Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Savelina Slivanus Mwijage

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nami ninaomba kuchangia Wizara hii ya Maji ambayo watu wengi wamechangia na mimi niweze kuchangia. Nilikuwa naomba sana, ningekuwa na uwezo hii Wizara ningeweka Mwanamke mmoja. Matatizo ya maji yanawasibu wanawake ndiyo maana tunapata matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kitabu cha nne Serikali haikutenga pesa katika mradi wa maji Mkoa wa Kagera. Tuna shilingi bilioni nne za wahisani na Mkoa wa Kagera Mwenyezi Mungu alitujaalia vyanzo vya maji na kila siku naongelea hapa. Kuna Mto Kagera, tuna Ziwa Victoria na Itimba, tuna Buhigi; ukizunguka Mkoa wa Kagera mzima tuna vyanzo vingi ambavyo ni vya kuweza kuwasaidia Wana Kagera, lakini ndio wa kwanza wanabeba ndoo baada ya kutua ndoo wanabeba ndoo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimeingia hapa mwaka 2005, kila mwaka nimelia na maji mpaka nimemaliza; na kila mwaka na kila bajeti tunalia na maji na ndio maana nasema hivi ukingalia Wizara ambazo wakina mama wameshika, wanajitahidi kutafuta vyanzo vya maji kuwasaidia akina mama wenzao ambao wanateseka na maji. Angalia Mheshimiwa Ummy, sipendekezi kwa sababu ni Kamati yetu, hapana, anajitahidi sana kuhangaika kutafuta vyanzo. Tunawawekezaji, mwekezaji akiingia kuwekeza ndani ya Mkoa au Wilaya kitu cha kwanza ukimwekea awe anachimba mabwawa kuwasaidia akina mama inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa ukiangalia hata kwenye hospitali hakuna maji, Hospitali ya Bukoba Vijijini akina mama wananunua ndoo shilingi 1,000. Ameenda kujifungua ataondoka na uchafu! Akina baba mmependeza kwa sababu ya maji. Mama atafulia nini kukufulia suti yako? Tukikosa hata maji ya kufua suti akina baba labda mtakuwa na uchungu wa kuwatetea akina mama wasibebe ndoo kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanawake wanatembea kilometa 20 au 15 kutafuta maji. Anaondoka asubuhi hajatafuta chakula, hajajua anapika nini, hajajua atalima wapi, hajajua atafanya nini lakini anakwenda kutafuta maji na maji yenyewe hayatoki; kama mnavyosema kwamba ni mabadiliko ya tabia ya nchi, mito mingi imekauka. Tuna mradi nimeuongelea hata hata mwaka jana, Mradi wa Kahama na Shinyanga, mnashindwa nini kuwasogezea watu wa Bukoba? Watu wa Muleba wamezungukwa Kanda ya ziwa yote imezunguka maji. Ukienda Ngara wana Mto Ruvu na Mto Kagera umezunguka una maji, watu wa Misenyi wanakunywa maji ambayo ukiyaangalie hata wewe kwenye glasi utafikiri ni maziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mtanzania wa karne hii mpaka huyu wa sasa hivi bado wanakunywa maji machafu kiasi hicho. Tuna Kienyabahsa kuna mto mkubwa ambao unaweza kusambaza hata Bukoba Vijijini. Tuna Ikimba ambayo inaweza ikasambaza hata Bukoba Vijijini na Wilaya zingine jirani; lakini ni kukosa kuwa na ma-engineer na Waheshimiwa Mawaziri muwe wabunifu wa kuweza kuleta hata wataalam kuchimba mabwawa ili watu wapate maji salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Karagwe kwa ndugu yangu Bilakwate, ni mjomba wangu, lakini pale ukienda utasikitika hawana maji kabisa na sasa hivi mvua inanyesha kwa nini usiwe na watalaam wa kuweza kutengeneza mabwawa angalau tukawa tunavuna maji ya mvua ya sasa hivi?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunalia na mafuriko hapa kila Mbunge anayesimama hapa analia na mafuriko. Yale maji tukiyavuna tukatengenezewa mabwawa kitaalamu tunaweza kupata maji miaka hadi miaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye kilimo cha umwagiliaji na ninalia kila siku, hapa huwa nauliza kwamba maswali ni kwa nini tusipate wataalam wa kuwafundisha wananchi wetu kulima kilimo cha umwagiliaji ili tukaweza kupata chakula cha kutosha na akina mama wakapata ajira ya biashara ya kuweza kuuza mboga na chakula? Kila siku tutakuwa tunasimama hapa tunalia na jambo moja la maji, maji/kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri nawaomba sana na ninyi mna wanawake mna mama zenu na ndugu zenu, muwasaidie hawa akina mama. Au tuwabebeshe ndoo, wakati mmoja na sisi wanawake tusimame tuseme wanaume mtuletee maji, mtaweza? Hamuwezi! Kwanza hata kusogeza chakula kwenyewe kukitoa hapa kukiweka pale unasema mwanamke kaniroga ananiambia nibebe chakula, sasa ukiambiwa ubebe maji! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na wewe ni mama, tunaoma sana muwaokoe akina mama hata akienda kujifungua hospitali, akiwa nyumbani ama akitoka kulima apate maji. Hata mtoto anatoka shule anafika nyumbani anakuta mama hana chakula, hajapika ni kwa sababu ya ukosefu wa maji. Naomba sana tena sana kwa sababu kila mwanamke anaesimama hapa au mwanaume anaongelea hivo hivo kuhusu maji. Mheshimiwa Naibu Waziri sehemu ya Bukoba Mkoa mzima wa Kagera nimekutajia Mito ambayo inaweza ika-supply Mkoa mzima watu wote wakapata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunakaa kusubiri bajeti ya Serikali na bajeti ya Serikali kwenye kitabu hamna, tunasubiri wahisani. Mtu akija kwako kukutembelea au kuja kwenye harusi yako akakuta wewe huimbi na yeye hawezi kuimba, sasa hao wahisani watakuwa wanatoa pesa mpaka lini? Wanakuta sisi hatukutenga pesa yeye mwenye anakuja kujitolea pesa, watachoka kutusaidia kama sasa hivi wanavyoendelea kuchoka katika kutuwezesha kwa angalau watuwekee bajeti kidogo ya kutusaidia sisi ili tuweze kupata hata mabwawa. Kila siku tukisimama hapa mnasema wahisani, kila tukifanya hivi mna sema wafadhili, kwa nini Serikali yetu isiwe inaona kitu cha muhimu?

