Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaitwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Wilaya ya Kibiti. Kwanza nikupe hongera kwamba umedhihirisha kwamba katika Bunge hili wewe kweli ni Mtemi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi kuwashukuru wananchi wangu wa Kibiti, na niwaahidi kwamba nitawapa ushirikiano kwa kila linaloleta maendele kwani hiyo ndiyo kiu ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hoja ya Mheshimiwa Magufuli Rais wa nchi hii, ni kipenzi wa nchi hii, kama ifuatavyo na nitaanza na ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mizunguko yake Mheshimiwa Rais yamekuwepo malalamiko mengi katika ardhi. Ningeomba mamlaka husika katika eneo hili wachukue hatua stahiki kwa kutoa hati za ardhi kwa haraka iwezekanavyo. Kwa hiyo nafahamu kumekuwa na migogoro mingi katika sekta hiyo na ninnaomba Waziri mwenye dhamana afanye kazi yake kuhakikisha Wilaya ya Rufiji hususan Kibiti, tunapata Afisa Ardhi Mteule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kuchangia kuhusu kilimo. Tunafahamu sasa kwamba wananchi imefika wakati walime kilimo chenye tija, walime kilimo chenye manufaa kwani hayo ndiyo mahitaji ya wananchi. Kumekuwa na kero nyingi katika upatikanaji wa pembejeo za ruzuku. Ningeomba kuishauri Serikali badala ya kupeleka vocha vijijini watoe kodi ambazo hazina ulazima ili pembejeo zipatikane kwa bei rahisi katika maeneo husika. Nafahamu kumekuwa na malalamiko mengi kwamba vocha zikifika vijijini wananchi hawazipati kwa haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika migogoro ya mifugo na wafugaji. Nafahamu katika Jimbo langu kuna migogoro ya wakulima na wafugaji katika Kata ya Mtunda. Ningeomba sehemu ambayo inahusika wachukue hatua haraka iwezekanavyo. Pia ningeomba nishauri katika sehemu husika ya Kata hiyo kuundwe Kamati ya Kusuluhisha Migogoro hiyo. Tungetoa wakulima watano na wafugaji watano ili wakae kuangalia ni jinsi gani watatatua migogoro hiyo, pindi itakaposhindikana ndipo taarifa ziende kwa DC naye achukue hatua stahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba wakulima na wafugaji wanatuletea kipato katika nchi hii, lakini wafugaji naona kama wamesahaulika. Kuna kila sababu ya kuandaa ranch katika Wilaya yetu ya Kibiti na huko kwenye ranch lazima zipelekwe huduma muhimu zikiwepo majosho, vikiwemo vituo vya minada ili sehemu husika wananchi nao waone kwamba wanafaidika na ufugaji huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine niende katika uuzaji wa korosho. Suala hili limekuwa na migogoro mikubwa kwamba mkulima anakatwa kodi nyingi na vyama vya msingi kiasi kwamba mkulima wa korosho anaona hana sababu ya kwenda kulima zao hilo. Ningeshauri kwamba baadhi ya kodi ambazo siyo za lazima zitolewe katika zao hilo la korosho.
Sehemu nyingine ambayo ningependa kuchangia ni katika huduma ya afya. Nafahamu kwamba Wizara husika imejipanga kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati katika vituo vya afya. Lakini si dawa tu wangeangalia na maslahi ya watumishi hao. Kweli nafahamu tuna migogoro mingi, tuna madai mengi ya watumishi ambayo hawajalipwa na kwamba tunaweza tukawapelekea dawa na wakashindwa kutuhudumia ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia sehemu nyingine ya kwenye viwanda. Ninafahamu Wilaya yangu ya Kibiti kuna kiwanda cha kusindika samaki, lakini kiwanda hicho kimetelekezwa, hakifanyi kazi. Kwa hiyo ningeomba pindi tutakapoamua kuunda viwanda vipya tukifufue na kiwanda hicho cha Misati. Kiwanda hicho kipo Nyamisati, umeme umekwenda lakini maji bado hayajafika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia katika miundombinu ya barabara. Tunafahamu pindi tutakapopeleka viwanda hivyo sehemu husika tupeleke na mahitaji muhimu yakiwemo barabara, maji, umeme wenye uhakika ili mwekezaji atakapokuja kuwekeza sehemu husika basi ashawishike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuchangia ni ajira kwa vijana. Tunafahamu nchi yetu ina tatizo kubwa la ajira kwa vijana, ninaomba mamlaka husika itoe mikopo yenye riba nafuu kwa vijana ili waweze kujiajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningeomba vyuo vyetu vya VETA kijana anapohitimu apewe mtaji wa kuanzia maisha, badala ya kusubiria ajira ili ajiajiri mwenyewe hiyo itakuwa chachu ya kumletea kipato na familia yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo ningependa kuchangia ni katika ukusanyaji wa mapato wa Halmashauri. Nafahamu kwamba sasa hivi Halmashauri nyingi zimefunga mfumo wa kimashine, ningeomba TAMISEMI wafutilie kwa karibu mno kuhakikisha kwamba mapato ya Halmashauri hayapotei. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia katika michezo. Nafahamu sasa hivi mpira ni ajira. Naamini katika Wilaya zetu tungetoa kipaumbele kwa kujenga viwanja vya kisasa, wananchi wanaweza wakajiajiri wenyewe kupitia sekta hiyo ya michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuunga mkono hoja. (Makofi)