Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Edwin Mgante Sannda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza niende moja kwa moja kwenye ushauri, leo nitakuwa nafanya zoezi la ushauri tu kwa Wizara na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo kama linanishangaza kidogo, ninaposikiliza Wabunge wenzangu wote na ninapofuatilia hali halisi ya migogoro inayotokana na mwingiliano mkubwa kati ya maeneo ya hifadhi pamoja na maeneo ya makazi nashangaa sijaona kama jambo hili limewekewa uzito sana kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri na nilitegemea kwa kuwa hili ni tatizo kubwa sana lazima ungelizungumzia kwa kina sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, karibu kila pori la akiba, kila eneo la hifadhi ni vurumai tu. Tumesikia madhara makubwa ya migogoro, tumesikia vifo, tumesikia wanyama wanadhurika ndiyo maana tunazungumzia habari ya kufanya mipango mizuri ya ardhi kwa ajili ya kuweza kutenga maeneo ya ufugaji, maeneo ya hifadhi na maeneo ya kilimo. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijaona uzito unaostahili kwenye hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende mbele kidogo kwamba, tatizo hili limekuwa la muda mrefu sana, kila kwenye pori kelele ni hizo, miaka nenda, miaka rudi ni kero kubwa kweli. Hatuna budi tufike mahali sasa tuweze kupata ufumbuzi wa kudumu kabisa wa migogoro hii baina ya maeneo ya hifadhi, mapori ya akiba, vijiji, maeneo ya wafugjaji na maeneo ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri kitu kimoja, tufanye mpango mahsusi wa kuwekeza kwenye elimu kwa mambo makubwa matatu. Elimu kwa maana ya mafunzo, hamasa na programu shirikishi. Kwanza kwa ajili ya kuimarisha mipaka, wakati wa kuimarishwa lazima tushirikishe wale wananchi vilevile. Tunapofanya wenyewe mwisho wa siku wananchi wanakuja kuona kwamba “aah, hawa walibadilisha mipaka” malalamiko mengi yamekuja maeneo ambayo wanasema mipaka ilikwishapimwa, zoezi la kuja kuimarisha na kuweka zile beacon limechukua muda mrefu. Serikali ilivyokuja kwa maana ya Wizara ilivyokuja walikwenda wenyewe, hawakushirikisha wale wananchi pale kiasi kwamba wananchi wanaona “aaah! hawa watu wametuvizia wakati hatupo wamekuja wameweka mipaka usiku” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kuna tatizo au shida gani ya ku-involve wananchi wakati wa kwenda kuimarisha mipaka. Kwa nini tusitumie muda mwingi angalau kuwaunganisha na kuweza kufanya nao kazi pamoja ili kuepuka lawama hizi na migogoro huko mbele. Nisisitize sana wakati wa mazoezi ya kuimarisha mipaka, kwanza tusichukue muda mrefu, lakini wakati wa zoezi hili tushirikishe sana wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine katika mapato tunayoyapata kwenye hifadhi zetu. Tuwekeze kidogo kwenye elimu ya uhifadhi kwa wananchi. Wananchi nao waweze kuelewa kwa nini na wao wawe sehemu ya kulinda yale mazingira ambayo tumeamua kuyahifadhi, nao wanufaike kwa namna moja au nyingine. Tukiwekeza kwenye elimu hiyo, vurumai itapungua, watu watazuia mifugo, wataacha shughuli za kibinadamu kwenda kwenye maeneo yaliyohifadhiwa itakuwa ni win win situation. Tumeweka kidogo na wao wanakaa kule wanajua kabisa kuna umuhimu, leo nimepata labda kisima cha maji pia, wakati mwingine wamekuja watu wametupa mafunzo hapa kama wanakijiji, keshokutwa tumepata madawati, tumejengewa madarasa. Tujitoe kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu hapa mmoja alisema ukitaka kula ni lazima uliwe, lazima utoe hela ili uweze kupata manufaa. Naomba nisisitize sana kwenye elimu ya uhifadhi kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuwekeze kwenye elimu ya utii wa sheria bila shuruti kwa wananchi na kwa wale Askari wetu maana tumekuwa na kesi nyingi sana. Mara ya mwisho niliongea hapa kuhusiana na Wizara hii, kesi kubwa sana ya mauaji. Sasa tufanye utaratibu ambapo yule Askari anaji-feel responsible kumkamata mtu, amhoji vizuri, afuate taratibu mpaka yule mtu amtie kwenye mkono wa sheria, siyo anajichukulia sheria mkononi. Wananchi nao pia waweze kuelewa kwamba ninapokutana na labda wanyama wameingia huku kwetu sio naua tu au sio nafanyaje. Tutii sheria bila shuruti, bila kuingia