Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mungu kwa kunipa afya njema na kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu. Nitaanza na suala la utamaduni katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, lugha ya Kiswahili inapewa kipaumbele cha juu katika nchi yetu, ni jambo jema. Ila napenda kuonesha hisia zangu katika Wizara hii kwa mustakabali wa Taifa hili kwa kuwa lugha ya Kiingereza imekuwa ikitumika maeneo mengi katika Serikali yetu, mfano interviews za kuomba kazi hufanywa kwa lugha ya Kiingereza, hotuba na mawasiliano mengi hufanywa kwa lugha ya Kiingereza, ukienda kwenye suala la biashara za kimataifa kati ya nchi na nchi kwa wafanyabiashara wetu na wa nje hufanywa kwa lugha ya Kiingereza.

Mheshimiwa Spika, kwa ushauri wangu ningeomba pamoja na kutumia Kiswahili, bado nchi yetu haijaweza kujitegemea kama nchi za Kichina wanavyoweza kutumia lugha yao ya ndani. Hivyo basi, kwa kuwa bado tunategemeana na nchi nyingine kiuchumi, bado tunahitaji kufundisha lugha za Kiswahili na Kiingereza katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, michezo; kwa kutambua umuhimu wa michezo katika Taifa letu, kuwa michezo ni afya, ajira, mahusiano na pia kutangaza Taifa letu kitalii, bado tuko nyuma sana kwa kutumia michezo yetu kwa manufaa ya Taifa hili. Nashauri Wizara kuwa na Sports Academy kila kanda kwa nchi yetu ili kuweza kuinua vipaji vya vijana wetu mpaka kwenye ngazi za chini.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze wadau mbalimbali kwa kutumia michezo kupeleka ujumbe wa jamii, lakini kama Wizara, tunaomba michezo itumike vizuri katika kuitangaza nchi yetu lakini pia kupinga vitendo mbalimbali vya kurudisha nyuma maendeleo ya nchi, mfano, kupinga ujangili wa tembo kupitia michezo, kupinga utumiaji wa dawa za kulevya na kupinga ndoa za utotoni na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, michezo kupitia utalii. Michezo ni kiunganishi kikubwa cha nchi na nchi kupitia vivutio vya utalii wetu. Nasema hivyo kwa sababu leo ukitaja Timu ya Arsenal unataja nchi ya Uingereza. Kwa Taifa letu bado hatujafika kuwa na Timu ya Taifa ambayo inaweza kuitangaza nchi yetu kiutalii. Hata Serengeti Boys ambayo inabeba jina kubwa la Hifadhi ya Serengeti, haijaweza kutangaza hifadhi yetu hata kwa hadhi ya nchi za Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, naomba kushauri Wizara kuwasaidia vijana wenye vipaji vya michezo ili kuitangaza nchi yetu. Limekuwa ni jambo la kawaida kuona mchezaji amejitahidi na kufika kiwango kikubwa ndiyo Wizara inamtambua. Nashauri vipaji vya vijana wetu vianzie shule za msingi ili waweze kusaidiwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni nimehudhuria Kilimanjaro Marathon, Mkoa wa Kilimanjaro na nilikimbia mbio za kilometa tano, kilichoniumiza ni kuona washindi waliopatikana ni kutoka nchi ya jirani ya Kenya. Hii inanipa tabu sana hata kutangaza Mlima Kilimanjaro kupitia mashindano hayo muhimu.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali kupitia Wizara ijifunze kuanzisha mashindano kama haya ambayo kwa sasa yanafanywa na wadau ili kuweza kuandaa vijana wetu mapema, hasa kutumia Jeshi letu ambalo pia lina nidhamu na vijana wengi. Vilevile, kama tunavyojua michezo ni ajira, tunaweza kuajiri vijana wengi kupitia michezo. Hii itarudisha nidhamu ya michezo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, taasisi nyingi za Serikali ziliajiri wanamichezo wengi kuwa watumishi, mfano mzuri ni TANAPA, iliajiri watumishi wengi wanamichezo.