Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Janet Zebedayo Mbene

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ileje

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya kuchangia hoja hii muhimu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Nashukuru kwa fursa ya kuchangia hotuba. Naipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi wake na maamuzi ya haraka katika kushughulikia changamoto za sekta hii. Ninawapongeza Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako na Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya na Katibu Mkuu na watendaji wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza Maoni ya Kamati na Kambi ya Upinzani na ya Waheshimiwa Wabunge wote waliotoa maoni mazuri yanayoletea kuboresha sekta hii kwa ajili ya kujenga uwezo wa Taifa hili, kumudu weledi na rasilimali watu ya kutosha, ushindani wa soko na kuboresha kiwango cha elimu inayotolewa nchini. Naomba mchango wangu ufanyiwe kazi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupata elimu bora ni msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na kijamii na kiuchumi popote pale duniani. Kwa upande wa Tanzania, naipongeza Serikali ya CCM kwa jitihada zake za mwaka hadi mwaka za kuongeza fursa ya elimu sawa kwa wote na utoaji wa elimu bora ya msingi, sekondari na ngazi ya elimu ya juu, hili ni jambo la msingi ili kufikia malengo makuu ya maendeleo endelevu. Isitoshe, jamii iliyoelimika vizuri ni kiini cha kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali kwa uwiano wa usawa na pia kustawisha utawala bora. Ijapokuwa Tanzania imepata maendeleo makubwa katika kutoa elimu ya msingi, bado kuna upungufu mkubwa katika suala la ubora wa elimu wanayopata watoto. Kukaa shuleni hadi kumaliza darasa la saba pia ni tatizo sugu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunazungumzia elimu ya mtoto wa Kitanzania kama mkakati wa kujenga rasilimali watu yenye uwezo mkubwa wa kushindana katika soko la ajira na kufanya kazi kwa tija, tunaitaka Serikali izingatie yafuatayo na kuyafanyia kazi:-

Moja, malezi ya mtoto miaka ya awali hadi kufikia miaka mitano. Malezi na makuzi ya mtoto yanahusisha pande zote za mambo yanayoweza kumfanya mtoto akue vizuri tangu umri mdogo, ujana hadi utu uzima. Kwa hiyo, masuala ya afya ya mtoto tangu akiwa tumboni, anapozaliwa hadi anapobalehe, utu uzima na uzee, elimu ya mtoto huyu tangu anapozaliwa hadi uzeeni ni muhimu. Ndiyo maana ni vizuri Serikali ikafanya kazi kama kitu kimoja ili kujenga misingi ya kumletea elimu mtoto mwenye afya njema kiakili na kimwili. Maendeleo ya mtoto kupitia ngazi zote hizi ndiyo msingi wa maendeleo mengine yote yanayofuata katika maisha ya mtu huyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kuhusu huduma za awali za mtoto kiafya, vituo vya kulelela watoto na shule za awali ni sehemu muhimu ya maendeleo ya mtoto kiakili. Pia inasaidia wazazi kupata nafasi ya kufanya shughuli nyingine za maendeleo ya familia. Vituo hivi vinawezesha watoto kuchanganyika na wenzao kwenye michezo mbalimbali na mafunzo mepesi yanayojenga uelewa, utambuzi na hata hisia zao juu ya masuala tofauti. Kipindi hiki ni muhimu kwa mtoto, kwani kinamtayarisha kwa shule rasmi na wanapokuwa tayari kwenda shule ukifika umri wa kwenda shule wanakuwa wachangamfu, wanakuwa rafiki zaidi na kujiamini zaidi. Wanakuwa na mahusiano mazuri na wenzao, ujuzi wa lugha na watakuwa na mawasiliano mazuri. Watoto walio tayari kwenda shule wana nafasi kubwa zaidi na kufanya vyema kwenye masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliwahi kueleza Bungeni kuwa mahitaji halisi ya madarasa ya awali ni 16,014 ambayo ni sawa na idadi ya shule za msingi zilizopo nchini kwa sasa. Shule zenye madarasa ya awali ni 14,946 ambazo ni sawa na asilimia 93.33 ya mahitaji. Hivyo, shule za msingi 1,068 hazina madarasa ya awali. Tunapenda kufahamu sasa kama idadi hii imeongezeka?