Mheshimiwa Naibu Spika, mnaanza kupanga miradi mipya, nimeona kwenye kitabu mna miradi mipya, kwa nini msimalize miradi ya zamani? Angalau mkasema Mkoa wa Kagera tunafanya hapa na Mkoa huu tunafanya hapa. Maliza miradi ya zamani ili msiwe na viporo kwa kuzidi kuongeza miradi mipya, itatusababisha kila siku tusimame hapa. Amesema Mheshimiwa Mnyika hata na mzee akizeeka anakaa chini mtoto anakimbia. Kwa hiyo, tunaomba CCM tuwasaidie huu mzigo umewachosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana tena sana, kilimo ni uti wa mgongo na kilimo tusitegemee msimu wa mvua. Hata mvua kama ya sasa hivi si inanyesha sana, kipindi kilichopita umetokea ukame mkubwa sana na mahindi yamekauka na maharage yamekauka, lakini sasa hivi maji ni mengi unayaona yamejaa tu, yatakauka tuendelee kulia tena na maji. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, tafuta wafadhili waweze kutusaidia kuvuna maji ya kilimo tupate kilimo cha umwagiliaji ili tupate chakula cha kutosha, mboga za kutosha na akina mama waweze kupata biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tupo karibu na Uganda, akina mama wakiwa wamelima kilimo cha umwagiliaji tunaweza kuuza mboga sehemu mbalimbali. Kwa sababu ukiangalia ndizi zetu wanatoa Bukoba, Karagwe na Ngara wanapeleka Uganda. Ndizi hizo hizo za Mkoa wa Kagera zinasafirishwa kwenda nje lakini sisi wenyewe hatuna mahali hata pa kuuza. Kama tukiwa na mboga kama hizo watu wanakuja wananunua na akina mama hawawezi wakalilia, hata ukimwambia mama changia mradi wa maji hatakataa kuchangia kwa sababu najua matatizo anayoyapata. Akina mama wanachangia harusi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nasikia wanasema tuongeze tozo kwenye mafuta, sasa tutakuwa tunaongeza kila siku kama bajeti inakwenda kuongezwa kwenye vinjwaji.

Kila bajeti inayokuja wanaongeza kwenye vinywaji, vinywaji itakuwa kama hii hii ya kuongeza mafuta unaongeza kiasi fulani kwenye mafuta, tusiongeze hapo. Tutafute vitu vingine vya kubuni ili tuweze kupata na sisi watu wa kutusaidia au mradi wa maji uweze kupata na vyanzo vya majiā€¦(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwijage muda wako umekwisha.

MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani.