Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi hii leo ya kuweza na mimi kuchangia.
Awali ya yote, nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu, Subhanahu Wataala, aliyenijalia uwezo na satwa ya leo kuwa mimi Asha Abdullah Juma kuwa Mbunge na kuweza kuchangia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi ya kwanza kabisa kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuweza kuwa Rais na kuongoza kwa speed hii ambayo anakwenda nayo, kwa kweli anafanya kazi nzuri sana.
Vilevile nachukua nafasi ya kipekee kupongeza hatua iliyochukuliwa na chama chetu ya kuweza kumpendekeza Mheshimiwa Samia Sukuhu Hassan akawa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Napongeza pia uteuzi wa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, anao uwezo wa hali ya juu sana na anakubalika na tuna matumaini atafanya kazi nzuri sana. Niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote mliopata nafasi hii, nawapongeza pia wale waliopata nafasi ya Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi ya kipekee kabisa nampongeza Mheshimi Dkt. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar na kwa kushinda uchaguzi. Mheshimiwa Ally Saleh nakuona hapo, nakuambia kwamba Mheshimiwa Dkt. Shein ndiyo Rais wa Zanzibar na amechagua cabinet nzuri naamini itamsaidia kufanya kazi nzuri. (Makofi)
Kwa kupitia Bunge hili, nilaani kitendo alichofanyiwa Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein cha kuzomewa lakini lile halikumrudisha nyuma yeye ameendelea kuwa Rais wa Zanzibar kwa kura nyingi na sisi tunamuunga mkono kwa sababu ndiye tegemeo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kitu kimoja, hii tabia ya kususasusa si nzuri, tabia ambayo inaoneshwa hapa kwa sababu inavunja demokrasia.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Anajijua mwenyewe aliyesusa. Inavunja demokrasia, watu wamewachagua mje hapa muwawakilishe, muisemee Serikali au muikosoe, mnakuja hapa kisingizio hiki, kile, mara kutoka nje, mara uzomee, mara unune, mara ugome, sasa ndiyo umechaguliwa kwa ajili hiyo? Ilimradi hakuna lililo zuri kwa upande wenu. Usichukue mshahara wa kutwa bila kufanya kazi ya kutwa.
Baniani mbaya ila kiatu chake dawa. Mshahara, posho yote mazuri mbona hamyakatai?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Asha…
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya dibaji hiyo, sasa niende kwenye hoja.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Asha naomba ukae.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja ya Waziri Mkuu mia juu ya mia.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba pia unilindie muda wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuchangia kwanza kwa kupongeza safu nzima ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba niseme kwamba kwenye Ofisi yako ukianzia na Mheshimiwa Jenista Mhagama, Naibu Mawaziri Mheshimiwa Dkt. Abdallah Possi na Mheshimiwa Anthony Mavunde, hawa ni vifaa, tumewapima kupitia Kamati yetu ya Katiba, wanafanya kazi nzuri sana. Naamini watatusaidia sana kwa maendeleo husika katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nianze rasmi na naanza na eneo la Tume ya Uchaguzi. Naanza kwa kupongeza kazi nzuri iliyofanywa na Tume ya Uchaguzi kuanzia Mwenyekiti wake Jaji Lubuva…
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Kailima na Jecha pia. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tume hii ya Uchaguzi imethibitisha demokrasia, kama tulivyoona vyama 22 vimeshiriki na vimeshinda vingine na sasa hivi tupo hapa kuwawakilisha wenzetu. Hivyo, ukipata wapiga kura waliofikia 15,596,110 sawasawa na 67.3% ni hatua nzuri. Tuiombe Serikali iiongezee Tume ya Uchaguzi nguvu ili kudhibiti wizi wizi na vitendo vya kuivurugia kazi Tume hii ambayo inafanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo nataka kuligusia ni hili linalohusu vijana ambalo kwenye hotuba hii limezungumzwa vizuri la kuwapatia mafunzo. Tunajua vijana wanatuzidi kwa namba, ni wengi, kwa hiyo inahitajika mikakati na imara zaidi ya kuwahusisha ili wasitutoke wakawa kundi la wanaofanya vurugu na fujo. Kwa hiyo, mipango hii iliyopangwa nafikiri ingekuwa vizuri pia ikaelezwa waziwazi kila Wilaya watapata mafunzo kiasi gani na mafunzo gani ili kujua hawa watu wanashughulikiwa ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nalotaka kuligusia ni hili la bandari. Tumeridhishwa na mpango ulioelezwa hapa lakini tuongeze kuoneshwa kwamba kunaongezwa vifaa vya kisasa zaidi ili kuharakisha upakizi na upakuaji na pia kudhibiti bila kutumia nguvu zaidi na pesa nyingi huu uvujaji na wizi katika bandari zetu. Pia nadhani kama ingekuwa vizuri kwenye eneo hili la bandari kukaimarishwa masuala ya uokoaji inapotekea disaster katika maeneo ya bandarini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jicho pia liongezwe katika kuimarisha bandari ya Mtwara na Tanga. Naona kama hii mipango iliyopangwa haijatosha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali hii ione umuhimu huo na hasa kwa vile kule Mtwara tuna mategemeo ya kupata shughuli nyingi za kupokea na kusafirisha mizigo. Kwa hiyo, ni vyema jitihada ikaongezwa kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine la muhimu kabisa ambalo linatakiwa lipewe nguvu ya ziada ni elimu. Pongezi pia kwa Serikali kwa kuweza kuboresha elimu ya awali. Naomba tuendelee kuunga mkono juhudi hizi, kama tulivyofanya kwa kutenga pesa tukaziweka kwenye madawati hivyo na kila anavyofikiria mtu kuna namna nyingine ya kufanya ili kuweza kuiboresha elimu hii basi na tufanye.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.