Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipatia afya nami kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa ni mnyimi wa fadhila kama nisipomshukuru Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli. Kwa kweli amefanyakazi kubwa na kazi nzuri na tarajio jema kwa wananchi wa Tanzania kwa maendeleo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuwashukuru Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wamefanya kazi nzuri ambayo sikutarajia kabisa katika kipindi hiki kifupi kuweza kuifanya kazi kubwa hii ndani ya afya katika nchi yetu. Wakati akisoma mdogo wangu Mheshimiwa Ummy taarifa yake ya Wizara, kwa kweli ameni-impress na kujua ya kwamba kumbe yeye ni bush doctor lakini kwa kweli ni daktari kamili, kwa jinsi anavyoifanya kazi yake kwa kuipenda na kuifahamu Wizara ya Afya na kweli ameishika na kuhakikisha kwamba anaifanyia kazi njema katika kipindi chake hiki cha uongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuzungumzia suala la maendeleo ya jamii. Kitengo cha Maendeleo ya Jamii kimesahaulika hivi sasa ndani ya utekelezaji wake wa kazi. Maendeleo ya jamii ilikuwa kila mwaka wanaketi Maafisa Maendeleo ya Jamii kukaa pamoja, kushauriana, kuelekezana na hatimaye kupeana ubunifu wa kuweza kuitekeleza Wizara yao, tatizo vikao hivi sasa hivi havifanyiki ikidaiwa kwamba bajeti ni finyu. Ninaomba vikao hivi virejee ili maendeleo ya jamii iweze kufufuka tena upya.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya jamii ni kitengo ambacho kinatoa elimu kwa akina Mama katika kuhamasisha ujasiriamali, kuwahamasisha akina mama kiuchumi, kuelekeza akina mama umuhimu wa kujiunga na tiba, umuhimu wa kujiunga na bima, umuhimu wa mikopo na namna ya utekelezaji wa mikopo hiyo ya vyombo vya fedha na SACCOS na kadhalika. Tatizo ni kwamba hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii hawana vitendea kazi, hawana usafiri na hata alivyozungumza Mheshimiwa Waziri ya kwamba wasitumie magari ya miradi ya UKIMWI na kadhalika, ajue wazi ya kwamba maendeleo ya jamii hawana usafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa hatuna usafiri, Wilaya zote hazina usafiri na hata ngazi ya Kata hawana usafiri hata wa pikipiki. Mimi ninavyoelelwa ni kwamba, Maafisa Maendeleo ya Jamii siyo desk officers, hawa ni field officers, wanahitaji kwenda kwenye maeneo, wanahitaji kupatiwa usafiri, vinginevyo watatumia nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri wana mambo mengi, wanawapa usafiri kwa kubahatisha, lakini wakiwa na usafiri wao watu wa maendeleo ya jamii watafanya kazi nzuri kwa wananchi wetu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninapenda kuishukuru Serikali yangu kwa kutoa ajira takribani kwa wananchi 52,000; ninaomba katika hawa 52,000 hebu tuangalie ajira ya Maafisa Maendeleo ya Jamii. Hatuna Maafisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Mkoa wetu wa Rukwa ndani ya kata 97 ukiacha zile zilizoongezeka tunao Maafisa 51 tu, tuna upungufu mkuwa wa Maafisa Maendeleo ngazi ya Kata, tuna upungufu mkubwa wa Maafisa Maendeleo ngazi ya vijiji na tunao upungufu mkubwa wa Maafisa Maendeleo wa Wilaya ya Nkasi na Wilaya ya Kalambo bado wana kaimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hawa Maafisa Maendeleo wa Jamii wa Wilaya ya Nkasi na Kalambo wapatiwe uthibitisho kamili wa Maafisa Maendeleo wa Wilaya yetu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni kuhusu suala la afya. Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Katavi tuko mbali na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ambayo iko Mbeya. Tumekubaliana Mikoa hii miwili tuweze kujenga hospitali ya rufaa kati ya Rukwa na Katavi na tumeweza kupata eneo la hekari 97 kuijenga hospitali hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa awamu ya awali imetupatia shilingi bilioni moja kwa maana ya kulipa fidia ya wananchi wetu waliokuwa katika lile eneo, ninashukuru sana kwa ngazi hiyo mliyoifikia. Kutokana na Halmashauri zetu kutokuwa na pato la kutosha, tunaomba Serikali Kuu iweze kuongeza hatua