Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Mnyika nataka nikuhakikishie kwamba ni vyepesi sana ngamia kupenya tundu la sindano kuliko upinzani kuiondoa CCM madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kumpongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa jitihada kubwa anazozifanya kwa kuwatetea wanyonge wa Tanzania na kutetea maslahi ya nchi hii. Ninampongeza kwa sababu amejitoa mhanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukawa Rais lakini usijitoe mahanga kwa ajili ya kupigania maslahi ya watanzania na kuziacha rasilimali zikiporwa na kutumiwa na watu wachache; ninampongeza sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli na ndiyo maana zile pushapu alizopiga, na yale majina ya tingatinga tuliyompa na zile nyimbo tulizokuwa tunaimba za Kisukuma ling’ombe lyamapembe, lyekumakinda mumbazu ndiyo maana sasa matunda tunaanza kuyaona, ndiyo maana amewanyima pumzi mafisadi, wakwepa kodi amewanyima pumzi hawapumui, wenye vyeti fake hao nao na wenyewe sasa ndio wanakandamizwa, ninakuomba Mheshimiwa Rais uendelee kukandamiza hapo hapo na wala usibadilishe gear. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge nianze kwa kuwapa nukuu zifuatazo, nianze na ukurasa wa 30 wa kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri, anasema; “Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa ndiye msemaji mkuu (champion) wa masuala yanayohusu maji Barani Afrika.” Na kwamba Waziri mwenyewe ni Rais wa Baraza la Mawaziri wa maji Afrika kwa kipindi cha miaka miwili. Waheshimiwa Wabunge, u- champion huu naomba niwakushe, u-champion wa maji wa Mheshimiwa Rais wetu aliuanza wakati ule alipopiga push up kwenye kampeni, na aliponyanyuka kutoka chini kwenye push up aliwaambia Watanzania kwamba najua Watanzania akina mama mna tatizo la maji, ninakwenda kutatua tatizo la maji na ole wake Waziri wa Maji nitakayemteua asipowaleteeni maji nitamgeuza kuwa maji na Watanzania waweze kumnywa. Mheshimiwa Waziri, bajeti hii jiandae sasa unaenda kugeuzwa maji endapo tozo ya shilingi 50 haitakubalika na kuongeza pesa kwenye bajeti hii, kwa ajili ya kutatua kero ya maji kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini champion mkuu wa maji Waheshimiwa Wabunge ni Yesu Kristu Mwana wa Mungu. Ukisoma Yohana 19:26-28 Yesu alipopata maumivu msalabani anateswa wakati mama yake yuko pembeni, alimwambia; “mama tazama mwanao” na baadaye alipoona kwamba lazima haya yakamilike akasema; “naona kiu.” Hakuna kitu kingine ambacho Yesu alikiona ni isipokuwa kiu, kiu ni maji na ndiye champion mkuu wa maji kwa ajili ya akina mama katika Taifa letu. Tatizo la maji kwa akina mama, huu ni mwaka wa saba nilipoingia Bungeni humu niliingia na nyoka ya shaba, nikawaambia akina mama msichague Wabunge ambao watapitisha bajeti isiyotatua kero ya maji. Leo ni mwaka wa saba maji bado ni kero kwa wananchi hasa Watanzania akina mama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie Wabunge wenzangu atakaye kwenda kupitisha bajeti hii kwa ndiyo! Ndiyo! Ndiyo! Ndiyo! Wakati Bajeti hii, haijaongezwa pesa ya tozo ya shilingi 50, niko tayali na mimi kuanzisha mwenge, mwenge wa sauti nitachukua kwenye Hansard sauti za Wabunge za ndiyo nitazikimbiza nchi zima kuwaambia akina mama sikilizeni Wabunge wanavyowasaliti na nyinyi hampati maji katika nchi