Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii. Nianze kwa kutoa pole sana kwa wananchi wangu wa Jimbo la Ukonga kwa mafuriko ambayo yametokea kwenye kata za Msongola, Chanika, Zingizingiwa, Gongo la Mboto, Pugu, Buyuni na Majohe ikiwepo na Kivule. Hali ya usafiri ni mbaya sana lakini wavumilie kwa sababu tumeshachukua hatua kwamba baada ya mvua hizi tutafanya ukarabati ili barabara zirudi katika hali yake ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nitoe pole kwa kufariki Mchumi wa Manispaa ya Ilala ambaye alikuwa pia Katibu wa Mfuko wa Jimbo la Ukonga. Nampa pole sana Mheshimiwa Mkurugenzi na watumishi wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala akiwepo Mstahiki Meya tupo pamoja nao na tunamtakia Mungu ampe pumziko la amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mwalimu wa masomo ya hesabu na chemistry na leo nimekusudia kuchangia kitaaluma zaidi. Ningeanza kwa kusema huwa napata shida sana, yako mambo Waheshimiwa Wabunge wanachangia humu ndani, wanazungumzia habari ya elimu lakini inabidi urudi kule kwenye TAMISEMI. Kwa nini Wizara isingeitwa Wizara ya Elimu na mambo yote yanaendana na elimu ili tumuulize yeye, ingekuwa ni rahisi sana. Kama tunazungumza habari ya shule, miundombinu, mahitaji maalum iwe yeye Waziri wa Elimu ndiyo unahusika. Kwa sababu tunazungumza habari ya matundu ya vyoo mpaka tukamuulize TAMISEMI, kwa hiyo, kidogo inaleta shida naomba mliangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hoja ya madai ya walimu. Mheshimiwa Waziri kama ana nia ya kutaka kufanya kazi ambapo mimi sina shaka na uwezo wake, yeye siyo mwanasiasa labda aanze kujingiza kwenye siasa ambayo kimsingi siyo fani yake. Kama anataka kufanya kazi vizuri hebu achukue kitabu cha Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani, achukue kitabu cha Maoni ya Kamati ajifungie avipitie atamaliza matatizo yaliyopo hapa. Wala ahitaji kuzunguka sana humu, achukue Maoni Kambi Rasmi ya Upinzani na Maoni ya Kamati akiyafanyia kazi mwaka ujao ataonekana Waziri bora kabisa wa Elimu katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa walimu wanadai shilingi trilioni 1.6 mpaka sasa wamelipwa asilimia mbili tu. Kwa hiyo, unapozungumzia kuboresha elimu lazima uzungumze kuondoa kesho na malalamiko ya walimu katika nchi hii. Kwa kweli imekuwa ni fedhea sana, ni kwa nini wataalam wa kada zingine hawalalamiki sana. Ukienda kwa madaktari wanalipwa, wanasheria wako vizuri sana, kwa nini kuna shida sana kwa walimu? Kwa hiyo, nadhani hili jambo kwa kweli ingefika mahali mkalimaliza mtamaliza shida ya walimu na walimu watafundisha vizuri kwa kupata stahiki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wamesahihisha mtihani wa form two tangu mwaka jana mpaka leo hawajalipwa. Kuna walimu wameenda likizo, madaraja wanalalamika sana tumekutana nao Mheshimiwa Waziri na hivi vitu ni vitu genuine. Kwa hiyo, ni muhimu mkayafanyia kazi, akija kwa Waziri anarudishwa TAMISEMI, TAMISEMI inaenda kwa Mkurugenzi. Wakati mwingine mwalimu anadai madai yake anafunga safari kutoka sehemu ya mbali anakuja Halmashauri anaambiwa faili limepotea na huyu ni mtumishi wa umma. Nadhani mngepunguza kero kwa walimu hawa mgetusaidia sana sisi ili mambo shule yaende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna hoja hapa ya Bodi ya Mikopo. Nilikuwa nataka niseme lakini yupo Mheshimiwa Ester Mmasi, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi mna shida, ilipokuja hoja hapa ya Bodi ya Mikopo, Waziri mlipambana na Mheshimiwa Mwenyekiti ulikalia Kiti mkatupa maoni yetu kabisa. Wanafunzi hao ambao wengine wanasoma na wengine wanaendelea kufanya kazi wanatakiwa kulipa fedha ya mikopo walikubaliana na Serikali kulipa asilimia nane, imetungwa sheria hapa ambayo inafanya kazi kisengere nyuma wanakatwa asilimia 15 na wameshaanza kukatwa wanalalamika. Kuna mwalimu ambaye anakatwa mpaka mwisho wa mwezi anaondoka nyumbani na shilingi 80,000 au shilingi 100,000 sasa unamfanyeje? Hakuna usafiri, nyumba za walimu, inabidi akodi wakati mwingine bodaboda au taxi aende shuleni. Kwa hiyo, ninyi mmetengeneza mazingira magumu sana kwa kuwahukumu walimu ambao humu Bungeni hawamo na tulipinga mkapitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya bure, juzi Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI alisema kwamba mpango huu ni nzuri, hatukatai mpango ni mzuri, kweli idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza wameongezeka sana. Sasa shida inakuja nataka mnisaidie, kuna shule moja ya kule Dar es Salaam katika mtihani wa form four waliopata division one walikuwa zero, division two walikuwa watano, division three walikuwa 17, division four walikuwa 70 na division zero walikuwa 105. Kwa hiyo, asilimia 11 ndiyo ilipata daraja la kwanza na la pili, asilimia 88.8 walipata zero na four. Sasa naomba mnijibu, hawa division four na zero wako wapi? Wameenda shuleni miaka minne badala ya kwenda kupata uelewa, wameenda kukua kimwili, wako wapi hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule ya pili, division one hakuna, division two wanne, division three wapo 11, division four ni 69 na zero 35. Wanafunzi 15 ndiyo waliopata daraja la kwanza na la pili na daraja la tatu na la nne 104, hawa wako wapi? Shule nyingine division one wapo wawili, division two wapo wawili, division three wapo 18, division four wapo 57, division zero wapo zero 97, wanafunzi154 ni four na zero hawa wako wapi? Ukifanya utafiti taarifa hii inasema asilimia 88 wamepata division zero na division four. Mtusaidie hawa Watanzania walio wengi wameenda wapi. Kwa hiyo hoja inazungumzwa ni kweli kwamba watu wameongezeka lakini kimsingi ubora wa elimu ambayo wanaipata siyo sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii elimu ya bure, mimi sijui kiswahili labda kwa sababu ni Mkurya, Waziri wa TAMISEMI juzi kasema walichofanya Serikali ni kuleta elimu ya msingi bila malipo. Hivi elimu ya bure na elimu bila malipo kuna tofauti gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitendo hicho kimekwaza wazazi wengi sana, wamekubali hawachangii chochote lakini mashuleni kuna tuition zinaendelea, kuna remidial classes na kuna mitihani inafanywa. Kwa hiyo, kuna ubaguzi, wale wazazi wanaoweza kuchangia wanachangia wale ambao ni wenzangu na mimi watoto wao hawasomi. Kwa hiyo, tayari mashuleni kuna matabaka. Ni muhimu mkaja na mpango, kama wazazi wanatakiwa kuchangia msizungukezunguke kutafuta lugha ya kudanganya. Waambieni Serikali imeondoa ada, michango mingine ni
halali, mshiriki kuboresha elimu ili watoto wasome vizuri kwa standard ambayo inaeleweka. Mtakuwa mmetibu tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu heshima ya walimu, kumekuwa na tabia, sasa hivi kidogo imetulia tuliisemea sana kwenye Kamati ya TAMISEMI, kitendo cha walimu matokeo yakiwa mabaya wanawajibishwa wao. Kitendo hicho kimewakwaza walimu sana tungependa waheshimiwe kama wataalam wengine. Kama kuna makosa wapelekwe kwenye vyombo vinavyohusika ili wachukuliwe hatua ambazo zinazotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtihani wa darasa la saba. Maswali ambayo yanatungwa katika mtihani wa darasa la saba ni ya kuchagua. Nimewauliza walimu kwa nini matokeo ni mabaya, wanasema Serikali imeleta asilimia 20 ya pass wakati wa Kikwete, kwa Magufuli wamesema ni asilimia 30, watoto hawa wanapewa maswali ya kuchagua, ana ana doo. Ndiyo maana shuleni kweli kuna watoto ambao ni form two hawajui kusoma na kuandika kwa sababu ameandika jibu ni “A” lakini ukimuuliza “A” umeipataje hawezi kukueleza.

