Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa inayokabiliwa na changamoto nyingi za afya kuanzia vijijini hadi manispaa. Kwa sasa kuna vituo vya afya 17 tu wakati tunatakiwa kuwa na vituo vya afya 117 ili kuhudumia wananchi wa kata 134 za Mkoa wote wa Singida. Sera ya Afya ya mwaka 2007 inatuelekeza kuwa na kituo cha afya kwa kila kata na zahanati kwa kila kijiji, hivyo hilo ni tatizo kubwa katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi waishio vijijini ambako kuna changamoto nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua katika kukabiliana na hali hii kuna vituo vya huduma za afya 69 ambavyo ujenzi wake uko kwenye hatua mbalimbali. Ninaomba Serikali iongeze nguvu kuhakikisha vinakamilika haraka ili tuokoe afya za wananchi wetu na kuendelea kujenga Taifa lenye watu wenye afya njema. Lakini nisisitize kwa Serikali kwamba ujenzi wa vituo hivyo uendane sambamba na uboreshaji wa usambazaji wa vifaa tiba pamoja na dawa muhimu kulingana na mahitaji, miundombinu, watumishi na maslahi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo kubwa la uhaba wa watumishi kwenye mkoa wangu wakiwemo Madaktari Bingwa hasa wale wa magonjwa ya akina mama ambapo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa peke yake inatakiwa kuwa na Madaktari Bingwa 32 lakini waliopo ni watano tu kwa mkoa mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida una upungufu wa watumishi wa afya wa kada mbalimbali 305. Hii ni idadi kubwa sana wakati vyuo vyetu vinazalisha wataalam kila mwaka. Ni kwa nini hawa wataalam tusiwasambaze kwenye vituo vyetu vyenye ukosefu wa wataalam?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuiomba sana Serikali yangu kuendelea kusimamia kwa haki na kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa kada ya afya ambao ni watu muhimu sana na wanafanya kazi kubwa sana na kwenye mazingira magumu. Watumishi wa afya wote wanaostahili kupandishwa madaraja na nyongeza za mishahara wapewe stahiki hizo kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwenye mkoa wangu kuna watumishi ambao hawajapandishwa madaraja kwa muda mrefu ikiwemo sababu ya Serikali kufanya uhakiki. Zoezi hilo limekwisha hivyo Serikali itimize wajibu wake. Zoezi hilo la kupandisha madaraja na maboresho ya mishahara yaende sambamba na mazingira bora ya kufanyia kazi kwa watumishi wa afya ambao wengi wao wa vijijini hawana makazi bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi hayana nyumba za watumishi, ofisi hazina hadhi, hivyo nina imani kubwa Mheshimiwa Ummy atauangalia Mkoa wa Singida ambao unapokea na kuhudumia wagonjwa wengi wakiwemo wanaopatwa na majanga kama ajali. Mkoa wetu unahitaji nyumba bora 1,072 lakini zilizopo ni 345 kwa mkoa mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naiomba Serikali kuangalia kwa umakini afya za wanawake na kutoa kipaumbele katika kupambana na ugonjwa hatari wa saratani ya kizazi na matiti ambao umekuwa tishio kubwa. Nashauri vianzishwe vitengo vya saratani kwenye Hospitali zote za Rufaa za Mkoa badala ya wagonjwa kujazana pale Taasisi ya Ocean Road ambayo ni ukweli kuwa imezidiwa sana. Umefika wakati sasa kuanza mikakati kabambe ya kudhibiti ugonjwa huo kuanzia ngazi za vijiji kwa kufanya upimaji na kampeni za uchunguzi wa mara kwa mara hasa maeneo ya vijijini ambako wagonjwa wengi hufika hospitalini wakati ugonjwa ukiwa umekithiri sehemu kubwa ya mwili wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nazindua kampeni yangu ya Kijana jitambue, wakati ni sasa ambayo ilitoa stadi za maisha kwa vijana kujitambua utu wao na mbinu za kujikwamua kiuchumi, tuliendesha pia zoezi la upimaji saratani ambapo wanawake wengi walipata fursa hiyo na wengine kubainika kuwa na tatizo hilo na kuelekezwa namna ya kupata huduma. Kwa hiyo, jambo hilo limejidhihirisha wazi kuwa wanawake wengi waliopo vijijini wameathirika na saratani ya shingo ya kizazi na matiti lakini wanakuwa hawajitambui kama wameathirika kutokana na kukosa huduma za awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya ya Mtanzania ndicho kitu muhimu cha kwanza kabisa kwani kama hatutakuwa na afya njema basi maendeleo ya nchi yetu yatazorota na kuwa nyuma, hivyo, Serikali inapaswa kuendelea kutoa kipaumbele kikubwa katika mapato yake katika Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ili kupunguza vifo vya akina mama na watoto ifike wakati sasa zahanati zetu na vituo vya afya viwe na wataalam wa kutosha, vifaa tiba vya kutosha na dawa za kutosha. Iwapo tutaimarisha huduma katika vituo vya afya na zahanati zilizopo zitasaidia sana kupunguza vifo vya akina mama na watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.