kule, bila ya kwenda kwenye hifadhi kufanya shughuli za kibinadamu, itatusaidia sana kupunguza hii migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la migogoro limekuwa ni kero kubwa ambayo bila ya kuiwekezea hivi hatutaweza kuimaliza kwa muda mfupi. Mheshimiwa Waziri, pia tufanye uwekezaji kwenye kutoa elimu ya ku co-exist. Wale watu wanaoshughulika na uhifadhi na wananchi waweze kuona umuhimu wa ku co-exist wao pamoja. Kila mmoja ni muhimu kwa mwenzio, siyo mmoja amuone, imefika wakati wanyama wanaonekana ni muhimu kuliko wanadamu, hatuwezi kwenda namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitoa ule mfano wa kijana aliyeuawa kwa ajili ya sukari guru, haiwezekani hata kama ameua mnyama gani, hebu tuone namna gani tunaweza tukaona kila mmoja kwa nafasi yake tunaweza tuka co-exist. Siku moja moja mwisho wa siku wakafikia wakaoana kati ya wahifadhi na wananchi kawaida wakawa wanakaa wanashirikiana kwa kila namna. Katika ufumbuzi ninaouona mkubwa wa hii migogoro, tuwekeze kwenye kutoa elimu katika nyanja aina hizo tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili nataka nizungumzie kwenye suala la utangazaji. Utangazaji wa vivutio vyetu, kwa kweli hatujawekeza vya kutosha. Wamezungumza Wabunge waliotangulia, huko tunaona wenzetu takwimu za watalii zinazidi lakini siyo bure, watu wame-invest kama kuna sera, kama kuna utaratibu wa kushirikiana na sekta binafsi kushirikiana na hizi wakala na taasisi mbalimbali tuweze kuongeza uwekezaji kwenye kutangaza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Waziri, ile michoro ya mapangoni ambayo iko kwenye historia sisi toka tuko wadogo tunaisoma, tunayo michoro zaidi ya
450. Wangapi wanaijua hapa, wala haiko mbali, iko hapa Kondoa tu kwetu. Wangapi wanaijua ile michoro, hatujai- promote, tumeiacha na ofisi ziko pale lakini hata rasilimali watu sijui kama inazingatiwa, kama watumishi wapo, yaani pako dull kwelikweli ni kana kwamba vivutio hivi havipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuwekeza, tunahitaji kujitoa ili tuweze kuvutia watalii wengi na tutaongeza kipato kupitia njia ya namna hii. Ni lazima tu- invest ili wale watalii tunaotaka waje, watakuja kwa wingi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri napenda sana nizungumzie kuhusiana na uwekezaji hususan kwenye maeneo ambayo yapo, tunayajua kihistoria lakini tumeyaacha kama malikale zimelala, tumeandika kidogo sana kwenye hotuba yetu hapa. Inaonekana hata dhamira ya dhati ya ku-promote vivutio hivi ni kama haipo. Sasa huku kwenye kutenga fedha ndiyo kabisa, kuko kutupu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwa safari yetu tunayotaka kuboresha utalii, nafikiri kwa utaratibu huu tutakuwa tumekwama sana. Namwomba pale anapokuja kwenye majumuisho nategemea na naomba nisikie anatueleza nini kuhusiana na investment kwenye promotion ya vivutio vya utalii, malikale na mengineyo. Pia atueleze vizuri mipango na programu zilizopo na uwekezaji ambao upo au anapanga kuuweka kwenye utatuzi wa migogoro hasa kwa njia hizi shirikishi. Kadri nilivyokuwa nimeelezea kwa maana ya kutoa elimu ya uhifadhi, kwa maana ya kutoa elimu ya kutii Sheria bila shuruti na kutokujichukulia sheria mkononi na pia kwa maana ya elimu ya co-existence, pamoja na programu shirikishi za kuwa- engage wananchi ili nao wajione kwamba ni sehemu ya uhifadhi na wasije kuwa wao ndiyo tatizo au changamoto zinazosababisha hii migogoro, badala yake wao wawe chanzo cha ufumbuzi na suluhisho katika kupata majibu ya migogoro hii ambayo imekuwa kero kubwa na inaleta madhara, inapoteza nguvukazi, watu wanakufa kila leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kondoa kuna mapori mawili, yote ni vurumai, karibu mara zote tunasikia huko watu wamekufa watano, mara amekufa mtu mmoja. Kila unapokuta pori la akiba au maeneo ya hifadhi ni vifo. Mheshimiwa Waziri tutavimaliza lini hivi, kweli kila siku tunazungumzia jambo moja tu la migogoro baina ya maeneo ya hifadhi? Tumeshindwa kabisa kupata ufumbuzi wa kudumu wa mambo haya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya kweli ipo katika hili? Mheshimiwa Waziri na...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.