Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon Faida Mohammed Bakar

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia pumzi hadi kufikia siku ya leo na tunawaombea maghufira ambao wametangulia mbele ya haki, Inshallah. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi sana kwa Serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na chama changu kitukufu Chama cha Mapinduzi. Na pia, napenda kuipongeza Serikali yangu ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Dkt. Shein, na vilevile kumpongeza Rais wangu Magufuli kwa jitihada kubwa ambazo anazichukua katika nchi hii, na kwamba ametujali sisi wanawake kwa kumteuwa Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza jembe! Huyu ni jembe kabisa! Huyu ni Mheshimiwa dada yangu Ummy, napenda kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kushirikiana na Naibu wake Dkt. Kigwangalla. Hawa ni viongozi bora sana na wanaiweza Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napenda kuongelea Benki ya Wanawake. Hii Benki ya Wanawake kila ninaposimama ninaitetea. Kwanza naipongeza kwa sababu imefanya kazi kubwa sana. Mheshimiwa Waziri ameongea kwamba shilingi 12,000,000,000 zimetolewa kwa wajasiriamali mbalimbali 9,650 katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Njombe, Iringa, Dodoma, Ruvuma, Pwani na Mwanza, lakini kila nikisimama najiuliza, napata wivu sana mimi nasema kwa nini hii Benki ya Wanawake na Zanzibar isiwepo? Hii Benki ni ya Wanawake wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii benki si ya Dar es Salaam wala si ya Mwanza wala si ya Songea wala si ya sehemu moja tu, hii ni Benki ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba Mheshimiwa Ummy uniambie leo, kila nikikuuliza unaniambai sijui hazijatolewa pesa milioni ngapi, kwani hii kazi ya kutoa hii pesa ni ya nani? Si iko katika bajeti ya Wizara yako? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naomba mshirikiane na Serikali na Wizara ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kule, mshirikiane Mheshimiwa Ummy, mimi sitapenda kusimama hapa tena kuiongelea Benki hii ya Wanawake wa Zanzibar.

Zanzibar kuna wanawake kama sehemu nyingine yoyote, Zanzibar kuna wanawake ambao ni wafanyabiashara kama sehemu nyingine yoyote, Zanzibar ni wapiga kura wakubwa wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba leo iwe mwisho, Mheshimiwa Ummy, naomba leo iwe mwisho wewe ni mwanamke mwenzangu naomba unisikie. Nasema mwisho iwe leo, la kama mimi sitajibiwa leo hapa kama Benki ya Wanawake itaanza shughuli zake Zanzibar, mimi na wewe tutakuwa hatuelewani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukatili dhidi ya watoto wa kike na wa kiume. Wote hapa ni mashahidi juu ya mambo yanayotokea katika dunia yetu hii, si hapa tu dunia nzima wanawake, na watoto wanadhalilishwa, wengi wa watoto wanadhalilika; wengi wa watoto jamani ni mashahidi kwenye whatsApp siku hizi mengi. Utaona mtoto kakatwa mkono, sijui kakatwa mguu, kakatwa kichwa; wanadhalilika watoto; kwa nini watoto wanadhalilika Mheshimiwa Ummy Ally Mwalimu kwa nini watoto wadhalilike? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kama Wizara yako inajitahidi katika kuwatetea watoto wa kike na wa kiume, lakini bado. Tunaomba watoto wa nchi wasidhalilishwe kwa sababu watoto ndio Taifa letu la kesho. Mheshimiwa Ummy Ally nakuomba sana maafisa wako wafuatilie sana habari kama hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo linajitokeza jamani, mimi naomba kusema tu ukweli, unanua sipendi kufichaficha. Watoto wanadhalilishwa kijinsia jamani ninyi hamjui wenzangu ninyi? Watoto wanadhalilishwa kijinsia, mimi nimekwenda kufanya ziara Mkoa wa Kusini Pemba, kila ninapokwenda wananiambia Mheshimiwa Mbunge tunalalamika watoto wetu washaharibika, watoto wameshaharibiwa, kwa nini baba mtu mzima uende kumharibu mtoto mchanga? Mtoto mdogo anayesoma shule, wa kike na wa kiume, kwa nini jamani? Nililia watoto wanadhalilishwa, wanaharibiwa maumbile yao jamani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, turudi kwa Mwenyezi Mungu binadamu, akina baba nawaomba hii si nzuri. Mheshimiwa nasema kwa uchungu kwa sababu mimi ni mzazi Mheshimiwa Ummy, watoto wanabakwa na wanadhalilishwa. Sitaki niseme mengi leo, nikisema nitalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wa Kusini Pemba walinililia wakasema watoto wetu wanadhalilishwa mpaka shule kule, na kuna baadhi ya walimu wanawadhalilisha watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani inakuwa hivi? Watoto wetu tunawazaa wenyewe watoto, mtu babu eti anakwenda kumfanyia ushenzi mjukuu wake! Eeh! Baba aliyemzaa mtoto anamgeuka, kwa nini? Turudi kwa Mwenyezi Mungu sisi binadamu, si nzuri, inatisha. Tanzania hii inatakiwa iwe ya amani na utulivu na upendo, kwa nini tunabadilika? Tumeacha dini sasa hivi tunahururika na dunia tunafanya mambo ya ajabu binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimba za utotoni. Baba mtu mzima anakwenda kumjaza mimba mtoto; Sheria ya Ndoa irekebishwe, iletwe Bungeni tuirekebishe sheria hii, haikubaliki, watoto wanadhalilika wanapigwa mimba na watu wazima walio na madevu yao mengi tu, wanawadhalilisha watoto. Hii haikubaliki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wengine wanawaozesha watoto umri mdogo kwa sababu ya visenti, kwa sababu ya ng’ombe. Kwa nini tunafanya hivi binadamu? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto tuwajali na tuwatunze. Watoto ndio watakaokuja kutusaidia sisi, tusijione vijana kesho kutwa sisi tutakapozeeka na tutakapokuwa hatujiwezi wao watatusaidia; kwa nini tunafanya hivi?

Mheshimiwa Waziri nakuomba ulisimamie, na anayepatikana na hatia hii achukuliwe hatua kali, naona bado hatua hazijachukuliwa kali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazee wetu, mzee wa mwenzako ni mzee wako, leo wewe mzee wa mwenzako unamdhalilisha. Kuna makabila mbalimbali wanawanyanyasa wazee kwa sababu ya kuona kwamba ni washirikina, wazee wakiwa na macho mekundu wanawaua; nashukuru Serikali siku hizi inajitahidi sana katika hili; na kuwaua ma-albino; nashukuru sana sasahivi Serikali imejitahidi, lakini tusichoke na tuone kwamba wadhalilishaji wa wazee wamo. Tuwalinde wazee, wapewe vituo vyao, nyumba zao ziwe safi, wapewe lishe kwenye vyakula vyao na vile vile walindwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mzee wa mwenzako ni mzee wako tusijione leo vijana, sisi wenyewe tutakuwa wazee na tutataka kuhudumiwa. Ukiwaona saa nyingine unalia wazee nyumba wanazolala zile. Vituo vile Mheshimiwa Ummy jitahidi, vituo hata kama… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.