Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE: JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwa haraka tu nianze kwa kutoa pole kwa wale wanafunzi wetu wa Lucky Vincent na Jimbo Vunjo

tulikuwa na wanafunzi wawili ambao ni Irene pamoja na Marioni walikumbwa kwenye mkasa huu. Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa la elimu nchi hii au tatizo kubwa la Taifa letu linaanzia Bungeni hapa. Suala la GPA unakumbuka mwaka 2013, Serikali ilivyoleta hoja ya kuondoka kwenye madaraja kuja kwenye GPA, Bunge hili likashangilia kweli kweli, likapitisha GPA. Baada ya miezi michache wakatoka kwenye GPA wakaja kwenye madaraja, Bunge hili hili likashangilia kweli kweli. Sasa tusitumie wingi wa itikadi zetu kuua Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na hiyo kwa sababu tangu tumepata uhuru, Serikali hii ni mwendelezo. Nimemsoma Eliufoo, hotuba yake hii hapa ya tarehe 11 Machi, 1967. Ukimsoma Eliufoo akiwa Waziri wa Elimu na akitoa ripoti ya Elimu ya mwaka 1966, zaidi ya miaka 50 iliyopita anazungumzia bodi ya kusimamia viwango vya elimu nchini Tanzania, wakati huo Mwalimu Nyerere alikuwa na Itikadi ya Ujamaa, lengo likiwa ni kujitegemea. Kwa hiyo, elimu ilikuwa inatolewa kwa misingi ya lengo la kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nimefanya utafiti, nitampatia na ripoti ya Eliufoo ambayo najua hana, ambayo ina zaidi ya miaka ambayo sijui kama ulikuwa ameshazaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli inaleta uchungu mkubwa sana kwa sababu kila Waziri anayeingia kwenye Wizara, yeye ndio sera, yeye ndio mitaala na yeye ndio kila kitu. Kama Bunge hili tulishangilia GPA, akaja Waziri huyu akabadilisha akaja kwenye madaraja tukashangilia; hivi tupo wapi? Reasoning power yetu ipo wapi? Kufikiri kwetu yamkini kuko wapi? Ndiyo sababu tunafika mahali kama Bunge haliwezi likasimamia Serikali vizuri hatuwezi tukafikiri vizuri, hatuwezi tukaiongoza Serikali vizuri, tutaendelea kupata matatizo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema no research, no data, no right to speak. Mwaka 2013 kwenye Bunge hili, Mheshimiwa Waziri wa Elimu alisema ataleta ripoti ya Sifuni Mchome, alisoma kauli ya Serikali Bungeni na tukashangilia, hii hapa; mpaka leo hii ripoti ya Mchome hatuna na wakati huo wanafunzi zaidi ya asilimia 65 walikuwa wamepata daraja sifuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia wakati Waziri wa Elimu anajibu hoja Bungeni hapa, ninayo majibu yake. Serikali ni hiyo hiyo moja, kwa sababu tangu tumepata uhuru Serikali ni hiyo hiyo moja. Waziri wa Elimu akiwa anajibu tarehe 01 Februari, 2013, siku ya Ijumaa, Mheshimiwa Waziri alitamka Bungeni hapa kwamba yale yote tuliyoyapendekeza yatatekelezwa na akasema Serikali itaunda Tume ya Kudumu ya Elimu nchini ya kupambana na matatizo yote na akaweka neno “education quality assurance and control.” Bunge hili hili! Kwa hiyo, hapa tunapoteza muda tu. Tunaongea, tukishafungasha makabrasha kesho kutwa, tumeondoka, hakuna wa kufuatilia, hakuna tathmini inayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 tulizungumzia kuhusu vitabu, mwaka 2015 tumezungumza, miaka mitano mfululizo tumezungumza udhaifu wa Sekta ya Elimu na tukaambiwa kuwa vile vilikuwa vya EMMAC. Mheshimiwa Mulugo amemaliza kuzungumza, alikuwa Naibu Waziri, waliivunja EMMAC hapa tarehe 5 Juni, 2013. Sasa udhibiti wa vitabu ukapelekwa Taasisi ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli leo hii Mheshimiwa Mama Ndalichako, Serikali ya Awamu ya Tano, wanaandika vitabu, kitabu cha Kiingereza Darasa la Tatu, hapa juu penyewe tu pameandikwa I learn English Language, ndiyo imekuwa ithibati. Hapa Kazi Tu! Serikali ya Awamu ya Tano “I learn English Language,” ndiyo fedha tunazopitisha Bunge hapa ndiyo zinaandika vitabu hivi, “I learn English Language.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu katika chapter one, mwanafunzi anaanza kusoma sentensi, “good morning; thank you; good morning dear mother; good morning, lakini unaenda mpaka chapter five ndiyo wanaanza kusoma a, e, i, o, u. Niliwahi kuimba hapa na leo narudia tena. Tuliwahi kusema kwamba mtoto anaanza kusoma a, e, i, o, u hizi ni herufi kuu tamka kwa sauti kuu ndio a, e, i, o, u na kikombe u, u, u kama jicho e, e, e mwenye mpira o, o, o ni kikombe u,u,u! (Makofi)