Takwimu za Serikali zimeainisha idadi ya walimu wa shule za awali kiwilaya. Je, walimu hawa wanasomea kufundisha watoto hawa? Je, idadi yao inatosheleza mahitaji? Kama siyo, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inatoa walimu wa kutosha kwa kila kijiji kuwa na shule ya awali? Naomba Serikali ije na mkakati wa shule za awali kila Wilaya kama ilivyo kwa zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kuwa Serikali itoe motisha kwa sekta binafsi kuhakikisha kuwa kila sehemu ya kazi au kiwanda au shamba kubwa la kibiashara linakuwa na kituo cha kulea watoto na vilevile kuwe na ramani za jinsi vituo hivi vitajengwa ili kuzingatia usalama wa watoto na upatikanaji wa huduma muhimu kwa mtoto, yaani kusoma, kucheza, kula chakula bora, kupumzika na kujisaidia. Hii itawafanya wazazi hata wa vijijini kuwa na imani kwenda kuwaacha watoto kwenye vituo hivi ili wao wakaendelee na shughuli nyingine za maendeleo, watoto wapate fursa ya kujifunza na kucheza na wenzao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu chakula na lishe bora shuleni; ipo haja ya Wizara za Elimu, TAMISEMI, Maji na Fedha kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha huduma zote zinazoainishwa kwenye hotuba hii vinafanikiwa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mpango wa kuwalisha watoto shuleni. Tunafahamu kuwa mpango huu uko katika hatua za awali na tayari baadhi ya shule zimeshaanza kupelekewa chakula kwa ajili ya kuwalisha watoto na kampeni za uhamasishaji kwa familia juu ya umuhimu wa lishe bora kwa watoto shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa shule ambazo chakula kinatolewa, basi kiandaliwe vizuri na kiwe na lishe bora na kiandaliwe katika mazingira yanayoridhisha ili kuwaweka watoto katika hali ya afya njema. Tuna wajasiriamali wengi wanaotenngeneza majiko mazuri yanayofaa kutumika kwenye taasisi mbalimbali wapewe tender za kutengeneza majiko kwa ajili ya shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla watoto wanataka kuona mabadiliko na maboresho kwenye maeneo ya lishe ya mama na mtoto na watoto wote kwa ujumla kwa kuhakikisha kuwa uhakika wa chakula unakuwepo, kuendeleza tabia ya mazoea ya kula chakula chenye lishe bora na kuelimisha watoa huduma kuhusu tabia ya kula chakula chenye lishe bora na kuelimisha watoa huduma kuhusu tabia ya kula chakula chenye virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini na njia bora za kuandaa chakula chenye lishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mapendekezo yafuatayo ili kulinda haki za watoto na kufanikisha eneo la pili miongoni mwa maeneo kumi ya uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushiriki wa Serikali na misaada mbalimbali, Wizara zinazohusika na masuala ya lishe kama vile Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu zitenge rasilimali na fedha za kutosha ili kuboresha lishe shuleni na katika familia. Pia Wizara hizi zihakikishe kuwa sheria husika zinatungwa na taratibu na viwango vinawekwa ili kuhakikisha upatikanaji wa vyakula vilivyosindikwa na vyenye lishe bora vinapatikana na kusambazwa kwa wingi nchini na kuwafikia walaji ili kuwakinga watoto na magonjwa kama yale ya utapiamlo na unyafuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Mheshimiwa Rais akutane pamoja na Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ili kujadili mikakati itakayofanikisha suala zima la kuratibu upatikanaji wa lishe bora katika jamii zetu. Serikali iwajibike kuanzisha programu mahususi za kusaidia familia moja moja kupata uhakika wa chakula na hivyo kufanikisha tabia ya kula chakula chenye lishe bora (kwa mfano kampeni ya nchi ya Rwanda ya kugawa ng’ombe mmoja kwa familia moja ambapo kila familia maskini hupewa ng’ombe mmoja wa maziwa kwa ajili ya lishe bora ya watoto).