Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kuwa Taifa lililoelimika ni Taifa bora kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ongezeko la mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari; kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto wa kike kupata mimba na hivyo kusababisha kukatisha masomo yao. Watoto hao wa kike wanapokatiza masomo yao wanakwenda kuwa walezi wa watoto hali ambayo inawafanya waingie kwenye umaskini na wengine kujiingiza kwenye ukahaba ili waweze kumudu kulea watoto wao. Hata hivyo, watoto hawa wanaweza kuingia kwenye hatari ya kupata maambukizi ya VVU na hivyo kuacha familia zao zikiwa na huzuni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, visababishi vingi vya watoto kuingia kwenye kupata ujauzito nitavitaja vichache ikiwemo hali ya umaskini inayowakabili wanafunzi, hivyo, watoto wa kike hudanganyika kwa urahisi, umbali mrefu wa kutoka kwenye makazi yao kuelekea shuleni, shughuli zinazowazunguka watoto hawa wa kike mfano kuchota maji, kuokota kuni na kadhalika. Nashauri Wizara ilete muswada wa kubadilisha Sheria ya Mtoto ili mtoto wa kike akipata mimba aweze kuendelea na masomo ili kuwasaidia watoto hawa. Hii iende sambamba na adhabu kali kwa mtu yeyote anayempa mimba mtoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miundombinu ya elimu, kumekuwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya elimu mfano vyumba vya madarasa, mabweni, matundu ya vyoo ambavyo haviendani na kasi ya ongezeko la idadi ya wanafunzi na miundombinu ya shule au elimu. Darasa moja wanafunzi zaidi ya 60 hii haileti afya ya elimu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uwiano katika wanafunzi na walimu, hili limekuwa ni tatizo kubwa sana hasa shule za Serikali ukilinganisha na shule za binafsi. Naomba Serikali na Wizara ijifunze kutoka shule za binafsi itasaidia kuboresha shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tatizo la walimu wa kufundisha viziwi na walemavu kwa ujumla, kumekuwa na tatizo kubwa la walimu wa walemavu kwenye shule zetu hivyo kupelekea watu hawa kukosa huduma muhimu ya kupata elimu sambamba na shule za ufundi na VETA. Mfano, shule ya Moshi Technical ilikuwa ikipokea walemavu wengi na walisoma pamoja na kupata elimu ya ufundi jambo ambalo limewasaidia sana ambao hawakuweza kuendelea na elimu ya juu wameweza kujitegemea kwa kujiajiri.

Nashauri Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI ili kuona namna ya kuboresha shule ambazo zinatoa mchanganyiko wa elimu ya ufundi na kawaida ili kusaidia vijana wetu vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikopo ya elimu ya juu; suala la wanafunzi waliokopa kurudisha mkopo ni la muhimu sana. Wasiwasi wangu ni namna ya urudishaji wa mikopo kwa wale ambao hawako kwenye mfumo rasmi wa ajira. Naomba Waziri atakapokuja kuhitimisha anipe ufafanuzi wa jinsi gani waliochukuwa mikopo ambao hawako kwenye mfumo rasmi wa ajira watarudisha mikopo hiyo ili kusaidia wahitaji wengine wa mikopo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha ya Kiswalhili kwa kufundishia. Nakubaliana na matumizi ya lugha ya Kiswahili lakini wasiwasi wangu ni kama tunaweza kutumia Kiswahili. Kama hatutaweza kukitumia mpaka elimu ya juu itakuwa ni changamoto kubwa sana. Nasema hivi kwa sababu lugha tunayoitumia kwa elimu ya juu ni Kiingereza hivyo italeta mkanganyiko kwa watoto hasa lugha ya Kiingereza wanapofika elimu ya juu. Nashauri tutumie lugha zote mbili kwa manufaa ya kibiashara na uchumi wa nchi yetu na Afrika Mashariki.