Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii. Hata hivyo, nitoe ushauri kwa Serikali na Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulinda na kuhifadhi eneo oevu la River Malagarasi. Eneo hili ni Ramsar Site chini ya udhamini wa UNESCO. Eneo hili limevamiwa na ng’ombe wengi ambao baadhi yao ni wale walioondoshwa huku Burigi Pori la Akiba na Kimisi. Ng’ombe hawa wanahatarisha uhai wa Mto Malagarasi. Chukueni hatua haraka bila kuchelewa ili kuokoa rasilimali hii muhimu kwa Taifa na kimataifa. Bila Mto Malagarasi hakuna Ziwa Tanganyika na bila Ziwa Tanganyika hakuna Mkoa wa Kigoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la Msitu wa Taifa wa Makere Kusini maarufu Kagera Nkanda lenye ukubwa wa hekta 97,000; Wilaya ya Kasulu tumeomba hekta 20,000 - 25,000 ili wananchi wapate eneo la kilimo na kufanya shughuli za kufuga nyuki na wanyama wengine. Tunahitaji sasa eneo hili lipimwe upya ili kuhuisha mipaka ya wakoloni (Waingereza) ambao walitangaza msitu huo mwaka 1954. Zaidi ya miaka 60 haiwezekani mambo yawe yale yale wakati idadi ya wakazi imeongezeka mara kumi. Baada ya re- mapping hiyo hali ya amani na utulivu itarejea baina ya wananchi na Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mbuga ya Hifadhi ya Gombe na Mahale zilizopo Mkoani Kigoma; mbuga hizi ni mpya, ardhi ni mpya na miundombinu yake ni mipya. Juhudi kubwa lazima ifanywe ili kutangaza vivutio vya pekee vya sokwe wanaopatikana katika mbuga hizo mbili katika nchi yetu. TTB wafanye kazi ya kutangaza vivutio hivi kwa juhudi kubwa. TTB wanaweza hata kutumia mbinu ya PPP/TTB Joint initiative. Taasisi ya Jane Godall watafiti wa sokwe Kigoma wanaweza kushirikishwa pia. Jengeni upya wa fikra katika tasnia hii ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivutio vipya vya utalii vilivyopo katika Mkoa wa Kigoma ambavyo vinahitaji kutangazwa na TTB pamoja na TANAPA ni pamoja na:-

(i) Njia ya watumwa ya Kigoma/Ujiji - Tabora - Dodoma - Morogoro hadi Bagamoyo. Hiki ni kivutio kikubwa sana kama kitakuwa promoted na developed. Njia hii ipo kihistoria, kazi ni kuwa na mkakati wa muda mrefu na dhamira ya dhati ya Wizara hii na TTB, tuanze sasa.

(ii) Makumbusho ya Dkt. Livingstone alipokutana na Dkt. Henry Morton Stanley 1871. Jengo la makumbusho lipo limejengwa, likamilike ili lianze kazi. Utendaji kazi wake lazima uende sambamba na promotion ya kivutio hiki. Nina hakika eneo hili linaweza kuingiza mapato mengi Serikalini.

(iii) Cultural tourism - Kigoma is rich in cultural activities lets promote this area. Tuanze sambamba na kutangaza mbuga zetu za Gombe na Mahale.

(iv) Ziwa Tanganyika na fukwe zake, hiki nacho ni kivutio kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TTB amkeni sasa, njooni na mikakati endelevu.