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuamsha na kuendeleza ufahamu kuhusu lishe bora kwa watoto; watoaji huduma, wazazi na jamii kwa ujumla, inapaswa kuelimishwa kuhusu uhakika wa chakula na masuala ya lishe kwa watoto kama vile njia bora za kutumia rasilimali chache zilizopo, uandaaji na ulaji wa chakula chenye virutubisho vya kutosha na utaratibu mzuri wa kulisha watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee lishe kama sehemu ya huduma ya afya. Zahanati na vituo vya afya viwe vinatoa taarifa na elimu kuhusu lishe bora kwa watoto na wajawazito na hata kwa wanawake wenye watoto wachanga pamoja na kutoa tiba ya kutosha na yenye kukidhi mahitaji ya watoto wachanga wanaosumbuliwa na magonjwa yanayotokana na lishe duni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa wote; iko haja ya kuweka utaratibu au programu za kudhibiti bei za vyakula ili kupunguza uwezekano wa kupandishwa kwa bei hizo kiholela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kupanua wigo wa programu za chakula kwa watoto shuleni kwa kuongeza fedha na rasilimali nyingine husika ili kuongeza idadi ya shule zenye kutoa chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ya usafi na usalama shuleni yako kwenye hali mbaya, ya chini kabisa, tofauti na miongozo iliyotolewa na Wizara ya Elimu na Ufundi, licha ya juhudi za Serikali za kuongeza vyumba vya madarasa pamoja na idadi ya shule za msingi, inaelekea mkazo mdogo sana umewekwa kwenye vyoo. Bado vyoo visafi na vyenye usalama kiafya ni muhimu kwa kujenga mazingira rafiki ya kufaa kwa kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za Serikali Tanzania za elimu ya msingi zinahitaji miundombinu bora na ya kukidhi mahitaji ili kuboresha mazingira na uwiano mzuri wa idadi ya wanafunzi na matundu ya vyoo yaliyopo shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma ya vyoo; shule zilazimike kuweka kipaumbele kukarabati miundombinu na kuboresha usafi wa vyoo na matundu ya vyoo yaliyopo shuleni ili kuepukana na maambukizi ya magonjwa. Pia kuweka mifumo mizuri ya kumudu takataka zinazozalishwa shuleni ili kuepukana na uchafuzi wa mazingira na kufurika kwa vyoo. Ukosefu wa huduma ya maji shuleni mara nyingi husababisha watoto kuwa watoro shuleni na maji machafu husababisha kuenea kwa magonjwa. Kwa hiyo, inapendekezwa kuhakikisha kwamba maji safi na yanayofaa kwa kunywa yanapatikana kwenye shule zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kiwango cha usafi wa mazingira na afya shuleni; shule zote lazima zikaguliwe na kuwajibika kwa lolote lile linalohusika na mazingira machafu na hatarishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina wajibu wa kusaidia shule aidha kwa kutenga fedha au kuzipatia rasilimali nyingine ili kutatua tatizo la mazingira machafu na hatarishi hasa kwa shule za Serikali zilizoko vijijini ambazo zinategemea mgao wa bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule nyingi pia zinakabiliwa na ukosefu wa maji safi na salama ya kunywa pamoja na viwanja vya michezo. Matundu ya vyoo na vyoo, upungufu uliopo ni kwenye kubuni michoro, kujenga na kutunza vyoo vilivyopo shuleni. Tunasisitiza kuwa vyoo vilivyopo havifai na ni vichafu kwa matumizi