Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nirekebishe jina siitwi Raphael Mbogo naitwa Taska Restituta Mbogo.
MWENYEKITI: Ahsante Restituta Mbogo.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nikushukuru kwanza wewe kwa kunipa nafasi hii kuchangia hoja hii ya Wizara ya Afya ambayo ni Wizara muhimu kwa sisi akina mama na ni Wizara muhimu kwa nchi yetu.

Napenda kwanza kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kasi yake ya hapa kazi. Ninasema hivi kwa sababu katika Mkoa wetu wa Katavi tulikuwa hatuna duka la dawa tangu labda niseme tangu Wilaya ile ianzishwe mwaka 1945.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata Mkoa hapa juzi, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipotembelea kule akatuahidi duka la dawa na ndani ya miezi sita duka la dawa la MSD lilikuwa limejengwa na tukaenda kulizindua, naipongeza sana Serikali.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kazi nzuri, kwa sababu baada ya uzinduzi tuliweza kupata pia vitanda, hivyo naishukuru sana Serikali hii kwa kasi yake ya ufanyaji kazi maana yake ndani ya miezi sita duka la dawa lilijengwa. Hongera Serikali yote, hongera kwa Mawaziri wote na hongera sana kwa Mheshimiwa Rais wetu na tunakupongeza sana endelea na kazi na hekima zako unazozitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda niende moja kwa moja kwenye hoja ya Wizara ya Afya. Ninampongeza Mheshimiwa Ummy na Naibu wake, naomba nitoe ushauri kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sihoji uwezo wao wa Watendaji wanafanya kazi vizuri sana akiwepo mwenyewe Mheshimiwa Ummy na Naibu wake, lakini naona Wizara hii ni kubwa, naona kama vile upande wa maendeleo ya jamii, wazee, unasahaulika. Naomba kutoa ushauri kwa Serikali iweze kuigawa Wizara hii, Wizara ya Afya ibaki peke yake, Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Wazee itenganishwe na hii Wizara, huu ni ushauri tu nautoa maana Wizara ya Afya ina mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye dawa hospitalini Waziri na Naibu wake washughulikie, zahanati, vituo vya afya, hela za mgao kwenda kwenye Mikoa yote mpaka Wilaya, vifaatiba kuangalia japokuwa ndiyo tunasema viko TAMISEMI, lakini Waziri pia anatupia jicho, yote hayo yanamkabili Waziri wa Afya na Naibu wake, naona kama vile kazi inakuwa kubwa mno. Natoa ushauri tu kuomba Wizara ya Afya ingeachwa peke yake ili iweze kutoa huduma vizuri kwa sababu kila Mtanzania bila kuwa na afya njema sidhani kama kuna kitu ambacho mtu anaweza akafanya. Hata hapa tunakaa kwa sababu tuna afya, ukiwa na afya iliyotetereka sidhani kama utaingia humu Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niongelee sakata la vyeti fake. Ninavyoongea hapa kule Mkoani kwangu Katavi kuna Halmashauri Tano, ndani ya hizo Halmashauri tano wafanyakazi 60 wa Wizara ya Afya walikuwa na vyeti ambavyo vinasemekana kwamba havijakaa vizuri au ni vyeti fake. Sasa tuna uhaba wa wafanyakazi 60 ghafla kwenye Mkoa wetu wa Katavi, tunaomba replacement. Uajiri wafanyakazi kama wafanyakazi wapya madaktari pamoja na wauguzi, hili limewakumba madaktari pamoja na wauguzi. Mkoa mzima kupoteza wafanyakazi wa sekta ya afya 60 ni wengi mno, utaangalia mwenyewe jinsi gani vituo vya afya, zahanati na hospitali zetu zitakavyokosa huduma na jinsi gani wananchi wa Mkoa wa Katavi watakavyokosa huduma. Naomba ajira iharakishwe ya hawa madaktari, Serikali jinsi ambavyo imezungumzia suala la vyeti fake basi wakamilishe huo utaratibu na ajira mpya za wale madaktari pamoja na wauguzi wenye vyeti ambavyo ni genuine iweze kutangazwa mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala la Kituo cha Afya cha Mkoani Katavi. Mheshimiwa Waziri kile kituo cha afya ambacho mwaka jana tulisimama hapa tukaomba kirekebishwe na kifanyiwe ukarabati, napenda kushukuru Serikali kituo cha afya kimefanyiwa ukarabati kimekwisha, tatizo hakijafunguliwa. Namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho yake atuambie kile kituo cha afya cha Mkoa wa Katavi ambacho kimekwisha kitafunguliwa lini?

Naomba pia kile chuo cha afya kiweze pia ku-train wauguzi wasaidizi ili tuweze kuwa na ma-nurse wengi na hawa Medical Assistants wengi ambao watakuwa wamekuwa trained Mkoani Katavi, kwa sababu ukiangalia jiografia kule kwetu ni Mikoa ambayo iko pembezoni lakini kama mtu atakuja atasoma kule ile miaka miwili atazoea mazingira kiasi kwamba hata kama atapangiwa kufanya kazi katika Mkoa wa Katavi atakaa. Ukimtoa mtu Mikoa ya mbali ukamleta kule anaweza akaona jiografia ni mbaya na hiyo kazi yenyewe asiipende kwa hiyo naomba kile chuo pia kiweze kuwa-train wauguzi wasaidizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la ndoa za utotoni. Sheria zetu tulizojipangia wenyewe katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaweza ukasema kwa upande mwingine zinachangia ndoa za utotoni. Tunazo sheria ambazo zinakinzana, tunayo Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo ibara ya kwanza inasema kwamba mtu yeyote ambaye yuko chini ya umri wa miaka 18 ni mtoto. Ibara ya kwanza hiyo ambayo ni ya Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inasomeka hivyo. Ukienda kwenye Sheria za Kimataifa ambazo tumeziridhia tunayo Sheria ya Kimataifa ya Mwanamke ambayo inatoa tafsiri ya umri wa mtoto na tunayo mikataba ambayo imeonesha umri wa mtoto ni miaka mingapi. Ukichukua zile sheria ambazo tumezisaini na tuliziridhia ambazo tunatakiwa tuzifuate zinakuja zinakinzana na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1970 ambayo inamruhusu mtoto wa kiume kuoa akiwa na miaka 18 na mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa unakuta kwamba kunakuwa na discrimination, ukishaweka ile tofauti ya age, moja kwa moja umeweka utofauti wa mtu mmoja kuwa supreme na mwingine kuwa chini yake kwa ajili ya jinsia. Kama unataka kuwaweka watoto wote kuwa sawa, unatakiwa ule umri usiweke ile tofauti kati ya mtoto wa kike na mtoto wa kiume. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.