Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kuhusu madai ya mtumishi aitwaye Ndugu Charles Kanyika. Naomba kuleta suala hili kwa maandishi kama ambavyo tayari nimewasilisha kwa Mheshimiwa Waziri. Mtumishi huyu anatarajia kustaafu tarehe 15/06/2017 mpaka sasa hajapelekewa michango yake PSPF kwa miezi 18 suala ambalo litaathiri mafao yake. Nimeambatanisha maelekezo yake baada ya jitihada zake kuomba ufumbuzi wa suala hili kutofanikiwa. Pamoja na kuwa huyu ni mtumishi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, ajira yake toka awali kwa mtiririko wa barua zake, mwajiri ni Wizaraya Elimu, naomba tumsaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikopo ya elimu ya juu, hii dhana ya kwamba mwanafunzi aliyesoma O-level mpaka A-level katika shule zinazoitwa za bei mbaya kwa hiyo hastahili mkopo kwa kigezo kuwa wazazi/walezi wana uwezo wa kulipia sio sahihi. Wapo watoto ambao wamesomeshwa na wafadhili baada ya A-level wafadhili sera zao au uwezo hauwapi nafasi ya kuwalipia elimu ya juu. Naomba wanafunzi wa aina hiyo watizamwe. Katika mchango wangu huu nimeambatanisha maombi kutoka kwa Padri Stephen wa Selesian of Don Bosco ambao watoto waliowafadhili wamekosa mikopo. Naomba ikiwa wana sifa Bodi ione uwezekano wa kuwasaidia. Nimeambatanisha barua pepe ambayo Padri Stephen aliniandikia na barua yangu kwa Waziri ambayo nakala nitaikabidhi Bodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu NACTE vs St. Bakhita. Kumekuwa na mkanganyiko wa namba za usajili ambazo wanafunzi wa St. Bakhita ambacho ni Chuo cha Uuguzi, wamepewa namba mbili tofauti na hawajui ipi ni namba yao ya usajili. Kila wanafunzi wanapohoji wanapokea vitisho kiasi cha hata kupewa supplematary au discontinuation. Naomba NACTE itizame suala hili ili wanafunzi wawe na amani, pia nimemjulisha Mheshimiwa Waziri suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu NACTE kuingiliwa na Serikali kuliko kawaida, kwa mfano, Kurugenzi ya Mafunzo ya Wizara ya Afya ni kama iko juu ya NACTE naona kuna namna ya kudhoofisha NACTE. Nashauri NACTE ipewe nafasi ya kufanya kazi kwa mazingira bora ya ku-regulate vyuo vya kati. Aidha, ijengewe uwezo wa rasilimali watu na nyenzo ili ifanye kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, NACTE ijitazame hasa katika kukagua vyuo, unakuta watoto wanasoma, wanamaliza vyuo, wakienda kwenye ajira ghafla wanaambiwa chuo alichosoma hakijasajiliwa na cha kusikitisha chuo kipo Dar es Salaam. Hili halikubaliki, ni uzembe wa hali ya juu. Pili, tozo mbalimbali wanazolipisha vyuo binafsi zimegeuka mzigo kwa wazazi. Ni kweli lazima kuwepo na tozo hizo ili kuiwezesha NACTE itekeleze majukumu yake ipasavyo lakini ziwe fair and affordable maana kinyume chake ni kuwabebesha mzigo kwa wazazi na walezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndoto ya uchumi wa viwanda bila kuweka nguvu kwenye elimu ya ufundi ni ngumu. Kwa ilivyo sasa Wizara ijikite (it has to take lead) kuhakikisha kuwa tunahuisha elimu ya ufundi katika maana halisi na sio kwenye maneno ya makaratasi. Tunahitaji ma- technician, ma-artisan kuliko hata graduates. Tunazungumzia uchumi wa mafuta na gesi lakini hata focus iko kwenye Post- graduate level (masters) na kuendelea. Nashauri sana, hata hii VETA isiwe bora VETA bali iwe na michepuo kulingana na mazingira na mahitaji ya maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikopo kwa kada za afya ngazi za chini. Naamini kama Taifa kila kada ina umuhimu wake lakini uzito na mahitaji yako tofauti. Nimelisemea hili katika mchango wangu wa Wizara ya Afya. Mahitaji ya kada za afya kuanzia Labaratory Technicians, Wauguzi, Maafisa Afya ni kada ambazo huko vijijini wanafanya kazi kama madaktari na ni tumaini kubwa la wananchi. Hata hivyo, gharama za ada kwa vyuo vya uuguzi ni wastani wa shilingi milioni 3.5 kwa mwaka. Kwa kuwa vyuo vya Serikali havina uwezo mkubwa wa kudahili (kwa takwimu uwezo ni around 5,000 vyuo vyote kati ya maombi 13,000), nashauri Serikali ifikirie uwezekano wa kutoa mikopo kwa kada hizo. Kwa mfano, Peramiho wanamsaidia mwanafunzi kumlipia 50% ya ada na akimaliza anafanya kazi mwaka mmoja huku akikatwa sehemu ya mshahara kufidia mkopo/ile 