Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia Wizara hii nyeti, Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa mimi binafsi nianze kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, niwashukuru Mawaziri wote, lakini hususan Waziri wa Maji. Sisi kwa Mkoa wa Tabora kwa kweli tunawashukuru sana. Mheshimiwa Rais alivyokuja Tabora kwenye kampeni alituahidi atatuwekea maji ya Ziwa Victoria. Lakini mpaka ninavyosema hivi tumeshazindua na mkataba umeshafanyika wa maji Ziwa Victoria na maji haya yataenda karibia eneo kubwa sana la Mkoa wa Tabora. Kwa hiyo, tunaishukuru sana Serikali, tunaishukuru Wizara na nimeongea na Mheshimiwa Waziri amesema muda mfupi watakuja kufanya uzinduzi Tabora tayari kwa kuanza kujengwa kwa mradi huu mkubwa ambao utamtua mwanamke ndoo ya maji kwa asilimia 90. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile niishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kutuletea mradi mkubwa wa JICA wa bilioni 29. Mradi huu umetusaidia Mkoa mzima, niweke tu sawa tu Hansard siwezi ku-attack Mbunge mwenzangu. Jana Mheshimiwa Sakaya alisema mradi huu umegusa Wilaya moja ya Uyui, si kweli; mradi huu umegusa Mkoa mzima wa Tabora. Mradi huu Wilaya ya Tabora Manispaa umeenda Kakolo kwa maana ya bomba, umeenda Mabama - Uyui, Kizengi - Uyui, Nzega kwa maana ya mabomba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mradi huu umechimba visima 101 Kaliua kwake Mheshimiwa Magdalena Sakaya visima vipo, Urambo, Sikonge na Mkoa mzima wa Tabora. Kwa hiyo, niweke Hansard sawa Mradi wa JICA umepita Mkoa mzima wa Tabora na si tu Wilaya moja kama ilivyosemwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema hayo machache naendelea kuipongeza Serikali, lakini changamoto hazikosi. Tunaiomba Serikali sasa wakati ikituletea maji ndani ya Tabora Manispaa maji haya sasa yatoke Tabora Manispaa kwenda Sikonge awamu ya pili. Vilevile hatukuwa na mpango wa kuyatoa maji haya ya Ziwa Victoria Tabora kuyapeleka Urambo, mimi nadhani tuweke mpango huu wa kupeleka Urambo. Najua Urambo kuna mkakati mkubwa wa Malagarasi kwa kupitia Kaliua na kwenda Urambo. Hata hivyo Mheshimiwa Waziri hili jambo ni kubwa, Malagarasi ipo mbali sana na Urambo na Kaliua, litachukua muda mrefu. Nikuombe Mheshimiwa Waziri kwenye mipango yako uweke maji ya Ziwa Victoria yaende Urambo, ni kilometa 90 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama mtayapeleka Igalula baadaye mkija kuyapeleka Urambo nadhani ni rahisi zaidi kuliko kupigana na Malagarasi kwa sasa. Ila mradi wa Malagarasi uendelee kama mlivyokuwa mmeupanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine kubwa ambayo tunayo watu wa Tabora Manispaa ni water table ambayo iko juu. Serikali imetuletea maji mengi sasa, kwa hiyo niwaombe Serikali itupatie pesa tulizoomba shilingi bilioni 14 kwa ajili ya mabomba ya maji taka. Tumeomba shilingi bilioni 14 tupate mabomba ya maji taka ili tuweze kupitisha maji taka, maji yasiwe mengi ili kuepuka magonjwa ya milipuko yatakayokuja baada ya kupata hayo maji mengi ya Ziwa Victoria.