ya watoto. Isitoshe, kuna upungufu wa vyoo na matundu ya vyoo unaosababisha mistari mirefu ya watoto katika kutumia huduma hiyo na kuwachukulia muda wa kuwa darasani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingi wanazopata watoto ni kutokana na umbali wa vyanzo vya maji kutoka majumbani mwao. Umbali mrefu unaathiri jukumu la kusoma na mara nyingi wanachelewa au kutokwenda kabisa shuleni kutokana na uchovu. Zaidi ya hayo, suala la usalama wakiwa wanaenda kuchota maji kwa kuzingatia kuwa njia ya vichochoro wanavyopitia siyo salama kwa watoto hasa wasichana ambao huwa na hofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uhaba wa maji; kaya na jamii nyingi zina upungufu wa huduma ya maji na zina mfumo mbovu wa usambazaji wa maji kama vile mabomba yaliyovunjika, hivyo hulazimisha kaya kununua maji kwa bei ghali kutoka kwa wachuuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukosefu wa usawa wa jinsia; wasichana mara nyingi wanatumwa kwenda kuchota maji na wanalazimika kutembea masafa marefu kutafuta maji hayo, wakati wavulana wanaruhusiwa kwenda shule. Jukumu hili la kutafuta maji mara nyingi huwaweka wasichana kwenye hatari ya kunyanyaswa na kudhalilishwa kijinsia na hata kubakwa na watu wasiowajua wakati wakiwa njiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza uwekezaji kwenye elimu ya awali kwenye maeneo yafuatayo; moja, makuzi ya awali ya maendeleo kiakili ya watoto. Nashauri wazazi/walezi na Wizara husika kubuni na kutekeleza shughuli mbalimbali zinazowawezesha watoto kukua kimaumbile na kiakili kwa kuanzisha shule za ziada za awali na kuwahusisha watoto kwenye shughuli za kuchangamsha akili, kutambua na kukuza vipaji na kukuza lugha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma ya mama na mtoto baada ya uzazi inahitaji kuboreshwa hasa kwa kupima, kinga na tiba kwa magonjwa sugu ya watoto na kupanua wigo wa huduma ili kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata chanjo na kinga kwa magonjwa mbalimbali. Utengaji wa bajeti ya kuwekeza kwenye miradi na mipango ya malezi na makuzi kwa watoto pamoja na ile inayosimamiwa na Serikali na Taasisi zisizo za Kiserikali ili kuongeza msisitizo na mwonekano Kitaifa na kikanda wa suala hili la makuzi ya watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu ubora wa elimu; ufundishaji shuleni bado si wa kuridhisha nchini kote. Kuna changamoto katika mitaala iliyopo pamoja na mbinu za ufundishaji ambazo hazina mwelekeo mzuri utakaowajenga watoto kupata ujuzi wa kutosha wa kuchambua mambo na kuwa wabunifu na uthubutu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upungufu wa walimu; mgawanyo wa walimu waliopo hauridhishi na husababisha shule nyingine kuwa na upungufu mkubwa zaidi. Isitoshe, pamoja na kwamba walimu wapo, mara nyingi wanakosa motisha na ari ya kufundisha na matokeo yake ni kutokufanya vizuri kwa watoto kwenye masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wenye ulemavu na wasichana hawapati elimu sawa na watoto wengine kutokana na mila na desturi ambazo zinawabagua. Vilevile makundi haya mawili hayathaminiwi na jamii zao ambazo huwapatia wavulana kipaumbele. Hali duni ya miundombinu shuleni/vifaa; shule zilizo nyingi hazipati mgao wa kutosha wa rasilimali na zimejengwa vibaya, hivyo kuyafanya mazingira ya kufundishia na kusoma kuzorotesha ufanisi katika kutoa elimu bora. Pamoja na hayo, shule nyingi hazina vyumba vya madarasa vya kutosha au vifaa vya kutosha kufundishia (karatasi, vitabu na kadhalika).

