Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Baada ya sauti hiyo kutoka Bunda sasa ni sauti ya mahaba kutoka Tanga, mubashara kabisa kule ambako mahaba yamezaliwa. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi napongeza kwanza Mawaziri wa Wizara hii, ni Mawaziri wasikivu sana. Kwa kweli nafarijika hata Mheshimiwa Ester Bulaya amemuita ni mzee wa site, kweli huyu ni mzee wa site. Mheshimiwa Naibu Waziri hata anapojibu maswali yetu hapa ndani anajibu kwa data na kwa uhakika. Kwa hiyo, tunawapongeza sana pamoja na changamoto hii ya upungufu wa bajeti katika Wizara yao, niwaombe Waheshimiwa Wabunge tulijadili jambo hili kwa umakini mkubwa, tutafute namna ya kupata vyanzo vya kuwawezesha hawa majembe wakahakikishe kwamba ile dhana ya kumtua mama ndoo kichwani inakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri amefika katika Jimbo la Mlalo lakini pia Jimbo la Lushoto katika Halmashauri ya Lushoto. Ninaomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri amepata wokovu na jiko lake linatoka Mkoa wa Tanga. Kwa hiyo, huyu ni shemeji yetu na ndiyo maana hii kazi unaona anaifanya ni kwa sababu ana mtunzaji mzuri kule nyumbani. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale katika Kata ya Manolo ule mradi wa vijiji 10 ulitoa ahadi kwamba ukamilike kabla ya Juni 30, nataka nikuhakikishie kwamba matenki yameshajengwa lakini bado hatua ya usambazaji wa mabomba inasuasua. Hii ni sambamba na kule Lushoto katika mradi ule wa Ngulu, kata ya Kwemashai, nao unasuasua, mkandarasi bado hajaanza hatua ya usambazaji wa mabomba. Kwa hiyo, nikuombe shemeji yangu ujitahidi kabisa kwamba ahadi uliyoiweka ya Juni 30 kwamba miradi hii iwe imekamilika, ahadi hiyo uitekeleze.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunayo miradi mingi, ile miradi ya maji ya mwaka 1972. Tunao mradi wa kata ya Mng’aro, kata ya Mbaramo, kata ya Rangwi, kata ya Lukozi na kata ya Malindi. Hii miradi ni ya mwaka 1972 imeshakuwa ni miradi chakavu na watu wameongezeka sana katika maeneo haya. Vyanzo vya maji vimezidi kupungua hasa kutokana na mabadiliko haya ya tabianchi, kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla kwamba miradi hii twende tukaiboreshe. Tutakapoiboresha katika hatua hizi za awali itatusaidia kwamba hatutakuwa na gharama kubwa ya kuandaa tena miradi mikubwa ya vijiji kumi kumi. Kwa hiyo, niombe sana kwa kuwa miradi hii haigharimu pesa nyingi sana ni vizuri tukaitekeleza wakati huu ambapo bado haijawa na mahitaji makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni pamoja na mradi ule wa kata ya Mlola katika Jimbo la Lushoto, nao ule ni mradi wa siku nyingi, mkandarasi alikuwepo site muda mrefu, lakini haupigi hatua. Niwaombe tuchukue jitihada za makusudi ili dhana hii ya kumtua mama ndoo kichwani iweze kutimia kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala zima la umwagiliaji. Katika Hosea 4, aya ya sita, anazungumzia watu wangu wanateketea kwa kukosa maarifa na anasema wazi kwamba kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa nami nitakukataa.

Katika Halmashauri ya Lushoto na Wilaya ya Lushoto kwa ujumla na Milima ya Usambara tunatiririsha maji mengi sana ambayo yanapotea tu na kuelekea baharini. Hata sasa tunavyozungumza tuna wimbi kubwa la mafuriko katika Mji wa Korogwe eneo la Mkumbara, lakini maji haya yote yanatoka katika Milima ya Usambara. Yapo makorongo mengi yanayoshusha maji na maji haya yanapotea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niiombe Wizara, hatuwezi tukawa na kilimo endelevu bila kuwa na skimu za kilimo. Nimeona hapa katika ukurasa wa 87 mmetaja baadhi ya skimu za kilimo kwa ajili ya kilimo cha mpunga, lakini kule kwangu kuna skimu ile ya Mnazi ambayo tumeizungumza sana Mheshimiwa Waziri, ambayo pia inakwenda kusaidia na kata jirani za majimbo ya Same Mashariki na Same Magharibi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nikuombe sana kwa pale Mnazi ambapo tulikusudia tujenge mabwawa kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji. Vilevile ukumbuke katika Wilaya ya Lushoto hili ndilo eneo pekee ambalo lina wafugaji, wenzetu hawa Wamasai. Kwa hiyo, tulikubaliana kabisa kwamba eneo hili tupate bwawa kwa ajili ya kutunza maji kwa ajili ya shughuli za kilimo, lakini pia maji haya yasaidie kunywesha mifugo, kwa sababu katika kata tatu za Jimbo la Lushoto ambazo ni tambarare ni pamoja na eneo hili ambalo ninalizungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunakusudia kwamba yatakapopatikana mabwawa katika eneo hili yatasaidia kutatua pia tatizo la wafugaji kuingiza mifugo katika Hifadhi ya Mkomazi na ndiyo maana nasema watu wangu wanateketea kwa sababu ya kukosa maarifa. Kwa hiyo sasa sisi tutumie maarifa haya ili kutatua kero hizi za wafugaji kuingiza mifugo katika hifadhi, lakini tutatue kero hizi za kuacha maji yakiwa yanapotea bila kuwa na matumizi yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi naomba nipendekeze eneo ambalo Wizara hii inaweza ikapata fedha, wenzangu wengi wamezungumzia kuongeza tozo katika tozo ile ya mafuta, mimi naunga mkono sina tatizo na hilo, lakini hivyo bado kuna eneo la simu. Mitandao ya simu hii wakati mwingine inatumika vibaya nadhani kwa sababu labda hatujasimamia hili eneo vizuri. Ni eneo ambalo na lenyewe tunaweza tukaja na wazo zuri tukapata tozo kiasi kutoka kwenye mitandao ya simu ili likaweze kutunisha mfuko wetu huu wa maji vijijini. Kwa hiyo niombe sana Wizara ya Fedha ijaribu kuliangalia hili tuone namna gani tunaweza tukapata chochote katika mifuko hii ya simu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA) huwa wanachukua asilimia katika Mamlaka za Maji lakini pia wanachukua asilimia tatu nadhani katika bili za TANESCO. Pesa hizi zingewekewa ukomo kwamba labda asilimia 40 ya pesa hizo wanazozikusanya kutoka mamlaka za maji na kwenye madini pamoja na TANESCO angalau asilimia 40 iingie katika mfuko huu wa maji ili kwenda kutunisha mfuko wa maji na kumtua mama ndoo kichwani kama ambavyo ilani inatuelekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la maji ni suala ambalo kwa kweli ni jambo kubwa sana ambalo ni ahadi ya ilani na wote hapa hakuna Mbunge ambaye hajaahidi. Kwa hiyo ninaiomba sana Wizara izingatie hilo. Ninaomba kuunga mkono hoja kwa asilimia 100. Ahsante sana, nashukuru sana.