50% ya ada. Tunaweza kuwa na utaratibu kama huo kusaidia kuongeza idadi ya watumishi wa kada ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maslahi ya walimu, ni kweli kuwa Wizara hii ina deal na sera, lakini imekuwa kama kukwepa majukumu, kila ukimzungumzia mwalimu utaambiwa mara ni suala la TAMISEMI au Utumishi na kadhalika. Mwalimu ni dereva, hata kama gari ni new model, ni Benz, Vogue na kadhalika kama dereva yuko demoralized hasa katika welfare, gari haliwezi kufika. Walimu wamegeuka kama second citizen, Maafisa Utumishi kauli zao kwa walimu wanapofuatilia haki zao ni vitisho mwanzo mwisho. Walimu wakitumika kwenye kazi za mitihani, vitambulisho, kura hawalipwi ipasavyo eti mtu anadanganywa na chai na keki kisha anapewa shilingi 10,000, is totally unfair.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta binafsi ni mdau muhimu katika elimu, kumeanza kujengeka dhana kama private sector ni mshindani wa public sector katika elimu kuanzia utoaji wa miongozo, vitabu na usimamizi. Kwa mfano, public schools zimepewa vitabu lakini private school siyo wapewe bure lakini vipatikane sokoni. Tulihimiza watu wajenge shule na vyuo vikuu, leo hii kauli zetu kama viongozi is like nani aliwaambia muwekeze kwenye elimu. Cha muhimu uwepo usimamizi bora, tuione private sector kama ni partner kwenye suala la elimu na sio washindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Tanzania Institute of Education, wengi wamesema kuhusu suala hili, taasisi hii ama iongezewe nguvu kiutendaji ama kuwepo chombo cha ku- regulate maana as of now ni mchapaji, muidhinishaji na msambazaji jambo ambalo siyo sawa kitaalam. Pia makosa kwenye vitabu yamekithiri na vitabu havifiki kwa wakati, kimsingi wamezidiwa. Nashauri wajengewe uwezo both kitaaluma na nyenzo. Vilevile kama tutarejea kurudisha Bodi ya EMAC na sekta binafsi, tuongeze umakini kwenye usimamizi. Katika uchumi wa soko ni vizuri tujikite kwenye udhibiti kuliko kuhodhi suala la vitabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye matokeo ya darasa la saba Mafinga Mjini pamoja na kuwa ni Halmashauri mpya tumekuwa nafasi ya nne kitaifa. Idara ya Ukaguzi hawana magari wala ofisi na vitendea kazi. Nafahamu jibu litakuwa hili ni suala la TAMISEMI lakini naamini ukaguzi uko Wizara ya Elimu, kwa hiyo, naomba ipatiwe gari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondokana na usumbufu wa michango ya chakula cha mchana, nashauri Halmashauri za mjini kama ilivyo Mafinga Town Council pawepo na utaratibu wa shule za msingi kusoma mpaka saa nane mchana siyo kama ilivyo sasa ambapo ama watoto wanarudia mchana au wazazi wanaombwa michango ya chakula. Kwa hali ilivyo na kwa mjini walimu wanatoka Kitongoji A mpaka B au C, sasa kwenda na kurudi ni gharama. Nashauri mliangalie kitaalam na kitaaluma ikifaa shule za mjini waishie saa nane mchana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi ni moyo wa elimu. Ukaguzi ni kama CAG kwa Serikali lakini level ya uhuru (independent) iko chini. Ukaguzi hii ya sasa inaikagua Serikali na walimu, je, sio muda muafaka sasa kuifanya iwe agency?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukufahamisha kuwa shule ya msingi ya mahitaji maalum Makalala ipo katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga na si katika Halmashauri ya Mufindi kama ilivyo kwenye kitabu Ukurasa wa 272 kuhusu nukta nundu, ukurasa wa 296 kuhusu usambazaji wa vifaa maalum. Hoja yangu, kwa kuitaja Mufindi DC badala ya Mafinga TC ina mkangayiko, hili limejitokeza kwenye maeneo mengi, hivyo kuchelewesha utekelezaji, kwa mfano kiutawala (administratively) vifaa hivyo vikifika Mufindi DC kuwe na taratibu za kuandikiana kwenda Mafinga TC ambako ipo shule ya mahitaji maalum Makalala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi/ushauri, naomba kwenye taarifa zenu muitambue shule ya mahitaji maalumu ya Makalala kwamba ipo kwenye Halmashauri ya Mji wa Mafinga na si Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi. Ninaelewa kwa nini watu wengi wanachanganya, ni kwa sababu awali ilikuwa Halmashauri moja kabla ya kugawanywa Julai, 2017 na kupata Mafinga na Mufindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.