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu nyingine kubwa inayosababisha mahudhurio hafifu ya watoto shuleni ni umbali mrefu wanaohitajika kutembea kwenda shule. Zaidi ya hayo, njia nyingine wanazopitia ni hatarishi hasa kwa wasichana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla kuna umuhimu wa Serikali kufanya maboresho katika sekta ya elimu kwa kuwa na walimu bora wenye ujuzi na ari ya kufundisha ili kuleta ufanisi. Uwekezaji zaidi uongezwe katika kuboresha elimu iliyotolewa shuleni hasa kwenye shule za Serikali na zile zilizoko vijijini ambazo zimesahaulika kupita kiasi. Mafunzo zaidi kwa walimu yapewe kipaumbele na kuongeza vifaa shuleni kama vile vitabu, karatasi, kwa shule zote na siyo tu zile za watu binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni utoaji elimu bure kwa wote. Mazingira ya shule yaboreshwe ili kuvutia na kuwa toshelezi na rafiki kwa watoto wote ikiwa ni pamoja na wasichana na wale wenye ulemavu ili kukwepa ubaguzi na maendeleo hafifu shuleni.

Kuhusu ukaribu wa shule na huduma ya usafiri; wakati wa kuchagua sehemu za kujenga shule mpya, umbali watakaotembea watoto kwenda shule na ukaribu na shule vizingatiwe. Pamoja na hayo, njia za kwenda shule lazima zichaguliwe vizuri na kuchunguzwa ili kuwalinda watoto dhidi ya watu wenye nia mbaya na hatari kwa maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuzuia mimba za utotoni, fursa ya kupata huduma za afya ya uzazi; juhudi zifanyike kutoa fursa zaidi kuwawezesha wasichana kupata huduma za afya ya uzazi katika maeneo yao wanapoishi na katika vituo vya afya/kliniki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu kuhusu mimba za utotoni shuleni, elimu ya afya ya uzazi isiishie tu katika ngazi ya shule za sekondari bali ipelekwe pia katika shule za msingi na katika Vituo vya Maendeleo ya Jamii ili kuwafikia wasichana ambao wako nje ya shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria na sera kuhusu suala la ngono kwa watoto hazitekelezwi ipasavyo wala kufuatiliwa kwa karibu ndani ya jamii nyingi. Juhudi zaidi zinahitajika kwa vyombo na watu wanaohusika na usimamizi wa sheria kuwajibika kufuatilia kwa makini na kupeleka Mahakamani kesi za kubaka, ngono za kulazimishwa na za kulipia kwa watoto na kuhakikisha wavunjaji wa sheria au wakosaji wanaadhibiwa vikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu wa usafiri wa wanafunzi, shule lazima ziwekeze katika mfumo na utaratibu mzuri wa usafiri kwa watoto badala ya kutegemea usafiri wa umma ambao huwaweka wasichana katika hatari ya kudhalilishwa kijinsia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu watoto waathirika wa mimba za utotoni na elimu; wasichana wanaoacha shule kwa sababu ya ujauzito waruhusiwe kurudi shuleni kumalizia masomo baada ya kujifungua. Shule lazima ziwahamasishe hawa wazazi ili watoto warudi shuleni na kuepuka kuwafukuza kwa kisingizio tu cha hali yao ya ujauzito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukomesha ndoa za Utotoni. Tunaamini kuwa mimba za utotoni ni chanzo kikubwa cha ndoa za utotoni na tunasisitiza na kuhimiza kuelimisha jamii kuhusu hatari na madhara ya matokeo ya mimba za utotoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukatili dhidi ya watoto ni kitendo cha kuvunja haki za binadamu na tatizo la kijamii na kiafya lenye madhara makubwa. Ukatili unaondoa nguvu ya misingi mikubwa ya malezi ya watoto ambayo watoto wanahitaji ili kukua na afya na maisha yenye tija na pia ukatili unakiuka haki za msingi za watoto kupata ulinzi. Matatizo mengi yanayowakumba watoto humu Tanzania ikijumuisha kazi zinazowanyonya watoto, kuwasafirisha watoto kwenda kufanya kazi hatarishi za kuuza miili yao na ukatili wa kijinsia yanaathiri vijana zaidi ya watoto wadogo. Mara nyingi asasi zile zile na hata watu binafsi ambao wanategemewa kuwalinda watoto kama vile walimu, polisi, familia zenyewe zimetajwa kuwa zinahusika kuendeleza ukatili dhidi ya watoto na udhalilishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla watoto wanahitaji ulinzi dhidi ya ukatili na aina nyingine za unyanyasaji. Sheria kuhusu kazi ngumu kwa watoto na adhabu kali za wakosaji ambao wanakiuka na kuwafanyia watoto ukatili yashughulikiwe kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yafuatayo katika kulinda haki ya mtoto na kufanikisha utekelezaji wa eneo la tisa la uwekezaji:-

