Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kuchangia hoja hii. Kwanza nianze kwa kutoa pole nyingi sana kwa wananchi Mkoa wa Arusha, kwa Watanzania wote, kwa walimu wote wa shule ya Lucky Vincent, mmiliki wa shule, wazazi waliopoteza watoto wetu wapendwa, nawaombea Mungu awape ujasiri wa kukabiliana na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nichangie Wizara hii kwa mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nilikuwa naomba kuelewa kwenye Halmashauri zetu kuna Afisa Michezo na Afisa Utamaduni. Sasa nilikuwa naomba kujua hawa watu huwa wanawajibika kwa nani? Mwajiri wao anakuwa ni Wizara ya Utamaduni au anakuwa ameajiriwa pale Halmashauri? Kazi zao zinakuwa ni zipi, kwa sababu ukiangalia kwenye michezo; michezo ndiyo hiyo imedorora mashuleni. Ukingalia pia kwenye utamaduni, utamaduni ni huo nao umedorora mashuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka miaka ya nyuma wakati sisi tunasoma, sisi tuliosoma zamani, kulikuwa na mashindano ya michezo. Unakuta zinakusanywa shule za primary za Wilaya hiyo zinashindanishwa na shule moja inaibuka inakuwa mshindi, inapewa zawadi ya kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kwenye suala la utamaduni, kulikuwa na mashindano; shule za primary zinashindana ngoma za utamaduni na shule moja inaibuka mshindi wa utamaduni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia katika kuimba kulikuwa na mashindano. Kwenye utamaduni walikuwa wanaweka mashindano ya nyimbo, ngoma, wanaimba ngoma za makabila tofauti na nyimbo zinatungwa zenye maudhui ya nchi hii ambazo zingekuwa na mafundisho. Wakati ule sisi ilikuwa ni mambo ya siasa za ujamaa, kwa hiyo, wanaimba nyimbo za ujamaa ambayo pia zilisaidia kuwajenga watoto mashuleni na kutujenga sisi pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vitu kama hivyo sasa hivi sivioni. Kwa hiyo, huwa inaniwia vigumu, halafu unapoenda kwenye Wilaya unashindwa kujua kazi za Afisa Utamaduni na Afisa Michezo aliyeko Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, wengi mtakumbuka, michezo imeibuliwa kule mashuleni, mimi ninao mfano wa watu ambao waliiwakilisha nchi hii nje ya Tanzania na wakailetea medali. Mwinga Mwanjala ni mchezaji ambaye aliibuliwa toka primary school na akaenda akaiwakilisha nchi hii, akaleta medali. Nzaeli Kyomo aliibuliwa toka secondary school, akina Gania Mboma wote hao waliibuliwa toka mashuleni na wakaweza kuiletea medali nchi hii na wakailetea heshima nchi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo nilikuwa naomba na niungane na wenzangu waliotangulia, michezo irudishwe mashuleni. Wizara ya Elimu irudishe mashuleni michezo iwe kama kipindi, kama ambavyo zamani tulikuwa tuna vipindi vile vya michezo. Pia viwanja vya michezo vijengwe vingi kwenye mashule. Shule inapoanzishwa wahakikishe kwamba ina kiwanja cha michezo; aidha iwe ni Shule ya secondary, primary kwa Shule za binafsi au Serikali viwanja vya michezo viwepo pale; iwe ni condition moja ya kuanzisha hiyo shule ili kuibua hivyo vipaji. Kwa sababu naona wachangiaji mnasema kwamba hatuna wawakilishi, mnaongea mambo ya mpira ya miguu kwamba Tanzania inakosa kwenda kucheza michezo ya kuiwakilisha nchi labda kwenye Kombe la Dunia au Kombe la Afrika, lakini ni kwa sababu tumeshindwa kuibua vipaji vya watoto ambavyo vinapatikana kwenye shule zetu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye utamaduni. Naomba nizungumzie suala la utamaduni; katika kitu ambacho mtu unaweza ukapoteza heshima yako ni kukosa utamaduni wa nchi yako au kabila lako.

