Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyenzi Mungu aliyeniwezesha kuchangia leo japo kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Maghembe, Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer Makani, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kuhusu uharibifu wa mazingira/maliasili. Serikali inajitahidi sana kutoa agizo na usimamizi wa upandaji miti, lakini baada ya kupanda, nani anafuatilia kuona kati ya miti milioni 1.5 iliyopandwa kwa mwaka ni mingapi imekufa na mingapi inaendelea kustawi kwa kila Halmashauri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Maafisa Misitu Mikoani na Wilayani wapo. Kwa hiyo, naomba kutoa ushauri kwa Mheshimiwa Waziri kupitia kwa Wakuu wa Mikoa watoe agizo la ufuatiliaji wa miti iliyopandwa kwa mwaka husika na ni mingapi imekufa na mingapi imeendelea kustawi? Namna hii tutaweza kuimarisha ufuatiliaji na kutoa report kwa Waziri. Pia itasaidia uwajibikaji wa upandaji miti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kama miti yote au asilimia kubwa ya miti inayopandwa itashika na kuendelea kustawi, tutaweza kurudisha uoto na ukijani wa sura ya nchi mahali pengi Mikoani na Wilayani mwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uharibifu ninaousema ni wa vitendo vya binadamu kwa kukata miti ovyo ovyo bila ya kibali maalum cha kuruhusiwa, ni wapi ukate? Pia kukata tu bila ya kupanda (bila ya kujali sera ya bwana misitu ya kata mti, panda mti) ni kweli wote mnajua kuwa miti nchi nzima inakatwa bila ya mpangilio, hasa katika misitu ya asili. Misitu inakwisha! Naishauri Wizara kuhimiza jambo hili hasa la kutunza miti ya kupanda miti ya asili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina shaka na Mheshimiwa Waziri, naamini ni mtalaam wa misitu, pamoja na watalaam wake. Tafadhali naomba Mheshimiwa Waziri aokoe nchi kwa kuhimiza utunzaji wa misitu ya Tanzania. Sitaki kurudia faida moja moja ya misitu kwani najua mnajua faida zote za misitu, tatizo ni kuisimamia ili iendelee kustawi na kupunguzwa au kukatwa kwa kibali maalum kutoka Wilayani ambapo Mkuu wa Wilaya ndiye Mwenyekiti wa Kamati husika. Naamini mambo mengine yanaingiliwa na Wizara kwa Wizara tofauti. Shirikianeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miti hiyo inakatwa kwa madhumuni mawili makubwa; kuni na mkaa. Namba ya tatu ya ukataji wa milunda ni kwa sababu ya ujenzi na miti mingine inakatwa bila vibali kwa madhumini ya kutengeneza mbao. Tafadhali tafuta mbadala ya kila kimoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, karibu asilimia 90 ya wananchi (Watanzania) wanatumia kuni na mkaa. Mheshimiwa Waziri, wewe ni mzoefu wa miaka mingi katika tasnia hii; je, tufanyeje kuokoa nchi na kupunguza au kuokoa kilio cha miti? Nashauri chekecheni vichwa watalaam, saidianeni na Katibu Mkuu, Naibu Waziri na Waziri mwenyewe kutafuta nishati mbadala ya kuni na mkaa ambayo itakuwa rafiki na wananchi wengi kama siyo wote kufuatana na aina ya nishati na mahali walipo. Kwa mfano, huu ushauri, ukiambatana na agizo na Sheria Ndogo ya Halmashauri tunaweza kushinda tatizo hili lililo mbele yetu kwa miaka yote. Kwa upande wa familia za wafugaji nashauri waelimishwe kutumia biogas kwani wanayo source.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na wafugaji, pia wananchi wengine wanaofuga ng’ombe wachache au mifugo mingine nao wapewe elimu ya biogas. Wananchi wengine kwa kushirikiana na watalaam husika waelekezwe jinsi ya kutumia joto la jua (solar). Naamini ni kujipanga na kuamua, wananchi wakielekezwa ni nini cha kufanya na kubanwa na utaratibu, sera, sheria ndogo watafuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia ya wananchi wanaotumia gas asilia ya nyumbani imeongezeka kidogo na hasa ukichanganya na asilimia ndogo sana inayotumia umeme. Tatizo kubwa ni bei. Mtungi wa gesi wa kati sasa ni kati ya shilingi 68,000; shilingi 54,000 mpaka shilingi 52,000 kufuatana na mkoa kwa mkoa. Mtungi huu ukibahatika utachukua wiki mbili au mwezi kwisha (inafuatana na wapishi na matumizi). Hivi kweli kufuatana na mishahara yetu, wangapi Watanzania wataweza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iingilie kati kushauriana na wafanyabiashara wa gesi ya nyumbani ili bei ipangue watu wengi waweze kumudu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa umeme, sisemi kwani ni ghali zaidi. Shaurianeni na Waziri wa Nishati. Namna hii tutaokoa maliasili yetu hasa misitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi wakati wa Maonesho ya Nane Nane wavumbuzi wajasiriamali wanaonesha aina mbalimbli za nishati, lakini hakuna anayezitilia maanani, mbali ya kuziona na kuwasifia. Nashauri tujaribu kuziendeleza zinaweza zikawa mkombozi kwa mfano, makaa ya magazeti/karatasi, joto la majiko (banifu), pumba (husks) ya mpunga na kadhalika. Okoa maliasili yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie utunzaji wa misitu. Huu ndiyo ushauri na ombi la Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo niongelee utalii. Nashauri utalii na hasa vivutio vya kila mkoa vitangazwe kikamilifu kwa pamoja na kuwavutia watalii wengi. Tamaduni za makabila yetu, pia ni utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia.