Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Edwin Mgante Sannda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Kwanza kabisa napenda kuipongeza Wizara chini ya majemedari wetu wawili hawa wana mama kwa kuwasilisha hotuba nzuri kabisa ya bajeti hii ya Wizara ya Elimu. Lakini na mimi nitumie fursa hii fupi nichangie machache, kimsingi nataka nizungumze kwenye upande wa ufundi, leo nitajikita kwenye ufundi tu sitaongelea kitu kingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mipango mizuri, utekelezaji ambao umefanywa huko nyuma lakini nataka nizungumzie ufundi kwa maana ya ufundi wa elimu na mafunzo kwa maana ya ufundi stadi na ufundi sanifu. Hapa tunazungumzia vyuo kama vile DIT, Mbeya Technical, Arusha Technical tunazungumzia pia VETA pamoja na FDC vile Vyuo vya Maendeleo. Huko nyuma tulikuwa navyo kwa maana halisi ya ufundi, lakini baadae tumekuja kutoka kila mmoja anataka awe meneja apate degree, avae tai kama Mheshimiwa Sannda wakati tunahitaji mafundi wakae site tuweze kupata weledi na umahiri katika utekelezaji wetu wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunajikuta tunaishia kwenye kazi zenye ubora wa viwango vya chini kwa sababu ya upungufu na ukosefu wa mafundi kule site, kila mmoja manager lakini technicians na artisans tatizo limekuwa ni kubwa sana. Ningependa sasa nimeona mipango na maelezo mengi ya huko nyuma na mipango kwa ajili ya 2017/2018, lakini ningependa Mheshimiwa Waziri unaporudi baadaye wakati wa kuhitimisha utueleze kidogo kuhusu sera na dhamira ya dhati ya kuhakikisha utekelezaji wa mipango hii na mikakati unakwenda kutekelezwa kwa maana ya kutenga bajeti nzuri ya utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya dhati itakuwepo tu pale ambapo tutawekeza kwenye vyuo hivi vya ufundi, turudishe polytechnics. Sasa tuna Vyuo vingi Vikuu vinatoa degree mbalimbali katika fani mbalimbali, lakini pia hatuwezi kutoka moja kwa moja kila mmoja akawa meneja, tunataka tujenge kundi kubwa la mafundi ambao watakwenda kuwa weledi katika utekelezaji pia watajijengea stadi za maisha za kuweza kujiajiri badala ya kila mmoja kusubiri kwenda kuajiriwa ofisini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijaona dhamira hii ya dhati kabisa katika uwekezaji kwenye hili. Tunahitaji tutenge bajeti yake lazima iakisi kwamba hapa tunataka kwenda kutekeleza hii mipango. Tutaongea mambo mazuri kweli kitabu chako kimeeleza vitu vizuri sana, lakini kwenye bajeti haipo hivyo katika nyanja hii. Kwa hiyo, ninakuomba Mheshimiwa Waziri, Wizara kwa ujumla na timu yako yote, suala la fani na mafunzo ya ufundi sanifu na ufundi stadi siyo kitu tena cha kukisubiri au kukifikiria labda tutakifanya baadae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zama hizi tunataka kwenda kwenye uchumi wa viwanda; uchumi wa viwanda bila hawa watu tutakuwa tuna-import skills nje sana. Tunahitaji watu wetu a ndani ili waweze kwenda na kuiwezesha azma hii ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujikita kwenye uchumi wa viwanda. Jambo langu kubwa ninaloweza kusisitiza tutenge bajeti na tuwe na dhamira ya dhati kabisa ya kuweka bajeti ya kutosha kwa ajili ya elimu na mafunzo ya ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo kama Chuo cha Ardhi kilikuwa chuo mahiri kabisa, watu wanavyokwenda kujifunza kule wanakwenda kujifunza muda mwingi ni mafunzo ya vitendo. Nadharia inakuwepo, lakini sehemu kubwa ya ufundishaji wao na mafunzo yao ni sehemu ya vitendo, kiasi kwamba wanapotoka pale shuleni ni watu ambao wameiva, wamepikwa wakapikika vizuri kabisa wanaweza kuwa tayari, wanasema wengine you hit the ground running ili uendelee na kupambana na maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninapende tu kusisitiza kurudisha na kuweka focus kwenye vyuo kama Chuo cha Ardhi, Mbeya Technical, Arusha Technical na vingine vya namna hiyo. Pia huku nyuma tulikuwa na shule za ufundi, ukitoka form four unaenda kuanza shule za ufundi kama ilivyokuwa Ifunda. Kwa hiyo, unaanza kupikwa kutoka hapo, ukija kwenda kwenye technical colleges huko ni mtu ambaye tayari mzuri kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani tulikuwa tunataniana tunasema wale ma-engineer waliokuwa wanakwenda site wanaajiriwa na makandarasi, waliotoka Chuo Kikuu wamesoma Uhandisi kabisa na wale waliotoka DIT ukiwaweka pamoja huyu wa Chuo Kikuu yeye ni mwepesi, mweupe kabisa. Tunataka watu watakaoenda kufanya kwa vitendo badala ya wengi kuwa na ndiyo tutakapoendeleza vizuri uchumi wetu wa viwanda na kujenga viwanda vingi na vikawa na wataalam wengi wa kuviwezesha vikastahimili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu kubwa kwa siku ya leo katika Wizara yako Mheshimiwa Waziri nilipenda sana niongelee suala la ufundi na sitazungumzia kitu kingine chochote. VETA pamoja na FDC najua ndiyo mmevichukua sasa hivi Vyuo vya Maendeleo basi tuwekeze zaidi huko, tuhakikishe kwamba na kwenyewe tunakuhuisha ili tupunguze hii kelele ya kila mmoja akimaliza siku hizi vijana wana hitaji msaada sana wa kutafutiwa ajira basi kila mmoja anakutumia CV yake ukiona ni degree, waite kwenye usaili utaona kasheshe yake, uivaji haujakaa vizuri, lakini tungekuwa na watu ambao ni wataalam anaweza akatoka ameshajifunza stadi za ufundi na stadi za maisha anaingia mwenyewe anajasiria viwanda. Anaanzisha kazi kelele na tatizo kubwa tulilonalo la ajira litakuwa limepatiwa ufumbuzi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi mimi nafikiri ya kwangu ni hayo na nitakuwa nimetunza muda kweli. Ninakushukuru sana na naunga mkono hoja. Ahsante.