yenu. Lazima tuwe na huruma kwa akina mama. Waheshimiwa Wabunge ni nani ambaye hakunyonya mtindi kwenye ziwa la mama yake katika nchi hii? Waheshimiwa Wabunge ni nani ambaye hakuishi miezi tisa kwenye tumbo la mama yake halafu leo inakuja bajeti ambayo haitatui tatizo la maji tunaendelea kufanya ushabiki katika suala la msingi la bajeti ya maji, hatutakubali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule vijijini kule Mwibara kule, miradi ya Buramba, miradi ya Kibara, Bunda Mjini amesema Mheshimiwa Ester Bulaya hapa, zaidi ya miaka kumi akina mama hawapati maji, kwa nini, ni kwa sababu ya Bunge hili lenye uwezo wa kutatua kero ya maji kwa akina mama tunafanya ushabiki na kupitisha bajeti ambazo hazitekelezeki. Naomba Waheshimiwa Wabunge tukatae. Nitashangaa kwa kweli Mbunge atakayepitisha bajeti hii ambayo haijaongezwa pesa za maji. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, ngoja ni waambie, kule vijijini wako wanaume ambao sasa hivi ni vilema ambao akina mama wanawaacha vitandani saa kumi usiku na kurudi saa tano ilhali wanadhani wana wivu kwamba akina mama wanakwenda kufanya mambo mengine wanapanda juu ya miti, matokeo yake wanadondoka wanakuwa ni vilema, leo tunakuja kufanya mzaa hapa. Waheshimiwa Wabunge, kule vijijini wanaoga kwa zamu maji hayatoshi. Aoge baba, aoge mwanafunzi aende shule, lakini hata wale wanaopata maji ya kuoga na wao wanachagua sehemu nyeti tu za kuoga kwa sababu maji hayawatoshi, halafu tunakuja tunafanya mzaa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye umwagiliaji. Nilishasema hapa Bungeni. Kule Mwibara kuna bonde zuri kwenye Ziwa Victoria kuanzia Musoma Vijijini kule Bugwema linakuja linapita kwenye kata ya Butimba maeneo ya Kabainja linaenda Karukekele, Namhula, Bulendabufwe, Igulu matokeo yake linaingia mpaka Genge, Kisolya mpaka Nansimo lakini hatuna umwagiliaji. Tumechoka kuletewa mahindi ya msaada ya kilo nne kwa familia ilhali tuna maji ya Ziwa Victoria. Tunaomba miundombinu ya umwagiliaji. Nimeangalia kwenye kitabu hiki hakuna kabisa, lazima tutende haki kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye mgawanyo wa fedha za maji. Nilikuwa nasoma humu unakuta kuna Halmashauri nyingine zina kata sita wana shilingi bilioni nne za maji. Kuna Halmashauri nyingine wanakata 20 mpaka 30; kuna Halmashauri nyingine zina majimbo mawili lakini wanapata shilingi milioni 800 tutakwenda wapi sisi, tutawambia nini wananchi wetu kwenye mgawanyo kamba huu? Tunasema tunagawana sungura mdogo, haiwezekani Halmashauri nyingine; niliona ya Mheshimiwa Kitwanga hapa ana shilingi bilioni nne wengine tuna shilingi 500,000,000 au kwa sababu anatishia kung’oa mitambo ya maji ndiyo sababu mnapatia maji? Haiwezekani, huyu sungura mdogo lazima tugawane hapa pasu kwa pasu; haiwezekani kabisa Halmashauri ipate shilingi milioni 500 wengine wana shilingi bilioni nne; haiwezekani tukamla kuku wengine wakachukua mapaja, wengine wakachukua mnaita chenye mafuta mafuta kile, halafu wengine mafuta mafuta yale, kakiuno kana mafuta na haka kakiuno kenye mafuta ndiko ambako wewe Waziri umechukua, ndiko wewe Naibu Waziri umechukua na sisi tunakataka hako, na sisi tunataka mafuta haiwezekani…(Makofi/Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ALPHAXARD K. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana