Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami naomba nianze kwa kutoa pole sana kwa familia zote ambazo zimeguswa na msiba ambao umetokea mjini Arusha kwa kipekee kabisa. Kwa kweli msiba ule ni pigo kubwa kwa nchi yetu, na tunafahamu kwamba kuna tukio linaendelea pale Arusha tunawatakia kila la heri na kwa kweli tunawapa pole nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yupo rafiki yangu mmoja yuko Marekani jana alinipigia simu akaniuliza na nikashindwa kutoa jibu na nilikuwa nataka watu wa Kiswahili watusaidie kutafuta, inawezekana likawa ni neno jipya ambalo linaitwa “Bashite” kutafuta maana ya Kiswahili ili liwekwe kwenye Kamusi. Kwa sababu kuna wakati walioko nje wanashindwa kupata connection ya mazungumzo hayo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nianze kwanza kwa kutoa shukurani nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwanza kwa kuonesha kwamba anajali michezo, lakini pili kwa upendeleo kabisa wa kuleta uwanja mkubwa wa michezo hapa Dodoma. Mikoa mingi sana haina viwanja vizuri vya michezo na ni nafasi pekee hii katika Mkoa wa Dodoma kupata uwanja ambao unaweza ukawa ni uwanja wa pili wa Kimataifa baada ya uwanja wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, maoni yangu katika suala hili, naiomba Wizara ihakikishe kwamba uwanja huu unakuwa na vitu vingi vya lazima. Hapa tunapoongea Tanzania hata pamoja na mchango mkubwa wa wasanii wa muziki, wasanii wa ngumi na aina nyingine za michezo, tuna maeneo machache sana ya michezo ya aina hii ambayo yapo. Hatuna ukumbi wa kisasa wa muziki, hatuna ukumbi wa kisasa wa ngumi, tuna maeneo tu ambayo ni ma-hall ambayo ni ya kawaida hayawezi kuhamasisha michezo hii ya Kimataifa. Kwa hiyo kuja kwa uwanja huu niombe wale ambao wanasaidia kwenye mipango wahakikishe kwamba uwanja huu unakuwa na complex ili uweze ku-accommodate michezo mingi na ya aina mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana wanamichezo wetu wengi, nianze na under 17 ambao kipekee sasa wanaelekea Gabon kwa ajili ya michezo hiyo ya Afrika; niwatakie sana mafanikio mema.

Vilevile niwapongeze sana wachezaji wetu wa Kimataifa walioko nje ambao wanacheza mpira wa kulipwa kama Samatta, Ulimwengu na wengine, niwapongeze sana Mwanariadha Simbu, Cecilia, Ginoka, Magdalena, Emmanuel, hawa wameendelea kuiuza Tanzania kwenye ramani ya Kimataifa. Wasiwasi wangu ni mmoja tu; ni mchango wa Serikali katika kuhakikisha kwamba mafanikio haya yanaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Spika, ni bahati kubwa leo tunao akina Samatta, tunao hawa wanariadha wengine na kwa kweli kimsingi nchi hii kwa ukubwa wake na idadi yake ya watu, tungeterajia iwe na watu kama hawa zaidi ya 100.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa sasa kinachoendelea ni kwamba anajitokeza mmoja na yeye anakuwa kama wa dawa. Hii maana yake ni kwamba maandalizi ya kuwapata ha watu huku chini yamekuwa ni madogo na matokeo yake kila anayechomoza anachomoka kwa bahati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwenye eneo hili, miaka ya nyuma tulipata wanamichezo wengi sana walitokea kwenye Majeshi hasa JKT, Polisi na JWTZ. Nadhani sasa Serikali inapoelekeza kwenye kuchagua vijana hawa kutoka kwenye maeneo mbalimbali kwenye Wilaya iweke kipaumbele sana katika suala la michezo ili kuwapata vijana hawa wanaopelekwa kwenye maeneo haya waweze kuandaliwa vizuri waweze kuiwakilisha nchi yetu. Ni kwa sababu tu kwamba zamani pia tulikuwa na mashirika ya umma ambayo yalikuwa yanaweza kuwa na timu hizi za michezo. Baada ya mabadiliko ya sera, mashirika haya yakabadilisha mfumo matokeo yake ni kwamba hayana tena nafasi ya kuandaa wanamichezo wengi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nadhani kwamba vyombo hivi vya dola ambayo kimsingi bado vina uwezo mkubwa wa kuwa na bajeti ya kutosha lakini na nafasi ya kuwaandaa vingeendelea.

Mheshimiwa Spika, nimeisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri na kwa kweli niseme ni hotuba nzuri sana, nampongeza yeye pamoja na Naibu wake na Katibu wake Mkuu ambaye ni Mwalimu wangu, lakini napenda kusema upungufu kidogo ambao nimeuona hapa. Kwanza nilitarajia katika taarifa hii nione kwa kina inazungumzia uongozi mbovu na migogoro mingi iliyopo TFF. Kwa sababu ni kupitia mpira nchi yetu inaweza ikatengeneza wanamichezo wengine wapya kama Samatta.

Mheshimiwa Spika, juzi hapa kabla timu ya Taifa ya Vijana haijaondoka, tulishuhudia vijana wale wanateremshwa kwenye basi kwa deni kubwa la kodi ambalo wanadaiwa TFF pamoja na TRA. Nikatarajia kuona ni namna gani sasa Wizara inaondoa aibu hii.

Mheshimiwa Spika, tuliona mwaka 2016 vyombo hivi vya mpira kama FIFA, CAF na TFF vilikuwa haviingiliwi na chombo chochote cha uchunguzi cha Serikali, lakini mwaka 2016 FIFA, FBI waliingia ndani, miaka kama kumi huko nyuma chombo cha Italia cha Usalama kiliingia ndani kuchunguza.

Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu sasa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, wakati nachangia katika ripoti yangu mwaka 2016 na hasa nilipogusia suala la rushwa katika Chama cha Mpira cha Tanzania, nilimtaka Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge na awaeleze Watanzania ni chombo gani independent ambacho kilifanya uchunguzi kama ilivyo FIFA, kama ilivyokuwa Italia na kama ilivyokuwa kwenye CAF hapa juzi, Rais mpya wa CAF alipochunguzwa kwa tuhuma za rushwa ambacho kiliihakikishia TFF kwamba sasa ilikuwa na uhalali wa kufanya maamuzi ya kuzishusha timu tatu za Majeshi ya Polisi na JWTZ, lakini pia na timu moja ya Geita Gold Sport ambayo ilishushwa daraja na kupandishwa timu nyingine kutoka nafasi ya tano kwa sababu za kuhisia.

Mheshimiwa Spika, mpaka leo tunazungumza na nimetazama sijawahi kupata hiyo taarifa, pamoja na uchunguzi huo mkubwa uliofanywa na PCCB.

Mheshimiwa Spika, niliahidiwa hapa na Mheshimiwa Waziri, kwamba baada ya uchunguzi huo wahusika watapelekwa mahakamani na hatua zitachukuliwa.

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe angalizo hapa kwa Serikali, mahakamani mara nyingi tunashindanisha maneno na inawezekana kabisa kwamba mwenye haki akakosa haki mahakamani kwa sababu ameshindwa kujenga kesi. Hii maana yake ni kwamba pamoja na uchunguzi mzuri wa PCCB na ushahidi wote waliopewa na wahusika kwamba palikuwa na harufu ya rushwa kubwa TFF, mpaka leo inavyoonekana wale watu ambao walituhumiwa na ushahidi wote wanaelekea kuokoka.

Mheshimiwa Spika, nataka tu nipate ushauri wa Mheshimiwa Waziri, ni kwa namna gani, ameitaja TFF, amezungumzia namna ambavyo anafikiria itaweza kusimamia michezo, lakini hajasema ni kwa namna gani anafikiria kuimarisha utawala bora kwenye TFF? Tunafahamu kwamba kwa mujibu wa sera, hizi ni taasisi ambazo zinajiendesha zenyewe, lakini kimsingi kama kuna rushwa, kama maamuzi yanayofanyika pale siyo ya haki, inakatisha tamaa wadau wa michezo.

Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza, leo ni mwaka mmoja na nusu tangu Geita Gold Sport walipoomba review ya kesi yao baada ya kukata rufaa, TFF hawajawahi kutoa maamuzi wala hawajawahi kusema rushwa alitoa nani? Alipewa nani? Shilingi ngapi? Wameishia kwenda kumfungia mchezaji miaka kumi, wamemfungia kocha miaka kumi ambaye haijulikani pesa alitoa wapi, kwa sababu viongozi wake wote wanaonekana hawana hatia.

Mheshimiwa Spika, nilitaka pia Mheshimiwa Waziri aje atuambie hapa, inapotokea suala kama hili, ni nini hasa nafasi ya Serikali? Kwa sababu tukiruhusu hali hii kuendelea tutafika mahali tutajikuta kwamba michezo ambayo inasemekana ni ajira haiwezi kuwa ajira tena. Wapo Watanzania wengi ambao sasa hivi wanafikiria wafike level ya Samatta, lakini kwa kukatishwa tamaa na matukio yanayoendelea katika TFF unaweza ukajikuta kwamba baadaye watu wote wanaona ni bora waachane na michezo wafanye kitu kingine.

Mheshimiwa Spika, nimelisema hili kwa muda mwingi kwa sababu ni suala ambalo linaigusa timu ya Geita Gold Sport ambayo ni timu inatoka Geita, ambapo wananchi wa Geita waliipandisha kwa gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nilikuwa nataka kusema, pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Rais kuhusu kiwanja cha michezo, tumeona kwenye bajeti hii, lakini pia bajeti ya TAMISEMI, ni sehemu ndogo sana ya pesa ambayo inaelekezwa kwenye kuimarisha michezo. Kule kwetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.