Moja, Sheria za Ajira ya Watoto na Sera. Serikali za Mitaa na wadau wengine wakuu lazima wawajibike katika kusimamia utekelezaji wa juhudi za kulinda haki za watoto. Serikali za Mitaa pia lazima kuongeza uelewa na kujiimarisha ili kumudu kwa ufanisi kusimamia kazi ya utetezi na ulinzi wa haki za watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi; nashauri Serikali kuandaa mfumo wa ufuatiliaji wa ulinzi wa haki za watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi hasa wale wanaoishi mitaani. Hii itasaidia wanajamiii na viongozi wa Serikali za Mitaa kuchukua hatua za kupima maendeleo yaliyofikiwa katika kukomesha ukatili na udhalilishaji wa watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu makazi ya muda au makazi salama; watoto pia walipendekeza kuanzishwa makazi au vituo vya muda vya kutosha kulelea watoto wanaoishi mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utekelezaji wa sheria; kutokana na ongezeko la ukatili kwa watoto, ajira za watoto na unyonyaji, watoto walipendekeza kusambaza sehemu zote nchini nakala ya Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu watoto wenye ulemavu; nchini Tanzania kama ilivyo katika nchi nyingine zinazoendelea na pamoja na kuwepo kwa sheria nzuri zinazolinda watoto, watoto wenye ulemavu, wanapata taabu sana wanapojaribu kuchukua fursa za kupata huduma mbalimbali kama vile huduma za afya, elimu na huduma nyinginezo wanazopata watoto wengine. Uelewa mdogo kuhusu ulemavu na fikra potofu za jamii kuhusu ulemavu na watu wenye ulemavu ni miongoni mwa vipingamizi ambavyo vinasababisha kupoteza fursa ya kuleta usawa miongoni mwa watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la ulemavu, kimsingi kuna haki ya msingi ya maisha na hali za watoto wenye ulemavu kuboreshwa hasa kwenye sera za shule na miundombinu na kujenga mazingira rafiki shuleni ambayo hayatakuwa tena na ubaguzi wala unyanyapaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu rafiki shuleni pamoja na majengo na madarasa ni muhimu yajengwe kwa kuzingatia kuweka sehemu maalum za kupita, alama maalum, vyoo maalum na aina nyinginezo za ujenzi unaokidhi mahitaji ya watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria na sera zinazowalenga watoto wenye ulemavu lazima zisambazwe kwa watu wengi ili zifahamike na kufuatwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matengo ya Bajeti na rasilimali zaidi lazima zitengwe kwa ajili ya watoto wenye ulemavu ili kufanikisha utetezi na ulinzi wa haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nashauri Serikali iongeze uelewa wa jamii kwani wale wenye ulemavu wa mtindio wa ubongo mara nyingi wanaeleweka vibaya na chanzo cha matatizo yao kubahatishwa tu (kwa mfano kudhaniwa kuwa wamerogwa) na hivyo jamii inahitaji elimu ya ufahamu ili kubainisha, kutofautisha na kuelewa aina mbalimbali za ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu kwa watoto wenye ulemavu shuleni; jamii husika na shule ziwajibike kuhakikisha kuwa watoto wote wenye ulemavu wanaandikishwa shuleni na kushiriki katika ngazi zote muhimu za elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na ninaomba maoni haya yaingizwe kwenye mipango ya Wizara ili kidogo kidogo yaanze kufanyiwa kazi na mpaka mwaka 2020 tutakuwa tumepiga hatua kubwa. Mungu awatie nguvu Waheshimiwa Mawaziri wote wawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.