Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Kemirembe Rose Julius Lwota

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kukushukuru kwa kuweza kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa kabisa anayoifanya na Watanzania wote wanaona, ninampongeza Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri wote kwa kazi kubwa wanazofanya na niwatie moyo ninawaambia wakaze buti, wapige kazi, hapa kazi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza pia Mawaziri Dada yangu Mheshimiwa Ummy na Naibu wake Mheshimiwa Kigwangalla kwa kazi kubwa wanazofanya, wametuletea ambulance kwenye Mkoa wetu wa Mwanza, wametupatia fedha za dawa, lakini hizi fedha za dawa mlizotupatia ni fedha ndogo hazitoshi, bado kuna baadhi ya vituo vyetu vya afya vina upungufu wa dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuzungumzia ni suala la vifo vya akina mama na watoto. Hili ni janga na naomba kama Serikali tulichukulie kwa umuhimu wake na tulipe kipaumbele. Kila siku ya Mungu akina mama kati ya 24 mpaka 30 wanapoteza maisha yao kutokana na uzazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watoto kati ya 170 mpaka 180 kila siku ya Mungu wanapoteza maisha kwa sababu ya vifo vitokanavyo na uzazi. Ninashukuru katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumza na amesema tukimpitishia bajeti hii itakuwa ni muarobaini wa haya masuala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu, mwaka 2000 kwa kila vizazi hai 100,000 vizazi 529 vilikuwa vinapotea, mwaka 2005 kwa kila vizazi 100,000 vizazi 578 vilikuwa vinapotea, mwaka 2010 vikapungua vikafika 454 na sasa kwa bahati mbaya mwaka 2015/2016 vizazi hivi vimeongezeka kwa kila vizazi 100,000 tunapoteza watu 556, hili ni janga na ninaomba sana Mheshimiwa dada yangu Ummy tulifanyie kazi hili ili tuweze kuepusha vifo hivi, akina mama hawa wakiwa wanatimiza wajibu wao wa msingi kabisa wa kupata watoto, kwa bahati mbaya vifo hivi vinatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifo vingi vya akina mama hawa vinatokana na mambo makuu manne, jambo la kwanza ni upungufu wa damu, damu salama ya kuongeza akina mama hawa inakosekana akina mama hawa wanapoteza maisha. (Makofi)

Jambo la pili ni uzazi pingamizi, akina mama hawa wanapotakiwa kwenda kufanyiwa upasuaji zahanati wakati mwingine ziko mbali, zilizopo karibu hazitoi huduma ya kupasua akina mama hawa wanapoteza maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kifafa cha mimba, Mheshimiwa Ummy ameongelea na tiba ni sindano za magnesium sulphate. Ninaomba sana katika vituo vyetu vya afya mambo haya yawepo ili tuweze kuokoa vifo vya akina mama. Mimba za utotoni na kuharibika kwa mimba, akina mama hawa mimba zinaharibika wanaenda kwenye zahanati zetu hatuna vifaa vya kusafisha hizi mimba na hii inasababisha vifo kwa akina mama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la upungufu wa wataalam kwenye sekta ya afya, Mheshimiwa Waziri amesema kuna ajira mpya kwenye sekta ya afya lakini ni janga kubwa kweli, hatuna wafanyakazi wa afya wa kutosha. Naomba hili suala tuliangalie na tuajiri wafanyakazi wa afya ili tuweze kuokoa maisha ya Watanzania hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nilisimama hapa na nikaongelea suala la vifaatiba. Hospitali yetu ya Sekou Toure kubwa kabisa ya Mkoa wa Mwanza hatuna CT Scan, tumeomba hapa Mheshimiwa Waziri akaahidi akasema CT Scan hii inakuja lakini mpaka sasa ninavyosimama na kuongea hapa CT Scan haipo. Hii inapelekea Watanzania wa Mkoa wa Mwanza waende kufanya vipimo hivi kwenye private clinics. Private clinics vipimo hivi ni kati ya shilingi 300,000 mpaka 400,000, ni aghali na Watanzania wengi hawawezi kumudu fedha hizi kuzilipa.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunaomba unapokuja hapa kuhitimisha utuambie ni lini vifaatiba hivi vitaenda kwenye Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la watoto njiti sijaliona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Watoto wanaozaliwa njiti ni wengi katika wodi yao, nimetembelea wodi yao Mkoa wa Mwanza, wodi haina vifaa. Watoto njiti hawa wanahitaji suction machines, wanahitaji blood pressure monitors, wanahitaji incubators ili waweze kuwekwa na kuhifadhiwa ili waweze kufika siku zao za kuweza kuruhusiwa na kwenda nyumbani, lakini inabidi watoto hawa waruhusiwe kwa sababu wodi ya watoto hawa haina vifaa. Mheshimiwa Waziri tunaomba sana uweze kutupatia vifaa hivi, wananchi na akina mama hawa wanahangaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la D by D, concept yake ni nzuri kabisa haina tatizo, lakini inatokea mkanganyiko kati ya Wizara ya Afya na TAMISEMI. Naomba ifike mahali sasa Wizara ya Afya isimame kama Wizara ya Afya. Tunapokuwa kwenye Halmashauri zetu huko tunauliza hili suala la afya mbona halifanyiki, mbona haliendi, tunaambiwa hili suala lipo TAMISEMI, ukienda TAMISEMI unauliza unaambiwa hili suala lipo Wizara ya Afya, sasa tufike mahali tuone ownership iko wapi na tujue Wizara ya Afya isimame kama Wizara ya Afya na tu-deal na Wizara ya Afya, peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba hii tumeona fedha zilizotengwa za dawa ni zaidi ya shilingi bilioni 230, kiuhalisia fedha za dawa zilizoenda ni shilingi bilioni 88 tu, nyingine zinaenda kwenye kusafirisha dawa, kwenye kujenga majengo, kwenye vifungashio, tungejua kabisa specific hela za dawa zimetumika...(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana kwa mchango wako.