(Hapa Mheshimiwa Mbunge aliimba wimbo wa a,e,i,o,u)

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo Kiingereza, chapter five ndiyo wanaanza kuimba a, e, i, o, u, njoo kwenye kitabu cha Darasa la Kwanza cha Kiswahili, yaani ukienda kitabu cha Darasa la Kwanza cha Kiswahili kilichopitishwa mwaka huu na Serikali hii ya Awamu ya Tano kimeandikwa taja majina ya wanyama, “yawanyama” ni neno moja. Ndiyo maana leo hii Wizara inamdhalilisha Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais yupo kwenye TV kila siku anasema “ka ta umeme,” neno moja. Yaani hata silabi haipo, “ka ta umeme,” yaani na watoto wetu ndiyo wanayojifunza “ka ta umeme,” ambayo ni silabi. Sasa quality Assurance and control, iko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Education Act ya 1962 section (3) inazungumzia namna ya kuhakikisha bodi inaweka vigezo gani, marupurupu ya Walimu, marupurupu ya Wafanyakazi, namna ya kuweka mishahara, allowance na kila kitu. Naomba urejee kwenye Education Act section (3) State of Education, inaeleza vizuri kabisa; “there-is hereby established a body to be known as the Unified Teaching’ Service…” na mengine yanaendelea, sitayasoma kwa sababu ya muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema nitampatia Mheshimiwa Waziri hii ripoti ya Eliufoo sasa ya 1967.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mengi ambayo tunayasema hapa, tunasema kwa nia njema kwa kuwa tunalitakia Taifa hili mema, lakini Serikali ambayo inaingia madarakani hata hamfanyi rejea kukaa ofisini, mwenzako amekukabidhi nini, inakuwa ni matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye vitabu sasa hivi, mbili ni namba shufwa au siyo namba shufwa; au mbili ni namba tasa au siyo namba tasa? Kuna mgogoro wanasema mbili siyo namba tasa; ndio sumu tunayolisha watoto wetu leo. Sifuri gawanya kwa sifuri wanasema ni sifuri, wakati haigawanyiki. Namba yoyote ikigawanywa kwa sifuri haigawanyiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa matatizo tuliyonayo, kwa mfano Jimbo la Vunjo, tuna Shule za Msingi 128 lakini Mwalimu mmoja kwa uwiano wa wanafunzi 61, Mwalimu mmoja kwa uwiano wa mkondo mmoja na nusu mpaka miwili, yaani hata miundombinu yenyewe, Kitaifa standard ni Mwalimu mmoja kwa wanafunzi wangapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Walimu wa Sayansi mliowaajiri tarehe 18 Aprili, 2017 hawajapewa fedha yoyote ya kujikimu na hili wala siyo la Vunjo tu, hata kule Rungwe nimepata taarifa zao, Bunda nimepata taarifa zao, Halmashauri ya Moshi nimepata taarifa zao, kote huko ni matatizo makubwa. Sasa kulikoni? Tufanye nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta binafsi, kwa nini hatuweki mazingira rafiki ya kuvutia kwa sekta binafsi yaweze kuwekeza vizuri elimu? Kuna tozo na kodi zipatazo zaidi ya 15 kwenye elimu, nani alisema elimu ni biashara katika nchi hii? Katika karne hii ya Sayansi na Teknolojia kodi 15 kwenye Sekta ya Elimu; tozo na kodi, yaani tumekosa vyanzo vingine vya mapato mpaka tunaenda kufanya elimu kwamba ni biashara!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea namna hii, mazingira ya walemavu wetu, tukienda kwenye TEHAMA, elimu ya juu yaani yapo mambo mengi. Wakati huo wa Mwalimu, walipoamua kutengeneza Taifa lenye skills, uwezo na ujuzi walijenga ile shule ya Galanos, Ifunda na Kibaha, kwa ajili ya michepuo ya kilimo na ufundi na wakajenga shule ya Wasichana ya Bwiru na shule ya sekondari ya Moshi kwa ajili ya mchepuo wa biashara, yaani unakuwa na elimu unajua unafanya nini lakini lengo lake miaka mitano, kumi, 20 ikoje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Mheshimiwa Waziri na ulikuwa kwenye sekta hii, hata tukisoma ripoti mbalimbali, ripoti hii hapa wakati huo ukiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na unajua ile ya mwaka 2010 ikatoka Juni, 2011 unaijua vizuri. Sasa haya mambo ya trial and error maana yake nini? Why? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie na nipendekeze tena kwa sababu naona muda wangu imebaki dakika moja, nasema kwamba elimu ndiyo mapigo ya moyo ya Taifa letu, mapigo ya moyo yakienda kinyume na asilia yake uhai huweza kutoweka. Tunao wajibu wa kuokoa uhai huu kwa sababu maendeleo ya Taifa lolote lile na jamii yake ni tunda la mfumo wa elimu. Lazima tujenge mifumo ya elimu inayojali utu wa mwanadamu, inayokuza utu wetu kwenye utamaduni wa Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.