Kwa hiyo, walimu wanalalamika wanasema maswali yasiwe ya kuchagua, wapewe maswali ya kuandika, watoto wapimwe uwezo, yule ambaye anaenda sekondari aende ambaye haendi mpeleke VETA wasipoteze gharama na muda. Katika jambo hili Mheshimiwa Waziri naomba isifanyike siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nizungumze hapa ni kwamba kuna upungufu wa walimu wengi sana hasa wa masomo ya sayansi na hisabati. Hata kwenye Lab. Technician kwa mfano Dar es Salaam, Lab. Technician wanaotakiwa ni 67 waliopo ni 7. Kwa hiyo, mwalimu anafundisha biology, chemistry au physics inabidi aende kwenye Lab. Shule ina wanafunzi 640 mwalimu mmoja wa physics awafundishe wote maana yake unamwambia kwa wiki atasahihisha madaftari 600 mzigo ni mkubwa kweli kweli.

Mheheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba nah ii kazi ya kuhakiki vyeti Mheshimiwa Waziri ambapo mmesema Wabunge, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya hawakikiwi siyo sawasawa sana. Mimi siungi mkono kwa sababu hawa ni watu ambao wanaendesha Mikoa na Wilaya ambapo kuna vyuo vikuu, kuna wataalam, wanaenda kwenye mahafali wanapaswa kuhamasisha vijana wasome. Sasa kama wewe ni Bashite namna gani utamhamasisha mtoto asome shule. Kwa hiyo, ni muhimu kila mtumishi wa umma ahakikiwe na vyeti vithibitike na walio-forge washughulikiwe, ndiyo tutajenga nidhamu ya taaluma ya nchi hii. Profesa hataweza kukubaliana na vitu vinavyofanyika ambavyo siyo sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nilizungumze ambalo mtanisaidia hapa ni uhamisho wa walimu. Ni kweli mnahamasisha mambo ya mahusiano, kuepuka UKIMWI na magonjwa mengine lakini kumekuwa na shida mwalimu kuhama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine aidha mwanamke kumfuata mwanamume au mwanaume kumfuata mwanamke, anapewa masharti kwamba atafute mwalimu mbadilishane. Hiki kitu siyo sawasawa na yenyewe ina-discourage walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwanamke anafundisha Kagera, mwanaume yuko Katavi, hayo mahusiano ya hii familia yanajengwa namna gani na tunataka kuwa na malezi bora?

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo mtu kila siku anafanya kazi anamfikiria mwenzake, mke anamfikiria mume na mume anamfikiria mke na matokeo yake hajiandai, hapitii vitabu mbalimbali, hafanyi andalio la somo na kusababisha matokeo kuwa siyo mazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ile ya Maoni ya Upinzani.