Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kipekee nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima na afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Naunga mkono hoja na nimpongeze sana Mheshimiwa Ndalichako na Naibu wake Mheshimiwa Injinia Manyanya pamoja na timu nzima kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuleta mageuzi katika sekta ya elimu. Bila elimu bora hakuna Taifa bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunatambua elimu ndiyo uti wa mgongo kwa Taifa lolote lile. Nikimnukuu Marehemu Nelson Mandela aliwahi kusema; “Education is the most powerful weapon you can use to change the world” akimaanisha elimu ndiyo silaha kubwa inayoweza kuibadilisha dunia. Kama kweli tunataka kuibadilisha dunia ya Tanzania ni vema sasa tukawekeza zaidi katika elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mimba za utotoni. Suala hili limekwamisha jitihada za watoto wa kike kufikia malengo yao. Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni. Kwa mwaka 2015 kulikuwa na mimba za utotoni 11,513 ambazo zilikuwa chini ya umri wa miaka 20. Miongoni mwa waliobeba mimba hizi walikuwa ni wanafunzi walioacha shule na wale walioolewa, idadi hii ni kubwa sana na inasikitisha, ni lazima tutafute suluhu ya jambo hili ili wanafunzi wa kike waweze kusoma vizuri na kuweza kufikia ndoto zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri Serikali kuja na mkakati au programu au kampeni katika shule zetu ambayo itamsaidia mtoto wa kike kuweza kujitambua, kujiamini, kujithamini utu wake, kuwa na vision na kuweza kufikia malengo. Tunataka mtoto wa kike wa Tanzania hii aweze kujitambua, aweze kujua anataka kwenda wapi na atafikaje huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukajenga hostel nyingi zenye uzio mrefu, lakini bila ya kumtengeneza mtoto wa kike, kumjenga kisaikolojia, kumpa elimu ya kutosha kuweza kujitambua itakuwa ni kazi bure na mimba za utotoni zitaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Serikali iliendesha zoezi la uhakiki wa vyeti vya taaluma kwa watumishi wa umma. Naipongeza Serikali kwa hatua hii kwani itasaidia kupata watumishi wenye sifa zinazostahili, lakini miongoni mwa watumishi waliokumbwa na kadhia hii ni walimu. Ningependa kufahamu ni walimu wangapi wa shule za msingi na sekondari walioathirika na zoezi hili la uhakiki wa vyeti na je, Serikali imechukua hatua gani za kuweza kuziba nafasi zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu ukiangalia shule nyingi nchini zikiwemo za Mkoa wa Singida zina uhaba mkubwa wa watumishi walimu. Kwa Wilaya ya Ikungi tu kuna upungufu wa walimu 348 hao ni walimu wa sayansi na sanaa na kwa Wilaya ya Singida Vijijini katika shule za msingi kuna uhaba wa walimu 754, idadi hii ni kubwa sana ukijumlisha na wale waliotumbuliwa katika zoezi la uhakiki wa vyeti hali hii inakuwa siyo nzuri. Naiomba Serikali yangu iangalie jambo hili kwa ukaribu na ipeleke walimu wa kutosha hasa katika Mkoa wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalimu ndiye mdau mkubwa katika elimu, tukiweza kumtengeneza kisaikolojia na kimaslahi tunaweza tukamuwezesha mwalimu huyu kufikia malengo yake. Kila siku hapa tutakuwa tunaimba elimu yetu imeshuka viwango, ifike wakati sasa walimu wapewe stahiki zao, walimu wawezeshwe kuwa na mazingira bora ya kufundishia kwa maana ya kuwa na nyumba bora za makazi, maslahi bora, miundombinu bora ya kufundishia hapo tutakuwa tumemwezesha mwalimu kuweza kumfundisha mtoto wa Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni maabara, Watanzania walio wengi wamejitolea kwa hali na mali kuhakikisha shule zetu zinapata maabara, maabara nyingi hazina vifaa na hazina miundombinu inayoridhisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru sana Serikali yangu kwa kusambaza vifaa vya maabara mashuleni lakini nielezee masikitiko yangu katika Mkoa wa Singida ni shule 18 tu ndiyo zilizopata mgao wa vifaa vya maabara. Idadi hii ni ndogo sana ukilinganisha na mikoa mingine na kama tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda tutafikaje huko bila ya kuwa na wataalam wa kutosha ambao watakuwa wameandaliwa vizuri katika maabara zetu? Nakuomba sana Mheshimiwa Ndalichako najua wewe ni msikivu, uuangalie kwa kipekee Mkoa wa Singida kwa kupeleka vifaa vya maabara vya kutosha pia vitabu vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni Idara ya Ukaguzi. Serikali imekuwa ikitumia rasilimali nyingi kuboresha elimu hasa katika shule za sekondari. Nadhani ifike wakati sasa tuwekeze nguvu kubwa katika idara zetu za ukaguzi vinginevyo tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu. Ni lazima ukaguzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu upewe msukumo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana.