Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Agnes Mathew Marwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nitoe pongezi sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kutoa elimu bure kwa wanafunzi. Imefikia hatua sasa vijijini watoto wengi wanakwenda shuleni, hakuna watoto wanaokaa majumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kipekee nimpongeze Waziri Mheshimiwa Profesa Ndalichako. Kwa kweli mama anafanya kazi nzuri sana, tuko nyuma yake na Mungu amsimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Magufuli ampe Mheshimiwa Profesa Ndalichako pesa ya kutosha ili arekebishe mambo mengi ndani ya elimu ili mambo mengine ambayo yanaleta shida ndogo ndogo yakae sawa. Kwa mfano, elimu ya shule za Serikali, shida siyo kwamba eti wanafunzi hawaelewi au Walimu hawafundishi. Hata kama wewe nyumbani kwako ukiwa una njaa huwezi kufundisha vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi iwaangalie hawa Walimu kwa macho mawili kwa sababu Walimu ndiyo wamemfundisha Rais, wamemtoa Mbunge lakini Walimu wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niongelee suala la kupandishwa madaraja kwa Walimu. Ni muda mrefu sasa Walimu wanalalamikia suala la kupandishwa madaraja na hasa vijijini. Mkoani kwangu Mara Walimu wengi wanalalamika hawajapandishwa madaraja. Namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie sana hili kwa macho mengine kwani hawa Walimu wanapopata motisha wanaweza kufundisha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine Mkoani kwangu Mara, Wilaya ya Rorya, Kijiji cha Kinesi, Tarafa ya Suba, kuna shule moja ya Isango. Hiyo shule ameuziwa sijui ni mtu gani, tangu mwaka 2014. Shule hiyo ilikuwa inasaidia watoto wengi sana na Mkoa wa Mara tuna uhaba wa shule.

Mheshimiwa Waziri hii kesi iko Mahakamani muda mrefu sana, nimwomba sana alisimamie suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Magufuli huko aliko namwomba, yeye ni mtu wa vitendo aangalie suala hili la Shule ya Isango ili irudi mikononi mwa Serikali na wananchi. Wananchi wa Rorya wanaweza wakaiendesha shule ile na wako wadau ambao wako tayari kwa ajili ya kuiendeleza. Sasa hivi imekaa kama gofu wakati Mkoa wa Mara tuna upungufu wa shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la ongezeko la tozo chefuchefu kwa hizi shule za watu binafsi. Nasema tozo chefuchefu kwa shule za watu binafsi kwa sababu, hizi shule zimeongeza na kupandisha kiwango cha elimu, kwa hiyo, tunapowawekea kodi nyingi ina maana kwamba tunataka kuwakwamisha wasiendelee au tunawakomesha wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema tunawakomesha wananchi kwa sababu hizi tozo zinapokwenda kwa hawa wakuu wa shule au wamiliki wa shule anayezilipa ni mwananchi. Yule Mkuu wa Shule unapomwongezea na yeye zile asilimia anaongeza ada kwa mwananchi. Katika mazingira ya kawaida tunawaonea wananchi, hatuwaonei hawa wenye shule. Kwa hiyo, hili suala tuliangalie mara mbili kwa ajili ya kupandisha kiwango cha elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Waziri wangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako, kipekee na-declare interest kwa sababu mimi pia ni mwanafunzi ambaye nimesoma hayo masomo ya QT. Wameongea humu Wabunge wengi lakini hawajaongelea suala hili. Kipekee nimwombe Waziri aangalie vile viwango vya ufaulu vishuke kidogo kwa hawa wanafunzi wanaosoma masomo ya jioni kwa sababu wanapokuwa wanawekewa marks za juu sana na wengi wao ni watu wazima, wanatoka maofisini, wanakuwa wamechoka wanawaza mambo mengine inakuwa ni vigumu kufaulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri washushe kidogo viwango hivi ili watu wengi wapate moyo wa kusoma. Mheshimiwa Waziri naamini hili atalichukua kwa mikono miwili ili hata wale ambao ni vilaza wenzangu na wao wakasome hii elimu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoani Mara tuna upungufu mkubwa sana wa walimu wa shule za msingi na sekondari na hasa vijijini. Wilaya ya Rorya, Tarime, Serengeti, Bunda, Butiama na Musoma Vijijini, nimwombe sana kiongozi wangu atuongezee Walimu ili wale wanafunzi na wao waweze kufundishwa vizuri. Kwa sababu wanakuwa wanafunzi wengi sana lakini unamkuta mwalimu labda mmoja au wawili. Kwa hiyo, kipekee nimuombe Waziri atusaidie kutupatia Walimu Mkoani Mara.