wa elimu bure vipo baadhi ya vifaa vinavyotolewa na Serikali bure vikiwemo vitabu, chaki hata pen, ni ombi langu sasa kwa Serikali kuanza kutoa taulo za kike mashuleni ili waweze kujihifadhi wanapokuwa katika siku zao za hedhi. Ni imani yangu kwamba kwa kufanya hivyo kilio cha ukosefu wa wasichana kukosa masomo kitapungua. Mfano mzuri, zipo nchi nyingine za Kiafrika ambazo tayari zimefanya hivyo na kupunguza changamoto hii kwa ukubwa. Nchi hizo ni kama Uganda, Kenya, Nigeria, Zimbabwe na nyinginezo ambazo zimekuwa zikitoa taulo za kike za kutumia zaidi ya mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la ukosefu wa madawati, kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali katika suala zima la ukusanyaji wa madawati kwa ajili ya shule za Serikali, zoezi ambalo limepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya ukosefu wa madawati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na utaratibu wa madawati yanayoharibika kusubiri kupelekwa kwenye karakana ya Wilaya kwa ajili ya matengenezo. Ombi langu kwa Serikali ione umuhimu wa madawati haya kuwa yanatengenezwa na wafungwa ili kuepusha madawati hayo kukaa kwa muda mrefu, saa nyingine hata miezi mingi kabla ya kutengenezwa. Ila kwa wafungwa yangekuwa yanatengenezwa hapo hapo mashuleni kwani mara nyingi uharibifu wake huwa siyo mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.