Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia mjadala wa hotuba hii ya maji. Nami naunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na niwapongeze sana kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya.


Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajielekeza katika kuwaombea maji wananchi wangu wa Mkuranga, uniruhusu nitumie nafasi hii ya dakika moja, mbili kuwaonesha Watanzania kwamba Chama cha Mapinduzi bado ndiyo Chama imara chenye haki ya kuendelea kuwaongoza Watanzania. Tulipokuwa katika uchaguzi wa East Africa kwenye Bunge hili, hatua ya kwanza Chama cha Mapinduzi kiliwakataa Mheshimiwa Wenje na Mheshimiwa Masha. Wenzetu wakaondoka wakaenda kuwaambia Watanzania kwamba sisi tunataka kuwachagulia watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jana unafiki wa Vyama vya Upinzani umedhihiri katika Bunge hili. Wale waliowaleta sisi tukawakataa, wametusaidia jana kuwakataa kwa vitendo. Makamu Mwenyekiti wao Profesa Safari wamempa namba ya viatu, namba 35, Wenje wamempa namba 34, Masha wamempa namba 44. Tunaendelea kuwaambia Watanzania kwamba Chama cha Mapinduzi ndicho chama cha kweli na ndicho chama cha kukiamini na Wapinzani hawa ni wanafiki wakubwa! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo na ujumbe umefika, naomba nisema yafuatayo sasa.

UTARATIBU...

MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka tuwaambie sisi bado ni Walimu katika Taifa hili, wao wakijua hivi, sisi tunajua hivi, hiyo ndiyo habari. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waitara, rafiki yangu kwamba hiki ndiyo Chama cha Mapinduzi ambacho hata yeye kilimlea pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana tumeendelea kuuthibitishia Umma wa Watanzania kwamba hiki ndiyo Chama cha Mapinduzi. Tutaendelea kuwafunzeni siasa, kwa sababu hiyo ndiyo kazi yetu. Kesho tutakwenda kupitisha bajeti ya Wizara ya Maji. (Kicheko/Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu ni kutaka kuona kwamba katika bajeti hii ya Wizara ya Maji tozo ya shilingi 50 inaongezeka. Mheshimiwa ukikaa hapo katika kiti tuelekeze, Kamati yetu ya Bajeti ikakae na Serikali iongeze bajeti ile ya tozo ya shilingi 50 tukawahudumie Watanzania. Watanzania wa Mkuranga Mjini wanayo maji pale katika Mlima Kurungu, kisima cha mita 600, kuna maji ya litres nyingi yanapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu mmoja pale anaitwa Manyaunyau, anawauzia Watanzania wa Mkuranga maji. Mtu mmoja amechimba yeye binafsi. Katika bajeti ya 2014/2015 zilitengwa hela hazikwenda, mwaka huu wa fedha wa 2015/2016 uliokwisha zilitengwa pesa hazikwenda. Sasa katika bajeti hii tunachotaka pesa ziende. (Makofi)



Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali. Katika miradi ya visima kumi, mimi nimechimba visima kumi Mwanambaya, Mlamleni, Mkenezange, Kimanzichana, Mdimni, Ng’ole, Mbulani, Yavayava, nimechimba huko kote. Ninachosubiri sasa ni kuona miundombinu ya maji inaenea kwa wananchi wa Jimbo langu la Mkuranga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sina wasiwasi kwa sababu nikimtazama jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, naamini kabisa kwamba maji yanakwenda kutatuka na Watanzania ile nia yetu tuliyowaambia ya kumshusha mama ndoo kichwani, tutaifanya hiyo kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri mimi ni Mbunge mpambanaji.

T A A R I F A....

MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, unilindie muda wangu. Nimesema hapa ya kwamba na sisi hicho alichokisema ndicho tunachokitaka. Hizi pesa zilizotengwa tuhakikishe zinakwenda kwa wananchi. Hizi pesa zikienda, tuna hakika azma yetu ya kumshusha mama ndoo kichwani itakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema hapa ya kwamba tuongeze tozo hiyo shilingi milioni 181, ninety something millions zote zimetoka katika tozo ya mafuta. Tukiongeza tuta-double, tutawasaidia Watanzania wakiwemo wa kwa rafiki yangu Mwalimu Marwa kule Serengeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kwa umuhimu kabisa, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri anisaidie kunipelekea pesa zile. Ukurasa wa 163 ziko peza zinapelekwa kwenye Miji 63. Mmoja katika huo Mji uwe ni Mji wa Mkuranga. Sisi hatutaki pesa nyingi, tunataka kama shilingi milioni 800. Nami kwa kuwa ni Mbunge mpambanaji, nimeshajiongeza, nimezungumza na Ubalozi wa Kuwait, wameniambia yatoe maji kutoka mlima Kurungu yapeleke katika tenki. Jenga tenki, sisi tutakusaidia katika pesa za kufanya distribution. Unataka nini tena? Mungu akupe nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa heshima kubwa na taadhima niseme kwamba Mawaziri wetu chapeni kazi, sisi tuko pamoja na ninyi, kazi yenu mnayoifanya tunaiona na tunataka tuwahakikishie mkienda mkakaa Serikali na Kamati yetu, mkatukubalia, tukaenda kubadilisha katika Sheria ya Fedha, tukaongeza tozo ya shilingi 50, basi mambo yatanoga sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.