Sasa hivi tuna mtandao wa mabomba ya maji taka kwenye kata mbili tu Ngongoni na Bachu Kidogo, huko kote hakuna mtandao wa maji taka. Kwa hiyo, tunaomba Serikali itupatie mtandao wa maji taka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ni madeni, Idara ya Maji inadai madeni makubwa sana. juzi nikiwa Tabora tarehe 28 mpaka tarehe 3 tulikatiwa maji, nikaenda Mamlaka ya Maji kuuliza tatizo ni nini? Wakaniambia tumekatiwa umeme tunadaiwa shilingi milioni 500 za umeme na TANESCO. Lakini TUWASA Tabora inadai shilingi bilioni tatu; ambapo Jeshi linadaiwa shilingi bilioni mbili, Kitete Hospitali ya Mkoa na inadai Polisi na Magereza hawawalipi pesa zao. Sasa hii taasisi itaendeshwaje kama taasisi hii ya TUWASA tu Tabora inadai shilingi bilioni tatu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali ije na mpango mkakati mwingine. Mimi nimefanya kazi Halmashauri, tulikuwa tunakatwa LAPF na nini, lakini hela haziendi sehemu husika. Serikali ikaamua madeni yote yale yatoke Hazina moja kwa moja yapelekwe sehemu husika. Kwa hiyo, mimi naomba Serikali yangu iamue sasa madeni yote ya hizi Mamlaka za Maji, ya Jeshi na nini bajeti zao za maji zikatwe moja kwa moja na Hazina zipelekwe zikalipe maji ili na wananchi wengine waweze kufaidika na haya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumekatiwa maji Tabora nzima kwa sababu tu kuna taasisi za Serikali zinagaiwa. TANESCO wakakata umeme wao, kwa hiyo, sisi watu wa Tabora wote tukakosa maji kwa sababu watu wanadaiwa madeni makubwa ambao ni Taasisi za Serikali. Naomba Serikali ije na mpango mkakati otherwise watu watakosa maji wakati Serikali imeshayaleta maji mpaka sehemu husika. Nawaombeni sana Serikali mliangalie hili suala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naenda moja kwa moja kwenye bajeti. Naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuhusu suala suala la tozo na mimi naiomba Serikali yangu iongeze shilingi 50 kwenye Mfuko wa Maji ili kupata shilingi 100. Lakini napingana na watu wanaosema kwamba tuikatae bajeti au tuibadilishe bajeti kwa sababu ukiangalia Kanuni ya 105 kwa kuokoa muda sitaisoma inasema kwamba sisi Wabunge kwa ushauri wetu Kamati hii inaweza ikarudi kwenye Budget Committee, ikakaa upya na ikaangalia taratibu je, hizi tozo tukiongeza kuna tatizo gani? Kama kuna tatizo basi labda tupunguze REA au tupunguze kwenye Mfuko wa Barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuwape muda Serikali wakakae kwenye Budget Committee wafanye hii kazi, lakini tukisema humu ndani tunaikataa bajeti hakuna tutakachokuwa tumekifanya ndugu zangu. Tusikubali kabisa kukataa bajeti, kanuni inatuelekeza kwamba tuna uwezo wa kuirudisha Serikali ikakaa tena upya na wakaja kwenye Kamati ya Bajeti wakati wa hotuba ya bajeti wakatuletea wameonaje na wamefikiriaje. Nawaomba sana ndugu zangu bajeti hii isirudishwe, isipokuwa warudi kwenye Budget Committee wakakae upya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu naomba niongelee kidogo, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC, nilipata bahati ya kwenda kukagua DAWASCO Dar es salaam. Nilikuta vitu vya ajabu kweli na vikashangaza na nikaona kweli Serikali yangu sasa iko kazini na inafanya kazi na inadhibiti hizi taasisi za Serikali. Wakati tumekwenda tumesomewa ile taarifa wakati huyu CEO aliyepo sasa hivi anaingia alikuta DAWASCO haina chochote hata senti tano, lakini alikuta deni la shilingi bilioni 28 la PPF, shilingi bilioni 16 la TRA, watumishi shilingi bilioni tano na alikuta upotevu wa maji asilimia 56 lakini alijitahidi kufanya kazi mpaka sasa hawadaiwi hata senti tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, fikiria hii ni mwaka 2017 ameingia mwaka 2015 mwishoni, hakuna deni hata moja; tunajiuliza kipindi kile hizi hela zilikuwa zinakwenda wapi mpaka madeni yakawa makubwa kiasi hiki? Kwa hiyo, naamini kabisa Mheshimiwa Waziri wa Maji hii kazi unaifanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Waziri nilikuwa na ushauri mmoja; DAWASCO inakusanya shilingi bilioni tisa kwa mwezi lakini inatoa asilimia 23 sawa na bilioni mbili inapeleka DUWASA.

Sasa mimi najiuliza hizi bilioni mbili DUWASA za nini? Wakasema sijui kwa sababu maji yanalipiwa umeme na umeme unalipwa na DAWASCO, service ya mitambo inafanywa na DAWASCO, lakini DUWASA ina watumishi 68 na hawa watumishi 68 wanapelekewa shilingi bilioni mbili kila mwezi, kwanini DUWASA na DAWASCO visiunganishwe kama tulivyofanya TRL na RAHCO? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.