Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami naungana na wachangiaji wote waliopita kwa suala la kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini. Tusipoanzisha Wakala wa Maji Vijijini, tutaimba nyimbo za siku zote ambazo hazitapatiwa majibu. Tukianzisha wakala tutaepusha malalamiko mengi ambayo yanajitokeza kwenye vijiji.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo ambayo ni vigumu sana kuweza kuyakamilisha kwa sababu suala la maji linahitajika maeneo yote. Wanafunzi hawawezi kukaa darasani kwa muda wote kama maji hayapo. Pia, kilimo tunachokisema kila siku kama uti wa mgongo na majina mengi ambayo tumejipa, hatuwezi kukidhi malengo kama suala la maji halitapewa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali, unajua tumekuwa na vipaumbele vingi, hebu tukae tuangalie kipaumbele ambacho Watanzania wanakizungumza. Leo kama maji ni kipaumbele cha nchi hii, hatuwezi kupunguza bajeti, tungeongeza bajeti. Inaonesha ni jinsi gani mambo tunayoyazungumza hapa ni kama kuna watu wengine washauri tena tofauti na Bunge. Suala la maji tulizungumza, tunazungumza tena, lakini kuna mambo ambayo yanapewa vipaumbele nje na yale ambayo Wabunge wanazungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Serikali, ni vyema wakazingatia basi yale ambayo tunayazungumza. Ukitazama hili suala la maji haliko upinzani, haliko chama tawala, wote tunazungumza maji, maji, maji. Tunaomba basi tupate mikakati ya Serikali, angalau basi wawe wanatusikia na kutusikia ni pale wanapojibu yale tunayoyazungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia vyeti fake, kuna bili fake, sijui kama Waziri anajua. Kama maji hayapo lakini bili zinasoma, zinasomaje? Kwa hiyo, kipindi wenziwe wanazungumzia vyeti fake, yeye ajue kuna bili fake! Naomba aje hapa atuambie kama maji hayapo bili zinakujaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye Mkoa wa Rukwa lazima wakae pamoja Wizara tatu, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji na Mazingira. Mkoa wa Rukwa hatujawahi kulia njaa hata mwaka mmoja lakini kinachotokea saa hizi kwa ajili ya kufurahishana, yaani anakuja mtu wa mazingira, wananchi wamelima mahindi, anawaambia wakate wamelima kwenye vyanzo vya maji. Ni kweli hatukubali kulima kwenye vyanzo vya maji lakini watuambieni Serikali wametenga eneo gani mbadala wananchi wakalime? Hatulimi bangi bali mazao ya chakula. Tunahitaji wakae pamoja waje na majibu ya kueleweka ya kuwasaidia Watanzania. Ni kweli wanaepusha vyanzo vya maji visiharibiwe lakini wanataka watu wafe na njaa? Waje watupe majibu ya uhakika Watanzania wa Rukwa wajue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nimwambie kwa taarifa tu Mheshimiwa Waziri, mwaka jana tu wanawake 12 wamepoteza maisha kwa kufuata maji umbali mrefu. Leo tunazungumzia maji hayohayo tena tayari bajeti imepungua wakati maji bado hawajapata. Leo mimi nakujaje


namshangilia hapa Mheshimiwa Waziri wakati wanawake walionipigia kura wanapoteza maisha na bado hana mikakati yoyote ya kuonesha mazingira rafiki ya kuwasaidia maji. Tunaomba majibu ya kuridhisha ambayo yatawasaidia Watanzania.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huu tunazungumza kuna wanawake ambao wamefariki, kuna wanawake ambao wamebakwa, kuna wanawake ambao wameathirika kuhusiana na ndoa zao, kuna wanawake ambao wamepoteza mapato, huu muda wanaofuata maji wanashindwa kufanya biashara wanaanza kuhangaikia maji. Mheshimiwa Waziri tunaomba na Waziri anayehusika na upande wa watoto, Wizara ya Afya, hakuna kitu kitawezekana bila maji. Kwa hiyo, wanapokaa pamoja waangalie basi, maji ni kipaumbele hakuna mambo mengine. Nakushukuru.