inayofuata ya uchoraji wa ramani na ujenzi wa hospitali ile iweze kuanzishwa katika Mkoa wetu wa Katavi na Mkoa wa Rukwa haraka iwezekanavyo ndani ya kipindi hiki tuweze kuifungua hiyo Hospitali ya Kanda ambayo ni hospitali ya Rufaa kwa Mikoa hii miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo linguine katika upande wa afya ni upungufu wa madaktari. Katika Hospitali ya Mkoa tunao madaktari 20, kati ya madaktari 20 tunaowahitaji tunao madaktari 12 tu ambao hawakidhi mahitaji. Upande wa Madaktari Bingwa, tunao madaktari watano lakini tuna uhitaji wa Madaktari Bingwa 15 waweze kukidhi pale. (Makofi)

Jambo lingine katika upande wa afya ni kuhusu vituo vya afya na zahanati. Tunazo zahanati na vituo takribani 54 ambavyo vimejengwa lakini bado havijakamilika. Tunaomba Serikali iweze kuhakikisha ya kwamba haya majengo ambayo hayajakamilishwa 54, zahanati zikiwa 48 na sita ikiwa ni vituo vya afya viweze kukamilishwa ili viweze kutoa huduma kamili na hatimaye kuondoa msongamano katika hospitali ya Mkoa ambayo hivi sasa ndiyo inaifanya hiyo kazi ili akina mama na watoto vifo viwe vichache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa vifo vya akina mama na watoto kwa kweli vimekithiri na tuna kila sababu ya kuweza kuhakikisha vinapungua kama siyo kuisha kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuzungumzia suala la 10 percent za Halmshauri; wakati TAMISEMI ikizungumza, ilisema kwamba itatoa waraka kupeleka kwenye Halmashauri kuhakikisha ya kwamba wanafungua mifuko na hizo fedha za asilimia 10 zinapatikana na zinagawiwa katika vikundi vinavyohitaji vya akina mama na vijana. Tunaomba waraka huo kutoka TAMISEMI utoke ili Halmashauri ziwe na uhakika wa kutoa hizi asilimia 10 na Wabunge wa Viti Maalum tupate hizo nakala za waraka huo ili tuweze kufuatilia hizi fedha kama zinatoka na kuwafikia walengwa wanaohitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalopenda kulizungumzia ni kuhusu ziara ya Mheshimiwa Waziri. Waziri alikuja Mkoa wa Rukwa bahati mbaya jioni yake akapata dharura ikabidi arudi Dar es Salaam na ziara yake ikafutika, hivyo tunamuomba Mheshimiwa Waziri urejee tena katika ziara yako ya Mkoa wa Rukwa ili uweze kufahamu changamoto za afya katika Mkoa wa Rukwa, kwa sababu Mkoa wa Rukwa hatuna hata Wilaya moja yenye Hospitali ya Wilaya, tuna Hospitali Teule tu, tunahitaji kuwa na Hospitali ya Wilaya.

Katika kuhangaika kutafuta hospitali ya Wilaya, tuliweza kuomba majengo ambayo yako chini ya TANROADS yaliyokuwa kambi ya kujengea barabara bahati mbaya inasemekana kwamba majengo yale ni madogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kutokana na juhudi uliyonayo Mheshimiwa Ummy na Mheshimiwa Kigwangalla, nina imani kwamba mtasimamia kuhakikisha Mkoa wetu wa Rukwa tunapata hospitali za Wilaya katika Wilaya zake zote nne ambazo kwa sasa hatuna hizo hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonekana ya kwamba Mkoa wa Rukwa tuko mwisho, tuko pembezoni, bila ya kuwa na afya bora itakuwa ni hatari, sisi ndiyo wazalishaji tunaowalisha katika nchi hii ya Tanzania. Hivyo tunawaomba kabisa kwamba tujaribu kuangalia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho katika upande wa afya ni huduma ya damu salama, akina mama na watoto ndiyo wanaohitaji kuhakikisha kwamba wanapata huduma salama na huduma salama ni damu, damu kwetu kuna tatizo la chupa za damu, sasa katika hizi chupa 250,000 sijui Mkoa wa Rukwa una kiasi gani cha hizo chupa, hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la pili ni kwamba, vituo vyetu vya afya havina majokofu ya kuhifadhi hiyo damu salama na wale wataalam wa kukusanya damu salama wengi wao hawajapata mafunzo, hivyo ni kwamba hawapo ambao wanaweza kukusanya damu salama na kuhakikisha kwamba wagonjwa wetu wanapata damu salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo tunawaomba mtoe mafunzo kwa wale wataalam wanaoshughulika na damu salama...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima napenda kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na big up.