Mheshimjiwa Spika, naomba hizi nyumba za makumbusho ambazo zimejengwa kule Dar es Salaam na moja iko kule Arusha, labda na Mwanza wanayo, naomba Wizara hii izingatie, hizi nyumba za makumbusho zijengwe kila Mkoa. Ninaamini kwamba kila Mkoa una utamaduni wake na kila Mkoa una makabila ambayo yalikuwepo kwenye huo Mkoa tangu wakati huo, ambao wana mila zao na vitu vyao vya zamani ambavyo walivitumia. Hivyo vitu vingeweza kuhifadhiwa kwenye nyumba za makumbusho za kila Mkoa ili iwe faida kwa kizazi kilichopo na kizazi kinachokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata kama sisi tutakuwa tumepotea, lakini pale mkoani watoto wataweza kwenda kutembelea kwenye zile nyumba za makumbusho na kuona vitu ambayo vilitumika zamani na wazazi wao. Kwa sababu mimi naamini kwamba mkataa kwao ni mtumwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata Uingereza wameweza ku- maintain vitu vyao vya asili na sehemu zao za asili ambazo zilikuwa zinatumika tangu enzi za King George. Unakuta yale maeneo yao ya asili yapo mpaka leo yanatumika kama makumbusho na wanakwenda ku-visit.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba hayo maeneo, kila Mkoa utenge sehemu ambayo watajenga nyumba ya makumbusho ambayo watahifadhi vitu vya makabila ya Mkoa huo kwenye nyumba hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwenye suala la mchaka mchaka. Nilikuwa naomba Wizara ya Elimu ishirikiane na Wizara ya Michezo mchaka mchaka urudi mashuleni. Sisi wakati tunasoma, tulikuwa tunakimbia mchaka mchaka asubuhi. Ni kiasi kwamba watoto wanapofika pale shuleni kabla hawajaingia darasani, wakimbie mchaka mchaka, wazunguke hata eneo la shule ili wawe wakakamavu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tulivyoona, Mheshimiwa Makamu wa Rais amesema kwamba watu wafanye mazoezi. Sasa kwa nini hayo mazoezi yasianzie kwenye shule zetu? Maana yake tunahimiza watu wazima wafanye mazoezi kama anavyosema Makamu wa Rais, basi na pia na mashuleni tuwahimize watoto wakimbie kabla hawajaingia madarasani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, nilikuwa naomba kuwe na paredi mashuleni, watoto wafundishwe kuimba Wimbo wa Taifa. Ni aibu unamkuta mtoto anamaliza Darasa la Saba hajui kuimba Wimbo wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, sisi zamani tulikuwa tunaimba Wimbo wa Taifa kabla hatujaingia darasani. Siku hizi sijui kama vitu hivyo vinatekelezwa. Ingewekwa tu kama policy kwamba watoto kabla hawajaingia darasani, waimbe Wimbo wa Taifa. Hii ni kwa faida yao, pia ni kwa faida ya nchi yetu. Sisi zamani mbona tulikuwa tunaimba Wimbo wa Taifa kabla hatujaingia darasani. Kuwe na paredi na mchaka mchaka, nilikuwa naomba nisisitizie hilo kwenye mashule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii itawapa ukakamavu na pia itawajenga kutokufikiria vitu vingine, kwa sababu mtu anakuwa amekimbia, mwili umechangamka, anapofika mle darasani ana-concetrate na shule, Ndivyo sisi tulivyolelewa. Vitu ambavyo tulilelewa ambavyo vilitusaidia sisi tunapaswa tuvipeleke kwa watoto wetu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulichangia ni kuhusu wasanii hizi kazi za wasanii waweze kupata haki zao, lakini pia usajili wa kazi za wasanii nilikuwa naomba labda wangeweka mpaka mikoani. Kwa mfano, kule kwetu Katavi, mtu atatokaje Katavi aende mpaka Dar es Salaam kwenda kusajili hiyo kazi yake? Kwanza kuna nauli, halafu kuna hizo kodi ambazo atatumia, pesa zenyewe za usajili nimesikia hapa mnachangia, sio mtalaam sana kwenye mambo ya usanii, lakini mnasema sijui shilingi 300,000 kodi sijui ya nini.

Mheshimiwa Spika, kwa kijana ambaye anaanza maisha, hiyo inakuwa ni hela ngumu sana kupata ili aweze kusajili kazi yake. Kwa hiyo, naomba ili kuwawekea unafuu, hizo ofisi za usajili za kazi za wasanii ziweze kupelekwa mpaka mikoani ili na wananchi hata na wale wasanii wangu wa kule Katavi waweze kusajili kazi zao kwa wepesi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nilikuwa naomba vitu vya zamani virudishwe. Kwa mfano, kulikuwa na zile sikukuu ambapo ilikuwa zinaweza kukutana ngoma za Mkoa huo zikashindanishwa na zikapewa zawadi. Zawadi siyo lazima iwe kubwa, lakini hii inatufanya tusipoteze utamaduni. Ndiyo maana unakuta mara nyingi mnawalaumu vijana wa sasa hivi wakitunga miziki sijui wanaimba miziki ya hip pop na nini, ile miziki wanayoiga kule ilitumiwa zamani na Waafrika weusi ambao walikuwa wanadai uhuru, ndiyo ikaja hii mambo watoto wakiimba wana-rap. Sisi tunayo miziki yetu ya asili ambayo inatutambulisha sisi kama Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, napata utata sasa hivi ninapoona kwamba hivi Mtanzania anaweza akasimama hapa akasema muziki wake wa asili ni upi? Kwa sababu naona miziki yote imechanganywa na utamaduni… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuunga mkono hoja ya Wizara ya Utamaduni.